Thursday, May 8, 2014

Uporaji wa sekta za mbao na uvuvi unaizuia Afrika isiendelee - Kofi Annan

ABUJA, Nigeria, May 8, 2014/ -- Rasilimali za Afrika zenye utajiri mwingi zinatoa nafasi ya kipekee ya ufanisi katika uimarishaji wa maisha ya raia wa Afrika, yasema ripoti mpya kubwa iliyozinduliwa leo na Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, lakini mara nyingi sana rasilimali hizi huporwa na maafisa wafisadi pamoja na wawekezaji wa kigeni. Aidha, Ripoti hii inaonyesha kwamba kuongezeka kwa ukosefu wa usawa vilevile kunaizuia Afrika isiikamate nafasi hii ya maendeleo.

Ripoti hii ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya Afrika (http://www.africaprogresspanel.org), Nafaka, Samaki, Pesa: Kugharamia mageuzi ya Kijani kibichi na Samawati, inawahimiza viongozi wa kisiasa wa Afrika kuchukua hatua hususa sasa ili kupunguza ukosefu wa usawa kwa kuwekeza katika kilimo. Pia, inataka hatua ya kimataifa kuchukuliwa ili kukomesha kile kinachotajwa kuwa uporaji wa sekta za mbao na uvuvi.

“Baada ya zaidi ya mwongo mmoja wa ukuzi, kuna mengi ya kushangilia,” Bwana Annan atawaambia viongozi wa kisiasa na wa kibiashara, wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti hii katika mkutano wa Baraza la Kiuchumi la Ulimwengu kwa Afrika (World Economic Forum for Africa). “Lakini ni wakati wa kuuliza kwa nini ukuzi mkubwa wa jinsi hii haujasaidia hata kidogo kuwainua watu kutoka katika umasikini na kwa nini utajiri mwingi wa Afrika umeharibiwa kupitia mazoea ya ufisadi na uwekezaji usio mnyoofu.”

“Afrika ni bara lenye utajiri mwingi, kwa hivyo ni kwa nini fungu la Afrika katika utapiamlo ulimwenguni, na idadi ya vifo vya watoto inaongezeka haraka jinsi hii? Jibu ni kwamba ukosefu wa usawa unadhoofisha uhusiano kati ya ukuzi wa kiuchumi na maendeleo katika hali ya maisha ya watu,” alisema Bw. Annan.

Hata ingawa wastani wa mapato umeongezeka kwa theluthi moja katika mwongo uliopita, kuna Waafrika wengi zaidi sasa wanaoishi katika umasikini-takriban milioni 45- zaidi ya waliokuwepo katika mwisho wa miaka ya 1990. Malengo mapya ya kimaendeleo huenda yakajaribu kuodoa umasikini Afrika kufikia mwaka wa 2030 - lakini kwa mkondo wa sasa, Mwafrika mmoja kati ya Watano bado atakuwa akiishi katika umasikini mwaka huo utakapofika.

Bw. Annan, ambaye aliathiri kwa kiwango kikubwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, asema: “ Mbali na kuahidi kutimiza malengo makuu, nchi zinapojiunga na mfumo huu mpya wa kimaendeleo ulimwenguni zinapaswa kuahidi pia kupunguza mapengo yasiyoweza kutetewa katika bara hili, kati ya matajiri na masikini, maeneo ya vijijini na mijini, wanaume na wanawake.”

Waandishi wa ripoti hii wanatambulisha kilimo kuwa msingi wa ukuzi ambao utapunguza umasikini. Wanadhihirisha kwamba masikini wengi wa Afrika wanaishi na kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na kwa wingi ni wakulima wadogo wadogo.

“Nchi ambazo zimejengwa juu ya misingi ya sekta bora za kilimo - kama vile Ethiopia na Rwanda- zimeonyesha kwamba maeneo ya vijijini yanaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ukuzi wa pamoja na upunguzaji wa umasikini,” Bw. Annan atasema katika uzinduzi.

Ripoti hii inahimiza kuwe na “mageuzi ya kijani kibichi ya Kiafrika,” ambayo yanadondoa masomo kutoka kwa mageuzi ya bara la Asia na kubadilishwa ili kufaa hali za Afrika.

