Friday, May 16, 2014

MAMA SALMA KIKWETE ATEMBELEA SHULE YA MSINGI YA MSIMBAZI MSETO KWENYE KITUO CHA WATOTO WENYE USONJI (AUTISM).

 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha kuwahudumia watu wenye usonji (Autism) hapa Tanzania Ndugu Daniel Long’lway wakati alipowasili kwenye Shule ya Msingi ya Msimbazi Mseto yenye kituo cha kuwahudumia watu wenye matatizo hayo 
  Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ndugu Raymond Mushi  (kushoto) na Diwani wa Bungoni Ndugu Fungo(kulia) na viongozi wa Shule ya Msingi ya Msimbazi Mseto kutembelea maeneo mbalimbali ya kituo cha kuwahudumia watu wenye matatizo ya usonji (autism) 
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipata maelezo ya  Shule ya Msingi ya Msimbazi Mseto iliyoko katika wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam.


 Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akimkumbatia mtoto mwenye matatizo ya usonji (autism)  wakati alipotembelea  kwenye kituo cha Msimbazi kilichoko wilayani Ilala 
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimpongeza mtoto Erick mwenye matatizo ya usonji (autism) baada ya mtoto huyo kufanikiwa  kupanga kete zake za kuchezea vizuri kwenye shule ya Msingi Msimbazi Mseto wakati Mama Salma alipotembelea
  Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipiga picha na watoto Abdallah Athuman (kulia) na Nasma Jumanne (kushoto) wenye matatizo ya usonji  (autism) wakati alipotembelea kwenye Shule ya Msingi Msimbazi Mseto
  Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akishiriki katika kuimba na kucheza na watoto wenye matatizo ya usonji (autism),wazazi na walimu wakati alipotembelea  Shule ya Msingi Msimbazi Mseto 
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akishiriki katika kuimba na kucheza na watoto wenye matatizo ya usonji (autism),wazazi na walimu wakati alipotembelea  Shule ya Msingi Msimbazi Mseto 
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na walimu na wazazi (hawapo pichani) wa watoto wenye matatizo ya usonji (autism) wanasoma katika Shule ya Msingi Msimbazi Mseto mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kituo cha kuwaelimisha watoto hao tarehe 15.5.2014.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na walimu na wafanyakazi wa Shule ya Msingi ya Msimbazi Mseto iliyoko katika wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam. PICHA NA JOHN  LUKUWI 

Na Anna Nkinda – Maelezo
Wazazi wenye watoto ambao wanatatizo la usonji (Autism) nchini wametakiwa kuwapenda, kuwatunza  na kuwapa mahitaji yao kama watoto wengine kwani ni makusudi na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kuwapa watoto hao.

Mwito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete wakati akiongea na walimu, walezi na wazazi wa watoto hao katika Shule ya Msingi Msimbazi Mseto kitengo cha usonji iliyopo wilaya ya Ilala  jijini Dar es Salaam. 

Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kuwapatia watoto hao  jambo la muhimu ni kumshukuru  na kuacha kujiuliza ni kwa nini aliwapa watoto wenye tatizo la usonji. 

“Ninawapongeza kwa kazi mnayoifanya na moyo wa huruma na upendo wa kuwatunza watoto hawa, msilalamike na kuhudhunika  bali wapendeni kama watoto wengine na kuwapatia mahitaji yao”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema yeye kama mzazi anaguswa sana na maisha ya watoto hasa wenye mahitaji maalum ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, walemavu wa ngozi na viungo. 

Kwa upande wa walimu wanaowafundisha watoto hao aliwapongeza kwa kazi wanayoifanya na kusema kuwa kazi hiyo ni wito na inahitaji moyo wa ziada hata kama watalipwa  malipo kiasi gani hayawezi kuendana na kazi wanayoifanya.

Akisoma risala ya Chama cha kuwahudumia watu wenye Usonji (National Association for People with Autism in Tanzania (NAP-T)) Daniel Longhway alisema chama hicho kinawanachama 41 na kitengo hicho katika shule ya Msingi Msimbazi Mseto kina wanafunzi 24 wanaohudumiwa na walimu tisa na kinawafuatilia watoto 50 ambao wame maliza muda wao wa kuwa shuleni na hivi sasa wako majumbani.

Alisema Usonji ni hali ya udhaifu katika ukuaji wa ubongo ambayo huleta athari kubwa katika mawasiano, mahusiano ya kijamii na utambuzi.Tatatizo hili ni la dunia nzima na bado hakuna maelekezo kamili ya chanzo chake wala tiba. Wanaoathirika zaidi ni watoto wa kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa nne kwa moja hii ikiwa na maana kuwa kila watoto watano wenye usonji wanne ni wa kiume na mmoja wa kike.

“Chama chetu kina mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na muamko wa wazazi kutowaficha watoto wenye usonji umekuwa mkubwa, vitengo vya kutoa elimu kwa watoto vimeongezeka, utengemano umekuwa mkubwa kwa watoto waliopo mashuleni pia wazazi na walezi hasa wenye watoto waliopo mashuleni wanapata ushauri nasaha”, alisema Longhway.

Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo ambako patajengwa chuo cha ufundi kwa watoto wakubwa wanaomaliza shule ambao hawana mahali pa kwenda, mabweni ya wanafunzi, madarasa, nyumba za walimu, viwanja vya michezo na ukumbi, upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Kutokuwa na usafiri wa kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani watoto pamoja na kuwapeleka walimu kuwatembelea wanafunzi majumbania ,kutokuwa na wataalamu wa speech therapy, Physiotherapy na occupational Therapy, chakula kwa wanafunzi na wanahitaji wasaidizi wawili kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi.

Mwaka 1997 wizara ya Elimu na Utamaduni ikishirikiana na wanachama wa NAPA - T walianzisha kitengo cha watoto wenye usonji katika shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa huduma. Hivi sasa Serikali inavitengo vitano, viwili vipo Dar es Salaam, viwili Arusha na kimoja Morogoro. Pia kuna vitengo kadhaa vilivyoendeshwa na watu binafsi.

No comments: