Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akiwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma na kupokewa na Mkuu wa Mkoa huo Dr. Rehema Nchimbi tarehe 11.4.2014.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akikaribishwa kwa shamrashamra za kwaya na matarumbeta wakati alipotua kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma kwa ziara ya siku tatu mkoani humo.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akipanda mti eneo la jengo la utawala wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakati alipotembelea chuoni hapo kwa ajili ya kufungua rasmi kongamano la Mustakabali wa mtoto wa kike katika mazingira ya sasa kwa wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu vilivyopo Dodoma na Morogoro. Kongamano hilo lilifanyika katika ukumbi wa Chimwaga tarehe 12.4.2014.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akikaribishwa ukumbini na wanafunzi wa kike waliojawa na furaha na hamasa kubwa.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akishiriki kucheza kwa nderemo na vifijo na wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu mbalimbali vya Dodoma na Morogoro wimbo uitwao ..”wanawake na maendeleo..” mara baada kuingia ukumbini. Mama Salma alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kongamano la mustakabali wa mtoto wa kike katika mazingira ya sasa.
Kaimu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Profesa Herman Mlacha akimkabidhi Mke wa Rais Mama Salma Kikwete zawadi ya ramani ya Tanzania yenye kuonyesha pia picha ya Chuo Kikuu cha Dodoma mara baada ya ufunguzi wa kongamano hilo tarehe 12.4.2014.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwahutubia mamia ya wanafunzi wa kike kutoka vyuo vikuu waliofurika katika ukumbi wa Chimwaga huko Dodoma tarehe 12.4.2014.
Na Anna Nkinda – Maelezo , Dodoma
Wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu nchini wametakiwa kujitambua na kufahamu wajibu wao kwa jamii inayowazunguka kwa kufanya hivyo wataweza kujiepesha na vishawishi mbalimbali vikiwemo vya ngono na kujikomboa kifikra, kiutamaduni na kiuchumi na hivyo kutimiza ndoto za maisha yao.
Pia wametakiwa kujuwa thamani yao na kuepuka kutumiwa vibaya na kushinda majaribu ya watu wanaotaka kuivuruga safari yao ya maisha na kutokubali mtu kuwajaza hofu na kuyumbisha uthubutu wao.
Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu waliohudhuria kongamano la mustakabali wa mtoto wa kike katika mazingira ya sasa lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga uliopo chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kila mtu amepewa karama za kumuwezesha kufikia wito wa kutimiza ndoto zake ili kuweza kufanikisha hayo hana budi kujitambua, kuvitunza na kuvilea vipawa na karama zake na kuyakubali madhaifu yake katika kutimiza azma zake.
“Kataa kabisa mawazo ya kukatisha tamaa kwani hofu kama ilivyo furaha huuambukiza , jaribu kuwaepuka marafiki wenye mawazo ya kukatisha tamaa kwani hao ndiyo maadui wakubwa wa maisha yako na wa kukukwamisha kufikia malengo yako.
Kuna wakati inawezekana ukawa na hamu ya kuona malengo yako yanatimia mara moja ukweli ni kwamba hamu yako ya kuleta mabadiliko ya haraka yanaweza kukuletea madhara makubwa kuliko faida na hapa ndipo mabinti wengi uharibikiwa kwa sababu wanakosa subira na hivyo kufanya mambo yao kinyume na utaratibu na malengo”, aliasa Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwahimiza wanafunzi hao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika vyuo vyao kwa kufanya hivyo watajiwekea mazingira mazuri ya kuwa viongozi wa baadaye pindi watakapomaliza masomo yao kwani viongozi wengi wanaowaona leo walianza kujishughulisha na uongozi wakiwa wanafunzi.
Mama Kikwete alisema, “Wanawake tuna nafasi ya pekee ya uongozi kwani sisi ndio wazazi na walezi tunaokabiliwa na changamoto nyingi, hivyo basi sisi tuna mchango wa pekee katika kutatua changamoto hizo lakini tutaweza kufanya hivyo kama tutaingia katika ngazi ya maamuzi jambo la muhimu ni kupendana na kuungana katika mambo ya maendeleo kwa ajili ya maslahi yetu kama wanawake”.
Akisoma Risala ya wanafunzi hao mwakilishi wa wanafunzi Hamida Salum alisema katika maisha suala la kujitambua ni la muhimu kwakuwa wanafunzi wengi wa elimu ya juu wanasoma bila ya kuwa na malengo hali hii husababishwa na kutojitambua kunakowapelekea kupoteza mwelekeo kwani lengo kuu linalowapeleka vyuoni ni kupata elimu.
Hamida alisema, “Changamotozinazomkabili mtoto wa kike ni nyingi baadhi ni kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi na jinsia jambo ambalo limesababisha wasichana wengi kujihusisha katika mahusiano yasiyo salama, dhana potofu ambayo imejengeka katika jamii kwamba wanawake hawawezi kuwa viongozi kiasi cha kuwaathiri hata watoto wa kike wenye uwezo wa kuongoza.
Sera nyingi za nchi yetu zimemsahau mtoto wa kike katika mambo yanayomuhusu na hivyo kumfanya aonekane ni mtu duni kwenye jamii kwani tumekuwa tukishuhudia wazee, watu wazima wakiwarubuni wanafunzi wa kike na kuwa na mahusiano nao ya kimapenzi ambayo yamepelekea wasichana wengi kupata ujauzito na hatimaye kufukuzwa shule”.
Wanafunzi hao pia waliiomba Serikali itazame upya sera ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hasa wasichana kwakuwawengi wao hawakidhi vigezo vya kupewa mikopo na wanahitaji kusoma hivyo wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo duni kiuchumi kushindwa kuendelea na masomo.
Kwa upande wake mtoa neno la shukrani Zakiah Mbuma ambaye ni mwakilishi wa wanafunzi alimshukuru Mama Kikwete kwa kukubali mwaliko wao na kuweza kushiriki nao katika kongamano hilo ambalo limewasaidia kujifunza mambo mengi kutokana na nasaha zake pamoja na mada zilizitolewa.
“Hivi sasa tumeweza kujitambua na kufahamu thamani yetu hapo ndipo tunaweza kufikia malengo , kutambua mazingira au wakati sahihi wa kufanya jambo , kwakuwa kila msichana amepewa vipawa na karama zake jambo la muhimu ni kukubali madhaifu na kuepuka kutumiwa vibaya”, alisema Zakiah.
Kongamano hilo la siku moja liliandaliwa na Chuo kikuu cha Dodoma na kuhudhuriwa na wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo kikuu cha Mt. John, Chuo kikuu Mzumbe, Chuo cha Mipango, Chuo cha Hombolo, Chuo cha Madini na Shule ya sekondari Dodoma .
Baadhi ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wakiwemo mawaziri, wabunge na wajumbe wa bunge la katiba walihudhuria kongamano hilo ambapo mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na malengo ya kujitambua, uongozi, afya ya uzazi na ujinsia na nafasi ya mtoto wa kike katika katiba mpya.
No comments:
Post a Comment