Kwa wakati huu, gharama ya uingizaji wa chakula kutoka nchi za nje ni dola za kimarekani bilioni 35, kwa sababu kilimo cha ndani kimekumbwa na uzalishaji wa kiwango cha chini, ukosefu wa uwekezaji, na ujitengaji wa kimaeneo. Kuongezeka kwa uwekezaji katika miundombinu na utafiti kunaweza kuinua kwa kiwango kikubwa mavuno ya eneo hili na mapato ya wakulima. Kwa wakati huo huo, kuondoa vikwazo vya kibiashara ndani ya Afrika kunaweza kufungua soko mpya.

Hata ingawa ripoti hii inakosoa viongozi wa Afrika, Ripoti ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya Afrika inaipa changamoto jamii ya kimataifa kuunga mkono jitihada za kimaendeleo za Afrika. Inadhihirisha kwamba sekta za kilimo na mbao ndizo sekta mbili muhimu zinazohitaji kuimarishwa ili kupambana na uporaji wa rasilimali za asili.

Uvuvi haramu, usiodhibitiwa na usioripotiwa umefikia kiwango cha juu kupindukia katika maji ya pwani ya Afrika. Afrika Magharibi hupoteza takriban dola za kimarekani bilioni 1.3 kila mwaka. Zaidi ya gharama za kifedha, uporaji huu huangamiza jamii za kivuvi ambazo hupoteza nafasi muhimu za uvuvi, utayarishaji na uuzaji wa samaki. Dola zingine bilioni 17 hupotezwa kupitia ukataji haramu wa miti.

“Uporaji wa rasilimali ni wizi uliopangwa na unaofichwa kwa hila katika biashara. Meli za biashara za uvuvi za kigeni, ambazo husajiliwa katika nchi za Kiafrika kwa hila, na kupakua samaki katika bandari ambazo hazirekodi mapato yao, hazina maadili,” alisema Bw. Annan, akiongeza kwamba shughuli hizi haramu hukuza tatizo la ukwepaji wa kodi na kampuni bandia. Ripoti ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya Afrika inahimiza kuwepo kwa usimamizi wenye wahusika wengi wa sekta ya uvuvi ambao utatekeleza vikwazo juu ya meli ambazo hazisajili na kuripoti mapato yao. Ripoti hii aidha inazihimiza serikali ulimwenguni pote kuidhinisha Makubaliano ya Port State Measures, mkataba ambao unalenga kuwazuia waporaji kupakua mapato yao haramu katika bandari.

Viongozi wa kisiasa wa Afrika wameshindwa kusimamia rasilimali za asili kwa masilahi ya wanaozimiliki kihalisi- watu wa Afrika. Pamoja na kupoteza pesa kupitia uporaji na usimamizi mbaya wa kifedha, Waafrika wanapoteza pesa za kigeni, si ambapo wafadhili wanapokosa kuweka hadi zao tu, bali pia wakati Waafrika wanaoishi katika nchi za kigeni wanapotuma pesa kwa familia zao. Inakadiriwa kwamba kila mwaka bara hupoteza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1.85 katika ada za kupindikia zinazotozwa kwa huduma hizi.

Zikiwa na mapato makubwa ya rasilimali, serikali za Afrika sasa zina nafasi ya kutengeneza mifumo bora ya kodi – na kutumia pesa za umma vizurikwa njia ya usawa, ripoti hii inaongeza. Kwa mfano, asilimia 3 ya pato la jumla la eneo (GDP) kwa sasa huelekezwa kwa ruzuku za nishati ambazo kwa sehemu kubwa huenda kwa watu wa tabaka la kati kati. Pesa hizo zinapaswa kugeuzwa na kupelekwa kwa matumizi ya jamii ili kuwapa masikini nafasi bora ya kutoroka mtego wa umasikini.

“Uwezo wa Afrika wa kukabiliana na hali ngumu, na ubunifu ni mkubwa,” asema Bw. Annan. “Tuna idadi kubwa ya vijana wenye nguvu. Wajasiriamali wetu wanatumia teknolojia kubadilisha maisha ya watu. Tuna rasilimali za kutosha kulisha si sisi tu bali na maeneo mengine pia. Ni wakati kwa viongozi wa Afrika - na wawekezaji shirika wenye uwajibikaji - kuibua uwezekano huu mkubwa.”

Distributed by APO (African Press Organization) on behalf of the Africa Progress Panel (APP).

Ikisimamiwa na Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Jopo hili lenye watu kumi hutetea, katika viwango vya juu sana, maendeleo endelevu na yenye usawa barani Afrika. Jopo hili hutoa chapisho lake kuu, Ripoti ya Maendeleo ya Afrika, kila mwaka mwezi Mei. (http://www.africaprogresspanel.org)

No comments: