Monday, July 21, 2014

hoja ya haja: Tamko la Jumuiya ya Kikristo Tanzania Linaturudisha Nyuma

Barua ya Wazi kwa Uongozi wa CCT juu ya Tamko la Mapatano ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 48 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania la tarehe 3 Julai, 2014.


   Sio la Kiponyaji, linatonesha Madonda
   Watu wa Mungu hawategemewi Kupotosha, Labda Wamepotoshwa


Na John Nkhundi
 Si kawaida yangu kulumbana na viongozi wa dini kwa sababu ya heshima waliyonayo katika jamii na matumaini ya waumini wao kwao.  Hata hivyo, leo nimelazimika kuandika baada ya kusoma tamko la Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) lililotolewa na Mkutano wa Halmashauri Kuu iliyokutana tarehe 3 Julai, 2014 ambalo maudhui yake ni ya kisiasa na limesheni mambo ya dunia.

Tamko hilo lililopewa jina la "Tamko la Mapatano ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 48 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania wa Julai 2-3, 2014" limenistua kwa mambo makubwa matatu. Mosi, tamko hili limetolewa Julai 3, 2014 lakini likatolewa magazetini tarehe 15 Julai,2014 tena katika gazeti moja tu la Mwananchi. Mtiririko huu wa matukio yaani muda wa Tamko lilipotolewa na muda lilipochapishwa kunatia mashaka ikiwa ni jambo la kimkakati au nasibu tu. Zaidi, upana huu wa muda kati ya lilipotolewa na kuchapishwa kunaleta pia wasiwasi kuhusu uhalisia wa tamko lenyewe. Maana, kwa kawaida matamko ya aina hii hutolewa mara tu Mkutano unapoisha, tena kwa kusomwa mbele ya waandishi wa habari.

Safari hii, hali ni tofauti maana tamko limechapishwa gazetini, wiki mbili baada ya kutolewa, tena bila ya jina la aliyelitoa zaidi ya jina la jumla yaani "imetolewa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania".  Aina hii mpya ya utoaji wa Tamko inatoa mwanya wa kuhisi kuwa pengine tamko hili si rasmi na limechakachuliwa kwa lengo mahsusi la aliyelivujisha. Maana ukilisoma kwa makini, halionekani kuandaliwa kwa ajili ya umma bali kumbukumbu tu.  Wanaoweza kututoa kwenye kitendawili hiki ni CCT wenyewe.

Pili, lugha yenyewe ya tamko na maudhui yenyewe ya Tamko yamesheheni siasa na sio utume. Usiposoma kichwa cha habari na hitimisho, unaweza kudhani limetolewa na chama cha siasa au wanaharakati.  Hii inajidhihirisha hata jinsi ambavyo Mhariri wa gazeti la Mwananchi alivyolitafsiri katika Toleo Na. 5105 lenye kichwa cha habari tena cha ukurasa wa mbele, yaani "Tamko Zito kwa Kikwete". Tamko hili haliponyi bali linatonesha madonda, jambo ambalo si kawaida kuliona katika tamko la watu wa Mungu,

Maudhui ya tamko yamesheheni historia na sio wakati ujao. Ni tamko lenye kuhukumu na sio kubariki, lenye kubomoa na sio kujenga. Ni tamko lililojaa lawama na sio toba, lililojaa chuki na sio upendo. Tamko linazungumzia madonda ambayo taifa imeyapitia, tamko halisherehekei maridhiano yaliyofikiwa kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar iliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na vurugu za chaguzi na kisiasa zilizozaa mchakato wa Katiba mpya. Tamko limelaumu pia, kupanuka kwa pengo kati ya maskini na matajiri, maadili ya viongozi wa umma na kuibuka kwa itikadi kali za kidini.

 Haya yote kwa kiasi kikubwa yanaashiria pia kupwaya kwa baadhi ya viongozi wa katika majukumu yao ya kulilea taifa kiroho. Maana sote tu mashuhuda namna ambavyo mafisadi, wala rushwa wanavyopokelewa makanisani na misikitini, na fedha zao zinavyobarikiwa kwenye harambee. Tumeshuhudia viongozi wa dini wakitenda maovu, tena makubwa yasiyofikirika. Isitoshe, suala la itikadi kali za kidini, zinachochewa na tamko kama walilolitoa CCT, ambalo limeacha misingi ya imani na kujiingiza katika uanaharakati na siasa. Tamko hili linanistua sana kwa kuwa hata viongozi wa dini nao sasa wanaonekana kuambukizwa ule ugonjwa wa watu wa kumlaumu kila mtu kwa mapungufu yao isipokuwa wao wenyewe.  Kaugonjwa haka ka kulaumu na kulalama kametamalaki kwenye siasa, nilikuwa na matumaini kuwa viongozi wa dini watatusaidia kukaponya, la hasha. Kama tumefika hapo, basi taifa linahitaji uponyaji mkubwa. Kitakachotutoa hapa ni maombi na dua tu.



Tatu, Tamko lina upotoshaji mkubwa kuhusu mchakato wa Katiba. Upotoshaji wenyewe ni wa dhahiri kuhusu mamlaka ya Rais kwenye Sheria ya Katiba juu ya uteuzi wa Wajumbe wa Tume na  Rasimu. Tamko linasema kuwa Rais aliwateua wajumbe wa Tume na hivyo aliwafahamu vizuri, kuwaamini na kuwaapisha. Linakwenda zaidi kusema kwamba Tume ilimshirikisha Rais katika kila hatua na kuwa kilichotolewa na Tume walikubaliana kwa pamoja na Rais. Hawakuishia hapo, Tamko likasema, "Tunaamini kuwa kile kilichoandikwa katika Rasimu ya Pili kilikubaliwa na mwenye kutoa hoja yaani Mheshimiwa Rais na hivyo akaagiza Rasimu hiyo itolewe kama ilivyo kwani aliamini kuwa huo ndio uamuzi wa wananchi wengi kuhusu katiba wanayoitarajia. Pia tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja alikuwa na uwezo wa kuzuia Rasimu hiyo isitolewe endapo kuna ibara ambayo ina mwelekeo ambao ungekuwa hatari kwa mustakhabali wa taifa letu".

Tuhuma hizi ni nzito sana haswa zinapotolewa na viongozi wa dini, tena Jumuiya ya Kikristo Tanzania. Inaniwia vigumu sana kuishuku CCT kuwa imepotosha makusudi. Hivyo, napenda kuamini hilo halikuwa lengo lao ila wamepotoka tu, au wamepotoshwa. Naweka akiba ya kutowatuhumu maana neno walilotumia zaidi ni "Tunaamini" jambo linalonipa faraja pengine walisukumwa na imani tu bila utafiti na taarifa sahihi. Ni kwa sababu hiyo nimeona niandike kwa ajili ya kuwasaidia zaidi kuhusu hili suala la tatu, kwa imani kwamba, watu wa Mungu walighafirika, na wakiigundua kweli itawaweka huru.

Mchakato wa Katiba unatawaliwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.  Sheria hii ndio rejea ya kila kinachofanyika katika mchakato huu. Moja ya sababu kubwa ya kuwa na sheria hii ni kuondoa mamlaka ya Rais na Serikali kuhodhi mchakato wa Katiba kwa kuepusha mgongano na mwingiliano wa maslahi. Katika mchakato wa Katiba, jukumu la serikali ni la kiuwezeshaji tu, sio hata la kiuratibu. Ukiisoma Sheria hii, Rais amedhibitiwa katika kuteua wajumbe anaopendekezewa na Makundi,  hana mamlaka ya kuingilia Tume, kazi ya Tume wala  kuibadilisha hata kuizuia Rasimu ya Tume kuwasilishwa Bungeni.   Pia, Sheria inaweka wazi kuwa Rasimu ya Tume haitokani na maoni ya wananchi pekee kama CCT wanavyojaribu kuamini na kuaminisha umma.

Ukiisoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 6 (6) inaelezea kuwa "Rais ataalika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini,asasi za kiraia, jumuiya, taasisi zisizo za kiserikali na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kuwasilisha orodha ya majina ya watu ili kuteuliwa kuwa wajumbe".  Ibara ndogo ya 1 hadi 3 ya Ibara ya 6 imeainisha kuwa Rais kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar watateua wajumbe kwa kuzingatia uzoefu, jiografia na mtawanyiko wa watu, umri, jinsia  na uwakilishi wa makundi mbalimbali kwa jamii. Hivyo, si kweli hata kidogo kuwa Rais aliteua watu kama alivyojisikia, na hivyo si sahihi kusema kuwa wajumbe wa Tume hawawezi kuwa na msimamo tofauti na Rais. Sheria hii kwa makusudi imeainisha makundi ili kutuepusha na uwezekano wa Rais kuteua watu wenye mawazo tu ambayo yanayompendeza yeye. Ndio sababu, uteuzi wa wajumbe wa Tume ulipokelewa vizuri na watu na makundi yote.

Suala la mamlaka ya Tume na uhuru wa Tume  limefafanuliwa vizuri katika Sura ya 10 inayotamka kuwa, "Tume itakuwa na mamlaka na uhuru kwa kadri itakavyokuwa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na mamlaka yake chini ya Sheria hii na haitaingiliwa na mtu au mamlaka yoyote". Ukiangalia kifungu hiki, hakuna namna yoyote Rais angeweza kuingilia kazi ya Tume. Hata pale ambapo Tume ilimshirikisha Rais ilifanya hivyo kwa utashi wake tu sio kwa shurti, na pengine kwa kutaka maoni au ushauri wake ambao pia hawakubanwa kuukubali au kuuchukua. Hivyo, sio sahihi kuhitimisha kuwa, kwa kuwa Mwenyekiti wa Tume alikutana kwa mashauriano na Rais katika nyakati mbalimbali, hivyo Rais ni sehemu ya majumuisho ya kazi ya Tume au Rasimu ya Tume. Kusema kuwa Rais ameikana Tume ni kupotoka, maana hakuwa na fursa ya kukubaliana na Tume. Rasimu ya Katiba ni ya Tume, na sio zao la muafaka kati ya Tume na Rais.

Tamko la CCT limeibua hoja nyingine kuwa, Rais alikuwa na mamlaka ya kuamua kutopeleka Bungeni Rasimu ya Katiba ya Tume kama asingeridhishwa na kipengele au ibara katika Rasimu ile. Hili nalo halihitaji maelezo mengi, maana Sheria imefafanua kinagaubaga kuwa dhima, ya Rais si kuihakiki Rasimu bali kuipokea na kuelekeza iwasilishwe Bungeni. Ibara ya 20 (1) ya Sheria ya  Marekebisho ya Katiba inatamka wazi kuwa,"Baada ya kukamilisha kazi yake, Tume itawasilisha ripoti kwa Rais na Rais wa Zanzibar.  Ibara ya 20(2) inaendelea kufafanua kwamba, "Rais, ndani ya siku thelathini na moja baada ya kupokea ripoti, atachapisha Rasimu ya  Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kwa ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa".  Hakuna mahala ambapo Rais, wala Rais wa Zanzibar wamepewa jukumu la uhariri au uhakiki wa Rasimu.

Hivyo, Sheria inamtaka Rais aelekeze Rasimu iwasilishwe  Bungeni bila kujali Rasimu hiyo imempendeza au kumchukiza. Jukumu la kuondoa au kurekebisha kipengele kinachoudhi au kukwaza halikuwekwa mikononi mwa Rais bali Bunge la Katiba.  Bila shaka waliotunga Sheria waliongozwa na busara kuwa Tume ya Katiba haiundwi na malaika na hivyo inaweza kuleta rasimu yenye makosa au mapungufu. Zaidi, ikaona mbali kwamba jukumu la kuiboresha likasimishwe Bunge lenye uwakilishi mpana wa jamii na sio Rais  katika ile dhana ya kutoa mamlaka ya kutunga Katiba kutoka kwa watawala kwenda kwa wananchi. Ndio sababu, kilele cha mchakato huu wa Rasimu ya Tume, sio Bunge la Katiba bali kura ya wananchi. Tunachokiona katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambacho ni kizuri ni kule kupanuka kwa ushiriki mpana wa wananchi katika kila hatua ya mchakato wa Katiba. Yaani, maoni ya wananchi waliojitokeza, kwenda kwenye mabaraza ya Kata, Bunge la Katiba na hatimaye Kura ya maoni.

Binafsi napata sana tabu na maelezo ya CCT tena yenye kuhitimisha kuwa Rasimu ya Tume ya Katiba ndio maoni ya wananchi. Upotoshaji huu ndio unaozaa hoja kuwa Rasimu ijadiliwe kama ilivyo, na isibadilishwe katika ngazi ya Bunge ambayo ina uwakilishi mpana kuliko ule uliozaa Rasimu ya Tume. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Ibara ya 9(1) a-d inaeleza wazi majukumu ya Tume yatakuwa ni "kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora ; kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na kuandaa na kuwasilisha ripoti.

 Aidha, Ibara ya 19(1) inatamka ifuatavyo: " Kwa msingi wa mahojiano na uchambuzi uliofanywa kwa kuzingatia vifungu vya 17 na 18 (yaani  maoni ya wananchi, tafiti na mabaraza ya kutoa maoni), Tume itatayarisha ripoti itakayokuwa na : (a) muhtasari wa maoni ya wananchi kwa kila hadidu ya rejea; (b) mapendekezo ya Tume kwa kila hadidu ya rejea;(c)ripoti za wataalam waeleekezi ambao Tume iliwatumia; (d) Rasimu ya Katiba. na (e) taarifa nyingine yoyote muhimu.  Hoja hapa ni kwamba, msingi wa Rasimu ya Tume ya Katiba iliyotolewa na Tume si maoni ya wananchi peke yake.  Hata pale Tume ilipobanwa kuhusu usahihi wa takwimu zilizopelekea hitimisho kuwa wananchi wengi wanataka serikali tatu, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Warioba alitoa utetezi kuwa, Sheria haikuwabana kuzingatia takwimu au maoni ya wananchi peke yake. Hivyo, hoja kwamba Rasimu ya Tume ndio maoni ya wananchi ni hoja dhaifu na muflisi. Rasimu ya Tume ni mseto wa maoni ya sampuli ya wananchi waliofikiwa, tafiti na maoni ya Tume yenyewe.

Hata tukiamua kwa imani kuwa watu wa Mungu wako sahihi kusema Rasimu ya Tume ni maoni ya wananchi, bado msingi wa imani yenyewe ni dhaifu mno. Tume tukufu ya Katiba kwa makusudi iliamua kupuuza maoni ya Mabaraza ya Katiba yaliyokuwa na uwakilishi mpana zaidi watu, kwa hoja kuwa ni maoni ya CCM, au ya kupikwa. Ni Tume hiyo hiyo iliyokuwa na ujasiri wa kupokea maoni yaliyotolewa na wanachama wa CUF kule Zanzibar yaliyotolewa katika awamu ya kwanza ambayo walikuwa wakisoma maoni kama yalivyoandikwa. Maoni hayo mengi ambayo yalitaka "Muungano wa Mkataba" Tume iliyachukua, tena ikaamua kuyatakasa ili yamaanishe Muungano wa Shirikisho wa Serikali Tatu. Wingi wa maoni hayo kiidadi na kitakwimu ndio yaliyofanya rasimu ya kwanza na baadaye ya pili ionekane kuwa wananchi wengi wanataka Serikali tatu. CUF walikuwa wa kwanza kukataa na kudai wao walipendekeza Muungano wa  Mkataba.

Iweje, katika awamu ya pili ambapo uwakilishi umepanuka kwa nchi nzima kuchagua mabaraza ya Katiba ambayo maoni yao yamepuuzwa kabisa na Tume.  Je, maoni ya Mabaraza ambayo Tume imeamua kwa makusudi kuyapuuza siyo sehemu ya maoni ya wannachi?  Iweje, viongozi wa CCT wabariki zao la matokeo ya kile kilichofanywa na CUF Zanzibar kisha waungane na Tume kuharamisha kile wanachodai kilifanyika kwenye mabaraza ya Katiba katika mchakato wa kutengeneza rasimu ya pili.  Kama maoni ya muundo wa serikali mbili si ya wengi, na mabaraza yalipika maoni, si jukumu hilo lingeachiwa Bunge la Katiba katika ule utaratibu wa kila hatua ya mchakato kuchuja maoni ya hatua iliyoitangulia? Je, hili ndio jambo ambalo watu wa Mungu wanalisimamia?

