Wednesday, July 30, 2014

TAMASHA LA USIKU WA MATUMAINI 2014 WABUNGE SIMBA NA YANGA FULL KUKANYAGANA UWANJA WA TAIFA


Makala na Nassor Gallu
SIKU ya Agosti 8, mwaka huu kutakuwa na bonge la mechi litakalopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo wabunge wanaoshabikia Yanga, watakuwa dimbani kupepetana na wenzao wa Simba.

Wabunge wa timu ya Simba wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Hebu jaribu kuvuta picha katika ubongo wako, waheshimiwa wabunge watakapoweka kando masuala ya ‘Ukawa’ na ‘Tanzania Kwanza’, kisha kukutana katika uwanja kuonyeshana umwamba kwa kusakata gozi la ng’ombe katika  mchezo huu wa kihistoria.
Kila timu tayari imeingia mafichoni kujiwinda na mchezo huo ili kuhakikisha inaibuka kidedea na kujenga heshima mbele ya watani wao huku Simba wakiahidi kulipiza kisago cha bao 1-0 walichokipata mwaka jana kutoka kwa Yanga.
“Tayari tumeingia kambini kujiwinda na mchezo huu ili kuziba midomo na kelele za Yanga ambao wamekuwa wakitamba tangu watubahatishe mwaka jana,” alijinasibu Hamis Kigwangala ambaye ndiye nahodha wa Simba.
Kwa upande wa mlezi wa Yanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abassi Mtemvu, alijigamba kuwa ni lazima waendeleze moto wa ushindi kwa kuwa wapo na kikosi imara na tayari wameshaingia kambini kwa kuwa mchezo huu ni siriazi kwao.

“Kwa kweli mchezo huu tumeuchukulia kwa mtazamo wa juu kabisa na lazima tuwapige kwa kuwa tuna damu changa nyingi, hatuna masihara, maana wakitufunga hatutakaa bungeni.
“Tupo katika maandalizi ya mwisho kwa sasa ingawa tulipoweka kambi yetu itabaki kuwa  siri,” alisema Mtemvu kwa kujiamini.

Baadhi ya wabunge wanaounda timu ya Yanga ni pamoja na Abassi Mtemvu, Ridhiwani Kikwete, Freeman Mbowe na  Mwigulu Nchemba, huku kikosi cha Simba kikiundwa na wakali kama Zitto Kabwe, Hamisi Kigwangalla, Wiliam Ngeleja, Juma Nkamia, Amos Makalla na Ismail Aden Rage.
Mbali na mchezo huo ambao utakuwa kivutio kikubwa kwa wadau wa soka, pia kutakuwa na mchezo mwingine wa kusisimua pale Bongo Fleva chini ya mkali wao, Peter Manyika itakapopepetana na Bongo Movie FC chini ya Jacob Steven JB.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Bongo Movie, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, tayari ameanika wachezaji wake huku akisema kuwa hahofii kwani kikosi chake kipo kamiligado kuelekea mchezo huo ambao wameuchukulia kwa umakini mkubwa.
“Sisi tumeuchukulia ‘serious’ sana mchezo huu kwa kuwa mashabiki wetu watakuja wengi na hatutakubali kuwaangusha.“Wachezaji waliopo kambini mpaka sasa ni Mzee Majuto, Kingwendu, Bambo, JB, Steve Nyerere, Dk Cheni, Ray, Mtitu, Cloud pamoja na Muhogo Mchungu,” alisema Bi Mwenda.
Wabunge wa timu ya Yanga wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Akijibu mapigo ya wapinzani wao, kocha wa Bongo Fleva ambaye pia anakinoa kikosi cha Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’, alisema Bongo Movie wajiandae kupata kipigo cha mshangao kwa kuwa wao hawatakwenda kuigiza uwanjani.
“Hawa waigizaji wajiandae na kipigo cha ‘sapraizi’, maana pale sisi hatuendi kuigiza, tunaenda kupiga kazi kwa kuwa mpira hauigizwi, unachezwa kila mmoja anaona, sasa acha wapige domo wataona kitakachowakuta,” alisema Pondamali.
Baadhi ya mastaa wanaounda kikosi cha Bongo Fleva ni pamoja na Peter Manyika, H-Baba, Ali Kiba, Rich One, Kalapina na wengineo.
Ukiachana na soka, pia kutakuwa na burudani mbalimbali ambapo mastaa kibao kutoka ndani na nje ya nchi watakuwepo kulipamba jukwaa la Usiku wa Matumaini.
Baadhi ya mastaa hao ni pamoja na Yemi Alade kutoka Nigeria, Madee, Ali Kiba, Roma Mkatoliki, Shilole, Menninah, Juma Nature na kundi zima la TMK Wanaume Halisi.
Mgeni rasmi katika tamasha hili atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal.Tamasha la Usiku wa Matumaini limedhaminiwa na Clouds FM (88.5),  Times Fm (100.5), Vodacom, Pepsi, Azam TV pamoja na Syscorp.
JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS

No comments: