Na Francis Godwin, Iringa
WASHIRIKI wa warsha ya siku moja ya mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya Hifadhi ya jamii (SSRA) mkoani Iringa wamepongeza jitihada mbali mbali zinazoendelea kufanywa na SSRA katika kuwakutanisha wadau wa mifuko hiyo kwa kuwapa elimu zaidi.
Pongezi hizo zimetolewa leo katika ukumbi wa VETA mjini Iringa na washiriki wa warsha hiyo ambapo wameshauri mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kuiga mfano huo wa SSRA katika kuwapatia elimu wanachama wake ili kutojutia kujiunga na mifuko hiyo.
Katibu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya Kilimo Bw Deus Magesa alisema kuwa jitihada kubwa zimekuwa zikifanywa na SSRA kwa kuwatembelea wadau wake na kuwapatia elimu mbali mbali juu ya mifuko hiyo pamoja na kupokea changamoto mbali mbali ila kwa mifuko husika ambayo wanachama wamekuwa wakikatwa fedha zao imekuwa haina utaratibu wa kutoa semina kwa wanachama wake.
Hivyo alisema kuwa kama msimamizi mkuu wa mifuko hiyo SSRA amekuwa akifika kutoa elimu iweje mifuko hiyo ya kijamii kama NSSF imekuwa ikishindwa kufika kutoa elimu kwa wanachama wake na kuwa wanachama wengi bado wanajua sheria za zamani ila sheria mpya ya mfuko huo hawaijui ila wahusika wa mfuko huo wa NSSF wamekuwa wakikaa kimya .
“Mfuko wa NSSF kweli unachangamoto nyingi kwa wanachama wake kwanza hawana kadi za uanachama na waajiri wengi wanatumia sheria za zamani kwa mfanyakazi anapoingia kuwa mwanachama wa NSSF ila mfumo huo bado unamkwaza mwanachama …hivyo nawaomba NSSF kuiga mfano wa SSRA katika kutoa elimu na kuwabana baadhi ya maofisa wa NSSF ambao wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wanachama wake”
Kwa upande wake meneja wa NSSF mkoa wa Iringa Marko Magheke mbali ya kupongeza jitihada za SSRA kwa kuwafikia wanachama wake bado alisema kuwa si kweli kama NSSF imekuwa ikiwanyanyasa wanachama wake na kuwa kikwazo kikubwa cha kutoa elimu kinasababishwa na waajiri ambao wamekuwa hawataki wafanyakazi wao kupewa elimu na zaidi maeneo ambayo elimu imetolewa basi ni kupitia vyama vya wafanyakazi wenyewe.
Kwani alisema ni vigumu kuwakusanya wafanyakazi katika kampuni husika bila ya mwajiri kukubali kufanya hivyo na kuwa waajiri wengi hawapendi kuona wafanyakazi wao wanajua haki zao juu ya mifuko hiyo ya kijamii.
“ Sisi NSSF kazi yetu moja wapo ni kutoa elimu kwa wanachama ila tatizo ni waajiri wenyewe ambao wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano kwa kuwatoa wafanyakazi wake katika uzalishaji kwa nia ya kupewa semina”
Pia alisema kuhusu lugha chafu kwa wateja yeye hajapata kufikishiwa malalamiko na kuwa kila mfanyakazi wa NSSF ananembo inayoonyesha jina lake hivyo kwa yule mteja atajibiwa vibaya ni vema kusoma jina na kupeleka malalamiko yake kwa meneja.
Hata hivyo aliwataka waajiri wote kuhakikisha wanafikisha michango ya wanachama wao kwa wakati na kuwa mwajiri kutofikisha michango hiyo ni kinyume na taratibu na NSSF inaweza kuchukua hatua kali dhidi yake.
Alisema kumekuwepo na changamoto kubwa ya waajiri kutofikisha michango ya wanachama na kuwa eneo moja wapo linalosumbua kwa waajiri wake kutofikisha michango ya wanachama wake ni pamoja na vyombo vya habari ambapo katika mkoa wa Iringa wadaiwa sugu ambao wamepata kufikishwa mahakamani ni pamoja na kituo kimoja cha radio mjini hapa na sekta nyingine mbili.
Sarah Kibonde Msika ni mkuu wa mawasiliano uhamasishaji wa mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya Hifadhi ya jamii (SSRA)nchini alisema kuwa lengo la kufika mkoani Iringa ni kuhamasisha wafanyakazi kuijua mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii.
Kwani lisema kuwa wakati takwimu zinaonyesha kuwa watanzania kama milioni 45 na nguvu kazi kama milioni 22 ila wanachama waliojiunga na mifuko hilo ni milioni 1.7 pekee hivyo lengo la SSRA ni kuona wanachama wanaongezeka zaidi.
Aliitaja mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii kwa Tanzania bara kuwa ni mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF),Mfuko wa pensheni wa PPF,mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSPF),,mfuko wa pensheni kwa wafanyakazi wa serikali (GEPF),mfuko wa Pensheni wa LAPF na mfuko wa Taifa wa bima ya Afya (NHIF) na kuwa kila mtanzania anapaswa kujiunga na moja kati ya mifuko hiyo .Alisema kuwa mifuko hiyo sita inasimamiwa na SSRA na kuwa lengo ni kuona wanachama wake wanaendelea kujiunga kwa wingi na kunufaika na mifuko hiyo.
Msika alisema kuwa Hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu na hii imeainishwa katika ibara ya 11(1)) ya katiba ya jamuhuri ya Muungano WA Tanzania na sera ya Taifa ya Hifadhi ya jamii ya mwaka 2003 na kuwa haki hiyo pia imeainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi Duniani (ILO).
|
No comments:
Post a Comment