Tamko la CCT pia limeshusha lawama kubwa kwa Rais Kikwete eti ameuvuruga mchakato wa Katiba. Wamemlaumu kwa hotuba yake kwa Bunge kuwa imeingilia madaraka ya Bunge la Kikatiba. Rais analaumiwa kwa kuipinga Rasimu inayotokana na Tume aliyoiunda. Ukaingizwa ushabiki kuwa Rasimu ile ya Tume haina doa na ni timilifu. Napata tabu sana pale mtu anapotia shaka juu ya dhamira ya Rais Kikwete kutaka Katiba mpya ipatikane, tena Katiba itokanayo na wananchi. Uamuzi huu wa kuanzisha mchakato karibu umgharimu katika chama chake, ambapo amefanya ushawishi mkubwa kuwafanya walipokee jambo hili jema. Isitoshe, kila panapojitokeza mkwamo, amekuwa akijitokeza kutoa uongozi ikiwemo kukutana na wapinzani katika hatua za mwanzo za utungwaji wa Sheria. Lugha yake daima na hata sasa imekuwa ni kuwataka pande zote kuzungumza na kuridhiana. Hiyo ndio lugha iliyosheheni katika hotuba yake aliyoitoa Bungeni tarehe 21 Machi, 2014 akilizindua Bunge. Katika hotuba ile, hakuna mahali Rais alitoa maelekezo zaidi ya kuonyesha mapungufu machache katika Rasimu, kukumbusha wajibu wa Wajumbe wa Bunge la Katiba wa kujiridhisha na vifungu, sentensi na dhana. Kwa mfano, kuhusu Muundo wa Serikali Tatu, Rais anasema:  “...mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu.  Na kama zipo mabadiliko hayo yaweje?  Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi wa hoja zenye mashiko”.  Hii inaonyesha wazi kwamba Mhe. Rais hakuelekeza Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Muundo wa Serikali Mbili.

Wakati tamko hili linatolewa, kumekuwepo na rai kutoka kila upande ya kujaribu kukwamua mchakato kwa kusihi pande zote kurejea Bungeni na kuwepo kwa maridhiano. Wadau wa siasa tayari wanakutana kutafuta namna nzuri ya kwenda mbele. Matarajio ya wengi wetu ni kuwa huu ndio wakati wa viongozi wa dini kuwaombea wadau hawa na kuhubiri upendo, kusameheana na unyenyekevu. Badala yake, tamko la CCT linaturudisha kwenye uhasama, badala ya kujadili kipi ni sahihi, tamko linajadili nani yuko sahihi. Tamko la CCT halituunganishi, linatugawa. Maana tamko linazungumzia Serikali moja na kusisitiza kuwa msimamo wake ndio sahihi, bila kukumbuka kuwa CCT ni mmoja tu ya wadau walio wengi, tena hata miongoni mwa wakristo wenyewe.  Kwa vyovyote vile maoni yao hayawezi kuwa ya mwisho. Wakati tamko la CCT linalaumu juu ya kuibuka misimamo mikali ya kidini, tamko lenyewe linabeba msimamo mkali. Tamko limejaa kiburi, hukumu na lawama. Hii sio lugha tuliyoizoea kutoka kwa watu wa Mungu. Au ndio tufuate wanachosema sio wanavyoenenda?

Tamko la CCT kinyume na matarajio ya wengi halijahubiri upendo na maridhiano bali kuchonganisha Tume, Rais na Bunge. Nimeshangazwa na tamko la Viongozi wa dini kusengenya kwa kushindwa kukitaja Chama inachodai kimevuruga mchakato wa Katiba. Ni nadra sana kusikia viongozi wa dini wakizungumzia Chama kimoja kisha wasikitaje. Hii si hulka ya uzazi wala ulezi. Haitegemewi kuwa ndio hulka ya viongozi wa dini na kwa kweli wanapoamua kulaumu upande mmoja tu ilihali kila mtu aliona kwenye televisheni ambavyo kila chama kilishiriki kwenye kukwamisha mjadala Bungeni, unapata hisia kuwa CCT katika hili imeegemea upande. Napata wasiwasi ikiwa kweli hili ni tamko la CCT, naendelea kuhofu kuwa limechakachuliwa. Ikiwa ni tamko rasmi la CCT, basi napenda kuamini kwa kuchelea kuchuma dhambi ya kuhukumu kuwa, CCT haikuwa na lengo la kupotosha umma, bali aidha wameghafirika au wamepotoshwa. Sio lazima wajitokeze hadharani kuomba radhi watanzania, bali waseme na mioyo yao na kumpigia goti mwenyezi mungu awasamehe. Kweli itawaweka huru.



1 comment:

Anonymous said...

umesema unatia shaka kwa kuwa hata tamko lenyewe halisemi limetolewa na nani. mbona hata wewe hizi hadithi zako ndeefu hujasema wewe ni nani?.
tuna mashaka hata hii hadithi yako itakuwa imechakachuliwa pia. huna lolote !!