Tanzania
inatarajiwa kuondoka kwenye kundi la nchi masikini na kuhamia kwenye
kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Kauli hiyo
imetolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
alipokuwa akifungua kongamano linaloendelea huko Berlin nchini
Ujerumani kama njia mojawapo ya kuadhimisha jubilee ya miaka 50 ya
muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kongamano
hilo linakutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabalozi,
wataalamu na wafanyabiashara mbalimbali ambapo Profesa Muhongo alipata
nafasi ya kuwasilisha mada kuhusiana na fursa zilizopo katika sekta ya
gesi, mafuta ikiwa ni pamoja na madini.
Profesa
Muhongo alisema ili nchi ya Tanzania iweze kupiga hatua kimaendeleo
inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye nishati ambayo ndiyo yenye mchango
mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Akielezea
juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na maisha
bora, Profesa Muhongo alisema kuwa serikali kupitia Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) imeanza juhudi za kupeleka umeme kwenye vijiji vyote kwa
awamu tofauti tofauti.
“
Hatuwezi kusema kuwa nchi imeendelea wakati wananchi wa vijijini hawana
umeme, na katika kutambua hilo serikali imeweka nguvu nyingi
kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inapatikana vijijini na kuchochea
maendeleo.” Alisisisitiza Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa
kutosha, serikali imekwishaanza mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la gesi
linaloanzia Mtwara hadi jijini Dar es salaam.
Akizungumzia
mradi huo, Profesa Muhongo alisema kuwa gesi itakayozalishwa itatumika
majumbani, viwandani, kwenye magari ikiwa ni pamoja na kuzalisha umeme
wa kutosheleza nchi na mwingine kuuzwa kwenye nchi za jirani na
kuliingizia pato taifa.
“
Kwa mfano mara baada ya kuzalisha gesi ya kutosha na kuondokana na
changamoto ya upungufu wa umeme wa kutosha kulingana na mahitaji
makubwa ya wananchi, umeme wa ziada utauzwa kwa nchi jirani kama Kenya
na Ethiopia.” Aliongeza Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo aliendelea kusema kuwa kugundulika kwa gesi katika mikoa ya
Lindi na Mtwara na kuanza kwa mradi wa bomba la gesi kumepelekea
wawekezaji kujitokeza ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha sementi
cha Dangotte kitakachokuwa kikubwa Afrika Mashariki.
Alisema
kuwa mnamo Oktoba 25, mwaka jana serikali ilizindua vitalu saba vipya
katika maji ya kina kirefu cha bahari ya Hindi na kitalu kimoja
Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika vya utafutaji wa mafuta na gesi na
kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo ya kuomba vitalu kwa kufuata
masharti yaliyowekwa kabla ya Mei 15, mwaka huu.
Profesa
Muhongo aliongeza kuwa mbali na umeme wa maji na mafuta Wizara yake
imeweka pia mkazo katika vyanzo vingine vya umeme kama makaa ya mawe,
upepo, nishati jadidifu kama njia mojawapo ya kuongeza umeme.
“Kwa
mfano umeme wa upepo unazalishwa mkoani Singida, vyanzo hivi na
vingine vinasaidia mikoa ambayo iko nje ya gridi ya taifa kupata umeme.”
Alisisitiza Profesa Muhongo.
Profesa
Muhongo aliwataka wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania kupitia sekta
za gesi, mafuta na madini na kuwahakikishia kuwa zipo sheria zinazotoa
mwongozo juu ya usimamizi thabiti ikiwa ni pamoja na sheria ya petroli
ya mwaka 2008, sheria ya umeme ya mwaka 2008, sera ya gesi asilia ya
mwaka 2013, sheria ya gesi ambayo bado ipo katika maandalizi na mpango
kabambe wa matumizi ya gesi asili ambao bado uko katika hatua za mwisho
za maandalizi.
Profesa
aliongeza kuwa miongozo mingine ni pamoja na sera ya nishati ya mwaka
2003, sheria ya petroli (utafutaji na uzalishaji) ya mwaka 1980, sheria
ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na nyinginezo.
Akijibu
swali lililoulizwa kuhusiana na wataalamu kwenye sekta mpya ya gesi
Tanzania Profesa Muhongo alisema Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini imekuwa ikipeleka wataalamu katika mafunzo ya muda mrefu katika
shahada ya uzamili katika vyuo vikuu vilivyopo nje ya nchi kama
Uingereza na Scotland.
Aidha
Profesa Muhongo aliongeza kuwa tayari chuo kikuu cha Dar es Salaam
ikiwa ni pamoja na chuo kikuu cha Dodoma vimeanza kutoa kozi ya masuala
ya gesi na mafuta ili kuongeza watalamu katika sekta hiyo.
Profesa
Muhongo alisema kuwa serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini
imekuwa ikidhamini wanafunzi wanaosomea masuala ya gesi na mafuta katika
chuo kikuu cha Dodoma ikiwa ni pamoja na nje ya nchi.
Aliongeza
kuwa ili kuhakikisha kuwa watalamu wa kati (technicians) hawaachwi
nyuma, Chuo cha Madini kilichopo Dodoma kimeanza kutoa mafunzo hayo
katika kiwango cha diploma.
“Juhudi
zote zinafanywa na serikali kuhakikisha kuwa inazalisha wataalamu wa
kutosha kwani ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya teknolojia; bila
utaalamu katika nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea kamwe, wanasayansi
wanahitajika sana.” Alisisitiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia
kwa upande wa madini, Profesa Muhongo alisema kuwa Tanzania imejaliwa
kuwa na madini ya kila aina chini ya dunia na kuna maeneo mengi sana
ambayo madini hayajachimbwa bado na kuwataka wawekezaji kuwekeza katika
sekta hiyo.
Profesa
Muhongo aliendelea kusema kuwa serikali imeandaa ramani za kijiolojia
na kuwataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa hiyo.
Alisema
kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani umekuwa ni wa muda
mrefu na kusisitiza kuwa ushirikiano huo unatakiwa uimarishwe haswa
katika uchumi ili kupiga hatua za kimaendeleo.
Aliongeza
kuwa ili kuinua sekta ya madini serikali imekuwa ikifanya juhudi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha shirika la madini la taifa
(STAMICO) na kuwawezesha wachimbaji wadogo.
“Kwa
mfano hivi majuzi tumetoa ruzuku ya dola za kimarekani 500,000 kwa
wachimbaji wadogo ambao tunaamini wana mchango mkubwa sana katika pato
la taifa.” Alisisitiza Profesa Muhongo.
Akijibu
swali kuhusiana na mchango wa madini kwa taifa, Profesa Muhongo
alisisitiza kuwa sekta ya madini imekuwa na mchango mkubwa katika pato
la taifa kwa kujenga mashule kwenye maeneo ya migodi, mahospitali,
ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na matumizi mengine.
Profesa
Muhongo alisisitiza kuwa serikali inawakaribisha wawekezaji kwa mikono
miwili kuwekeza katika sekta hizo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano
wa kutosha ili kujenga uchumi na kudumisha uhusiano kati ya Tanzania na
Ujerumani.
Alisema
kuwa suala la rushwa halina nafasi katika uwekezaji na kuwataka
wawekezaji hao kujitokeza na kuwekeza kwa kuwa fursa ni nyingi mno.
Alitaja
sheria zinazosimamia sekta ya madini ni pamoja na sheria ya madini ya
mwaka 2010, sheria ya ulipuaji baruti ya mwaka 1963, sheria ya usimamizi
wa mazingira ya mwaka 2004, sheria ya kodi ya mwaka 2004 na nyinginezo.
No comments:
Post a Comment