Na Francis Godwin Blog.
DIWANI wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kata ya Lupingu wilaya ya Ludewa mkoani Njombe John Kiowi amempongeza mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kwa jitihada zake anazozifanya katika kuwapelekea maendeleo wananchi wa Ludewa huku akiwashangaa wapinzani wanaopinga jitihada mbali mbali zinazofanywa na serikali ya chama cha Mapinduzi (CCM) na kudai kuwa yeye si mpinzani wa uchwara wa kupinga maendeleo .
Akizungumza na wanahabari jana wakati wa zoezi la mbunge Filikunjombe na diwani huyo kushiriki na wananchi wa kata ya Lupingu kuchimba mashimo ya nguzo za umeme na kusimika nguzo hizo za umeme , Kiowi alisema kuwa ni zaidi ya wabunge watano wamepata kuliongoza jimbo hilo la Ludewa ila ni mara yake ya kwanza kuona mbunge akishiriki bega kwa bega na wananchi wake kuchimba mashimo kama ambavyo mbunge huyo anafanya .
" Jamani wananchi kwanza ni jambo la kumpongeza mbunge wetu mbali ya kuhimiza wananchi ila mwenyewe pia amekuwa mstali wa mbele katika kushiriki tofauti na wana siasa wengine ambao muda wote wao ni watu wa majukwaani ila vitendo sifuri .....nasema Ludewa imempata mbunge na niweke wazi hapa mimi sio mpinzani hivi tujiulize wenyewe nikisema mimi ni mpinzani napinga nini hapa haya maendeleo ni kwa faida yangu na wananchi wote sasa kama mbunge wa CCM wanafanya kuna haja ya upinzani hapa "
Kiowi alisema kuwa ataendelea kufanya kazi na mbunge Filikunjombe ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM katika kata yake kwani chama chake cha TLP katika kata ya Lupingu kinatekeleza ilani ya CCM ambacho ndicho chama kilichopo madarakani na peke yake bila kumtegemea mbunge hawezi kufanya lolote.
Diwani Kiowi ambae alikuwa amevalia sare za CCM katika shughuli hiyo ya maendeleo alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa yeye si mpinzani ila ni mpenda maendeleo hata sare za CCM zinazotolewa na mbunge Filikunjombe amekuwa akizivaa na amekuwa mstali wa mbele kumpongeza mbunge huyo kutokana na kuwa mbunge wa mfano kwa kufanya kazi bila na makundi yote .
Hata hivyo diwani huyo alisema kuwa katika suala la maendeleo hata kuwa tayari kuona watu wachache wakimkwamisha mbunge huyo kwa kushindwa kuunga mkono jitihada zake katika kuwaletea maendeleo na kudai kuwa kwa upande wake anaona wapinzani ni wana CCM wenyewe wasiopenda kujivunia maendeleo makubwa mbayo mbunge Filikunjombe ameyapeleka Ludewa .
Kwa upande wake mbunge Filikunjombe mbali ya kumpongeza diwani huyo wa TLP kwa kushiriki vema katika shughuli za maendeleo bado alisema kuwa ni wapinzani wachache nchini ambao wanajitoa kama diwani huyo katika shughuli za maendeleo zinazoitishwa na mbunge wa CCM
Alisema yapo baadhi ya maeneo wabunge ama madiwani wa upinzani wamekuwa ni watu wa kupinga kila jambo linalofanywa na mbunge ama diwani wa CCM na wengine wasiokuwa na uzalendo na Taifa wamefikia hatua ya kubeza hata jitihada zinazofanywa na Rais Dr Jakaya Kikwete katika kuliletea maendeleo Taifa jambo ambalo si la kizalendo hata kidogo na kuwa huo si upinzani wa kweli.
" Nataka kusema hivi wakati wa kampeni ndio wakati wa kupingana kisera ila baada ya chaguzi hakuna haja ya kuendelea kupingana ni kuwa wamoja na kuwaletea wananchi maendeleo hivi hebu niulize ujenzi huu wa barabara ya Lupingu ,Ludewa na Njombe Ludewa unaoendelea ni kwa faida ya nani hii barabara inatumiwa na wana CCM pekee mbona hata wapinzani mnapita katika barabara hiyo hiyo sasa unapinga nini wakati huu wa CCM kutekeleza ilani yake ....tuwe na uzalendo wa nchi yetu tusiwe wa kupinga kila kitu na mimi nikueleze wazi kama ungejaribu kupinga mradi huu wa umeme kwa kutoshiriki tungeonana wabaya mbele ya safari"
Akielezea mradi huo wa umeme Filikunjombe alisema kuwa kwa kasi ambayo wananchi wanaenda nayo katika kujitolea nguvu zao kuchimba mashimo na kusogeza nguzo katika mashimo hayo ni wazi mradi huo wa umeme utakamilika kabla ya Desemba mwaka huu .
Aidha alisema kuwa wakati akiingia madarakani mwaka 2010 ni kijiji kimoja pekee cha jimbo hilo la Ludewa ambacho kilikuwa na umeme wa mafuta ila sasa zaidi ya vijiji 10 vina umeme na kuwa hadi sasa jumla ya vijiji 49 vitafikiwa na mradi wa umeme huo ambao unatekelezwa kwa nguvu za serikali ya Tanzania , Swedeni na kanisa na Romani Katoliki Dayosisi ya Njombe.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kushoto akishiriki kubeba nguzo za umeme wakati wa uhimizaji wa wananchi wa kata ya Lupingu kushiriki maendeleo ya kupeleka umeme kata ya Lupingu |
Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe akishiriki kubeba nguzo |
Vijana wakishirikiana na mbunge wao kubeba nguzo za umeme |
jitihada za kupeleka umeme Lupingu zikionekana |
Mbunge Filikunjombe shimoni na diwani wa TLP wakishiriki kuchimba mashimo ya nguzo za umeme |
Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe akishiriki kuchimba mashimo ya nguzo za umeme pamoja na wananchi wa kata ya Lupingu |
No comments:
Post a Comment