Tuesday, July 1, 2014

Balozi Seif Ali Iddi atembeela Kijiji cha Mvuleni Shehia ya Kidoti Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejitolea na kujizatiti katika kuwaondoshea usumbufu wa upatrikanaji wa huduma muhimu wananchi wake katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Alisema kipaumbele kimewekwa zaidi katika kuhakikisha huduma za  maji safi na salama pamoja na umeme zinapatikana ili kuwapatia fursa nzuri wananchi hao kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mvuleni kiliopo Shehia ya Kidoti ndani ya Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kuwapa matumaini kwamba Transfoma inayofungwa  hivi sasa katika kijiji hicho iliyotolewa na Serikali kuu ni hatua za awali za kuwaondoshea usumbufu huo.
“ Huduma ya umeme katika Kijiji cha Mvuleni imeshafika. Kilichopo hivi sasa ni kutakiwa muwe na subra kwa ajili ya kusogezwa kwenye maeneo yenu ili mpate kuutumia”. Alisema Balozi Seif.
Aliwaomba Wananchi hao kuendelea kuwa wastahamilivu katika kipindi hichi ambacho Serikali imeamuwa kuwapatia huduma za maji safi na salama  wananchi hao kwa njia ya mgao kwa kutumia magari ya Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } hasa katika kipindi hichi kigumu cha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alisema Serikali Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } na Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } itaendelea kuimarisha miundo mbinu ya miradi ya maji na umeme ili huduma zote mbili zipatikane na kuwafaidisha wananchi katika muda wote kijijini hapo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatahadharisha Wananchi hao wa Mvuleni kuwa macho na baadhi ya watu wanaojinasibu kwamba huduma za miradi ya maji ndani ya eneo hilo imetekelezwa chini ya ufadhili wao.
“ Mradi wa Maji uliomo ndani ya Jimbo la Nungwi umeanza tokea awamu ya Sita ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoongozwa na Mheshimiwa Amani Karume na baadaye Rais wa sasa Dr. Sheni akauzindua Mradi Mkubwa wa Tangi la Maji ndani ya Jimbo hilo. Sasa anapokuja mtu akasema huduma hizo kaleta yeye wakati hata hajaingia madarakani na mradi huo upo tayari, mjue huyo kwa kweli anakuongopeni mchana “. Alieleza Balozi Seif.
Akitoa ufafanuzi wa miradi mbali mbali ya maji ndani ya jimbo la Nungwi   Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar  { ZAWA } Dr. Mustafa Garu alisema Jimbo hilo linatarajiwa kufaidika na mradi wa maji ulioanzishwa na Serikali kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA }.
Dr. Garu alisema  wahandisi wa Mamlaka hiyo hivi sasa wako katika hatua za kukamilisha ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhia maji liliopo katika eneo la Mwanguo ambalo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Alisema Wataalamu wa Mamlaka hiyo wamekuwa wakiendelea  kuchimba idadi  kubwa ya visima katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba  ili kujiepusha na athari ya kutumbuka kwa maji ya chumi katika vianzio vya maji.
Wakitoa Taarifa yao fupi Wananchi hao wa Kijiji cha Mvuleni wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua inayoendelea kuchukuwa ya kuwapunguzia matatizo yanayowakabili zikiwemo huduma za Maji safi na Umeme.
Hata hivyo Wananchi hao walisema visima vinavyosambaza huduma za maji katika maeneo ya fukuchani kutoka  Kiashange na Kigongoni kwa wakati huu havikidhi kabisa mahitaji  ya wanajamii wa eneo hilo kikiwemo kijiji chao.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pemba Juma Khamis aliiomba Serikali kupitia Mamlaka inayohusika na huduma za maji safi na salama kufanya utafiti  ili kujua tatizo linalosababisha usumbufu wa maji katika Jimbo la Nungwi.
Mh. Pembe aliafiki na kuunga mkono hoja ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kaskazini Unguja Nd. Haji Juma Haji ya kutaka kufanywa uchunguzi huo kutokana na  uwepo wa zaidi ya Visima 13 ndani ya Jimbo la Nungwi wakati uwezo wa upatikanaji huduma hiyo umekuwa na mashaka.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/7/2014.

No comments: