Wednesday, March 12, 2014

SERIKALI YAJIPANGA KUWA NA SERA YA FILAMU

Mtendaji Mkuu Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo akiwasilisha Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu wakati wa moja ya kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni, kulia ni Mkurugenzi msaidizi kutoka Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Verediana Mushi, na Kushoto ni mdau wa filamu Bw. John Kitime.
Wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu wakijadiliana wakati wa kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni. (Picha na Genofeva Matemu).

Na: Genofeva Matemu – Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WHVUM

Serikali ya Tanzania imejipanga kuendeleza kwa dhati TASNIA ya Filamu ili kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa wasanii na pia kuongeza uchumi wa nchi.

Ni dhahiri kuwa sekta ya filamu ni njia madhubuti ya kutambulisha jamii kiutamaduni, kisiasa na kijamii  na pia katika kukuza na kuongeza fursa za nchi katika uwekezaji na utalii. 

Filamu na Makala za Filamu zikitumika vizuri zitaweza kuhamisha na kuondoa tofauti  mbalimbali zilizopo ndani ya jamii na hivyo kuongeza umoja na mshikamano baina ya watu wa makabila na watu wenye asili mbalimbali, hivyo kuutambulisha utamaduni wa Mtanzania.
Kazi na shughuli za Filamu nchini zimekuwa zikisimamiwa na Sera ya Utamaduni ambayo ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1997 pamoja na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza na 4 ya mwaka 1976. 

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2013 kumekuwepo na maendeleo  makubwa katika Tasnia ya Filamu nchini hivyo kuisababishia Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kutokidhi baadhi ya mahitaji ya tasnia ya filamu na kupelekea mahitaji ya kurekebisha Sera ya Utamaduni kama Sera mama na kutungwa kwa Sera ya Filamu.

Mnamo Desemba 12 mwaka 2013, wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo, Bodi ya Filamu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walishiriki katika kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu.

Wadau wengine ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Kazi na Ajira, BASATA, Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mtandao wa Muziki, Swahili Films, ROSAF, TAPAF, Umoja wa Mashirikiano wa Filamu, Filamu Cental, Chama cha Hakimiliki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho pamoja na G&S Associates and Advocates. 

Hata hivyo wadau ambao hawakushiriki walipewa nafasi na Serikali kuwasilisha maoni yao ambapo mwitiko umekuwa mzuri na maoni yanaendelea kupokelewa ili hatimaye kuwa na Sera bora na shirikishi.

Katika kikao hicho Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu iliwasilishwa kwa kuelezea historia fupi ya filamu nchini, vikao vya wadau vilivyofanyika vya mapendekezo ya kuwa na Sera ya Filamu kati ya mwaka 2004 na 2013, nyaraka kama Mpango Mkakati wa Bodi ya Filamu unaoonyesha haja ya kuwa na Sera ya filamu pamoja na kuelezea malengo mahususi na matamko ya Sera mpya inayopendekezwa kutungwa.

Aidha, wadau walijadili uzoefu wa nchi nyingine kama Kenya, Nigeria, China, Afrika Kusini, Marekani, Canada, India na Uingereza na matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika pamoja na Changamoto zinazoikabili Tasnia ya Filamu nchini. 

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau ni pamoja na kuwa Sera itamke uanzishwaji wa  Chuo cha Taifa cha Filamu, Sera itamke kuwepo kwa Mfuko ambao utasaidia katika kuimarisha Sekta ya Filamu na Sanaa za maonyesho kwa ujumla, Sera itoe tamko kuhusu kusimamia  maadili katika tasnia ya  Filamu na kudhibiti ukatili wa kijinsia katika  tasnia ya Filamu.

Pia walipendekeza kuwa hoja na matamko yawe na takwimu zaidi, Sera itamke namna ya kumlinda msanii wa Tanzania, mzalishaji wa ndani na wawekezaji, pamoja na kupiga vita udhalilishaji wa watoto wa kike.

Kwa upande mwingine, wadau hao walitoa pongezi kwa Wizara kwa kuandaa Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu iliyotokana na maoni mbalimbali ya wadau, Sera ambayo itaiwezesha Tasnia ya Filamu kupata mwelekeo bayana na kukidhi matakwa ya kila mdau katika tasnia ya filamu.

Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa imekua na inaendelea kushirikiana na wadau wa Filamu kwa kila hatua ili hatimaye ifanikishe azma ya kuwa na nyaraka zote muhimu katika kuendeleza, kusimamia, kuratibu na kukuza tasnia ya filamu nchini.

No comments: