Monday, July 21, 2014

HARRIET SHANGARAI: MGOMBEA WA NAFASI YA MAKAMU WA RAIS WA JUMUIYA YA WATANZANIA DMV ANAOMBA KURA YAKO

HARRIET SHANGARAI
Ndugu WanaDMV, kwa heshima na taadhima nachukua nafasi hii kujitambulisha kwenu rasmi kama Mgombea wa Nafasi ya Makamu wa Raisi wa Jumuiya ya Watanzania DMV.

Nikiwa na mapenzi ya dhati kwa jamii,nimekuwa mtetezi wa haki za watoto yatima toka utotoni mwangu. Binafsi, nilijitoa kwa kidogo nilichokuwanacho na pia, nimekuwa muhamasishaji wa misaada ya elimu,chakula mavazi na malazi kwa watoto yatima. Kwa ufupi  nimeona mafanikio ya kina, japo bado wahitaji ni wengi.

Vile vile, nilikuwa mstari wa mbele katika uanzishwaji wa Kikundi cha Wanawake cha Kupambana na Ukimwi “KIWAKUKI”.Chombo hiki kimedumu takribani miaka 25 na  kinaendelea kusaidia wengi nchini Tanzania kikishirikina na mashirika mbali mbali duniani.

Nikiwa Mwanadiaspora nimepitia changamoto nyingi za afya na huduma zake. Jambo ambalo lilinishawishi kuingia taaluma ya afya ili niweze kuwa msaada kwa jamii. Jitihada hizi zimenipelekea kuanzisha blog yenye kutoa elimu afya kwa jamii kwa lugha ya kiswahili “NesiWanguBlogspot.com”. Nia ni kuleta mwamko katika uwanja wa afya na huduma zake.

Zaidi, nimejihusisha na zoezi  la utafutaji wa Maangalizi ya Afya kwa wanaDMV.  Zoezi hilo lilikuwa  jaribio la ufumbuzi wa matatizo ya fya kwa Wanadiaspora. Nashukuru kwa mchango wa kila mmoja wenu na ninaomba Wanadiaspora wa vitengo vya afya kuwa mstari wa mbele katika kujali afya za jamii yetu.
        SERA ZA MGOMBEA;



Jumuiya na Watoto;

  • Jumuiya iwe ni chombo cha kuunganisha watoto wa Kitanzania kwa kuweka taratibu za shuguli endelevu zitakazowakutanisha watoto wetu kupitia michezo  na vipaji vyao mbali mbali, ili kuwapatia uwanja wa kujitambua na  kung’ara katika jamii yao
  • Kuhamasisha  watoto wetu kushiriki katika vikundi mbali mbali vinavyotoa  mafunzo ya lugha, tamaduni na historia ya nchi kama  “Dasara la Lugha ya Kiswahili”, “Tanzania Youth Diaspora & Friends” na vikundi vingine mbali mbali.
  • Kushirikisha  Wazazi na Wakufunzi wa vijana  ili kutoa mafunzo na mwongozo kwa watoto wa kiume na wakike pale wanapoingia katika umri wa ujana (Adolescence). Lengo  ni kuwaelimisha na kuwatahadharisha vijana wetu kuhusu changamoto mbali mbali za ujana na matokeo ya maamuzi yasiyo sahihi .

Jumuiya na Vijana;

  • Kutoa mwongozo na msaada kwa vijana wetu, ili waweze kusimama Kielimu na Kiuchumi, na kuishi katika Maadili yanayokubalika na sheria za nchi.

  • Kufuatilia upatikanaji wa nafasi za udhamini (scholarship) kwa vijana, ajira, misaada na mikopo inayotolewa kwa wajasiriamali wadogo wadogo hapa nchini.

  • Kuwakilisha  na kuhamasisha wanaDMV kushiriki mikutano inayohusu sauti za  wahamiaji watokao bara la Afrika  kama vile  “African Affairs Advisory Group” (AAAG),Montgomery county, “Office on African Affairs”( OAA), DC nk. Hii itawezesha sauti zetu kuwakilishwa kwa County Executive na DC Mayor ambao wana malengo ya kuimarisha jumuiya za Waafrika katika maswala ya uchumi,elimu ,afya na utamaduni. (Tutambue kuwa,  mchango wetu wa uchumi ni mkubwa na unatambulika na serikali ya nchi)

  • Kuhamasisha vijana kushiriki katika mikutano na fursa za elimu zinazosimamiwa na utawala wa Rais OBAMA kwa  maendeleo ya Afrika kupitia “Young African Leaders Initiative” (YALI).

  • Kutafuta ufumbuzi na msaada kwa wanaDMV walio katika mazingira magumu; kama vile, wajane na dada zetu wanaojikuta katika mahusiano gandamizi hapa nchini.

Jumuiya na Wazee;

  • Kuwa na siku maalum ya kuwaenzi  wazee wetu DMV na kuwapa uwanja wa kutoa hoja zao ili kuzitafutia ufumbuzi
  • Kutambua mchango wa  wazee waliotutangulia na kuwa wa msaada pale wanapotuhitaji
  • Kuwashirikisha katika shughuli zote na  kutambua nafasi yao kama walezi wa jamii

Jumuiya na Afya;

  • Kushirikiana na wanaDMV wa kitengo cha afya ili tuweze kutoa msaada endelevu  kwa wanaDMV.
  • Kutoa taarifa na mafunzo endelevu ya elimu afya kwa jamii
  • Kufahamisha WanaDMV kuhusu huduma msingi za jamii zipatikanazo hapa nchini.
  • Kuhamasisha wanaDMV kupata bima mbali mbali zitakazo wawezesha kukabiliana na mabadiliko mbali mbali ya maisha kama magojwa,majanga, uzee na kifo
  • Mwisho, kukumbushia wanaDMV umuhimu wa kuandika wosia (Advance directives), ili kuondoa msuguano endapo kifo kitatokea.

Jumuiya na Sheria;
  • Kupata Mwanasheria atakayehudumia wanaDMV kwa bei nafuu na kutoa ufafanuzi wa sheria katika maswala ya uhamiaji, ajira, mahusiano na ndoa.

Jumuiya na Tabaka;
  • Jumuiya iwe ni chombo kisichofungamana na upande wowote kwa kuwaunganisha wanaDMV na kuwashirikisha bila  upendeleo katika fursa mbali mbali zinazojitokeza katika jamii yetu.

Wapendwa wanaDMV, nipo tayari kutoa ushirikiano wangu kwa Viongozi  woote watakaochaguliwa na kushirikiana na makundi yote bila kujali  jinsia, dini,itikadi za vyama au kabila

          Tukiweza Kufanikiwa Ugenini , Tutafanikisha na Nyumbani pia.

                                                                                  
                                     Naombeni Kura!
Asanteni sana

1 comment:

Anonymous said...

nakutakia kheri upate uchaguzi huo ili utimize ndoto zako.