Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bibi. Anna T. Maembe akisisita haja na umuhimu wa wazazi kuwawezesha watoto wao wa kike kuyapenda masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu ( STEM) badala ya kuliachia jukumu hilo serikali au walimu. Alikuwa akizungumza katika mkutano wa pembezoni ulioandaliwa kwa pamoja kati ya Tanzania, Uingereza na Kampuni ya Kimataifa ya GlaxoSmithkline ili kujadili fursa na changamoto za mwanafunzi wa kike katika masomo hayo, kulia kwa Katibu Mkuu ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bibi. Irina Bokova ambaye alikuwa modereta wa majadiliano hayo na pia alielezea nafasi na Mchango wa UNESCO katika kumsaidia mtoto wa kike. Kushoto ni Balozi Ramadhan Mwinyi , Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Wizara ya Wanawake na Usawa wa Uingereza, Bibi, Maria Miller ( Mb) akielezea uzoefu wa nchi yake katika kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya STEM, kulia kwake ni Bibi Nicola Yates, Makamu wa Rais wa UK and Ireland Phamarceuticals na Meneja Mkuu wa GlaxoSmithkline. Nyuma ya Waziri Miller na anayefuatilia kwa makini majadiliano hayo ni Mwanamitindo Bi. Flaviana Matata ambaye pamoja na kujikita fani ya mitindo na ambayo imemjengea heshima kubwa, lakini pia kupitia Taasisi yake ya Flaviana Matata Foundation ameonyesha mapenzi makubwa ya kuwasaidia wanafunzi kuipenda shule na kudumu shuleni.
Makatibu Wakuu kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bibi. Asha Ali Abdullah ( Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto) na Bibi. Mwanaidi Salehe Abdulla ( Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amari) wakifuatilia majadiliano hayo kuhusu fursa na uwezeshaji wa wanafunzi wa kike kujiunga na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu.
sehemu wa washiriki wa Mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake, walioshiriki majadiliano hayo ambapo pia walipata fursa ya kuchangia kwa kuuliza maswali meza kuu iliyowahusisha Katibu Mkuu, Anna Maembe, Mkurugenzi Mkuu UNESCO, Irina Bokova, Waziri Maria Miller ( Mb) na Nicola Yates Meneja Mkuu GlaxoSmithkline ambao ndio waliokuwa wazungumzaji wakuu.
Katibu Mkuu Maembe akipeana mkono na Waziri Miller ( Mb) mwishoni mwa mkutano huo wa pembezoni.
Na Mwandishi Maalum
Tatizo la wanafunzi wa kike kutochangamkia au kuyapenda masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) ni tatizo linalozikumba nchini nyingi duniani zikiwamo zilizoendelea.
Na kwa sababu hiyo imeelezwa kwamba, ushirikiano wa karibu kati ya serikali kuu, sekta binafsi, wazazi , walimu na wanafunzi wa kike unahitajika hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote na hasa wakati huu ambapo Jumuiya ya kimataifa inajipanga na kuandaa ajenda mpya za malengo ya maendeleo endelevu baada ya 2015.
Hayo yamejitokeza siku ya jumatano wakati wa mkutano wa pembezoni ulioandaliwa kwa pamoja kati ya Tanzania, Uingereza na Kampuni ya Kimataifa ya GlaxoSmithkline na kuwashirikisha wajumbe wanaohudhuria mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Watoto na Jinsai, Bibi Anna Maembe kwa upande wa Tanzania, Bibi Maria Miller ( Mb) Waziri wa Wanawake na Usawa kwa upande na Uingereza na Bibi. Nicola Yates Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Madawa ya Uingereza na Ireland na Meneja Mkuu wa GlaxoSmithkline ndio waliokuwa wazungumzaji wakuu wa mkutano huo ambao dhumuni lake lilikuwa ni kutafakari, kubadilisna uzoefu, changamoto na kutafuta mbinu zaidi za kuwasaidia wanafunzi wa kike kupenda STEM.
Mkutano huo ambao ulivutia washiriki wengi hadi wengine kukosa nafasi ya kuingia, modereta wake alikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Bibi. Irina Bokova.
Akielezea uzoefu wa Tanzania na changamoto zake katika eneo hilo , Katibu Mkuu Anna Maembe, amesema, pamoja na kwamba serikali kuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo sekta binafsi kuweka mifumo mbalimbali inayolenga kuwasaidia na kuwahamasisha watoto wa kike kuchangamkia masomo hayo bado safari ni ndefu.
Akasema changamoto kubwa ni katika eneo la ufuatiliaji ili kubaini kama wanafunzi waliosaidiwa na kujengewa uwezo wamefikia wapi katika masomo yao na baada ya kuhitimu je wanafanya kile walichosomea.
Akaongeza kuwa itakuwa ni kazi bure kama serikali peke yake itaachiwa jukumu hilo pasipo wazizi wenyewe kuhamasika na kuwajengea mazingira mazuri watoto wao wakike tangu wakiwa na umri mdogo wa kuyapenda masomo hayo.
“Sisi katika Tanzania tunaishukuru sana serikali kwa mchango wake wa kuwasaidia wanafunzi wa kike kujiunga na masomo ya sayansi, hesabu, uhandisi na teknolojia, lakini serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu, nafasi ya wazazi ni muhimu sana sana” akasisitiza.
Akaongeza pia kuwa Tanzania inao wanawake ambao ni wahandisi, wataalamu waliobobea katika ufundishaji wa hesabu, sayansi na hata utafiti na wengine wanaongoza Idara za Serikali au kampuni binafasi.
Akasema hao wote wanaowajibu wa kujitokeza ili kutumia uzoefu wao kuwahamasisha wanafunzi wa kike kufikia pale walipofika wao.
Naye Waziri wa Uingereza yeye alisema, hata katika nchi yake, bado wanafunzi wengi wa kike hawapendi masomo hayo, na hata kama wakiyasoma, si wote waoishia kufanya kazi walizosomea.
Akasisitiza haja na umuhimu wa sekta binafsi kusaidiana na serikali katika eneo hilo na pia umuhimu wa watoto wa kike kuhamasishwa na kujengewa uwezo wakiwa wangali wadogo ili kutambua vipaji vyao.
Naye Makamu Rais na Meneja Mkuu wa GlaxoSmithKline yeye aliainisha program mbalimbali ambazo kama sekta binafsi imekuwa ikichangi katika eneo hilo.
Akasema uzoefu uonyesha kuwa watoto wa kike wakiwezeshwa na kuhamasishwa wakiwa wangali wadogo wanayofursa kubwa ya kupenda hesabu, sayansi, uhandisi na masuala ya teknolojia. Na pia inakuwa hamasa kwao wakiwaona wanawake waliofanikiwa katika maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment