MKURUGENZI wa Mashitaka Nchini (DPP), amemfutia mashitaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime (61) na kisha kumuunganisha na wenzake 11 na kuwasomea upya mashtaka 27 ya mauji katika mtaa wa Indira Gandh, yaliyotokana na kuporomoka jengo la ghorofa 16.
Mbali na Fuime washtakiwa wengine ni, Diwani wa Kata ya Goba, Ibrahim Mohamed maarufu kama Kisoki, Raza Ladha, Goodluck Mbanga, Willbroad Mugyabuso,Mohamed Abdulkarim, Charles Ogare, Zonazea Oushoudada, Vedasto Ruhale, Michael Hema, Albert Mnuo na Joseph Ringo.
Washtakiwa hao walisomewa hati mpya ya mashitaka baada ya kuondolewa hati ya zamani ya mauaji ya bila kukusudiwa na kuunganishwa Fuime na idadi yao kufikia 12, mbele ya Hakimu Mkazi Devota Kisoka.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka na Wakili wa Serikali Joseph Maugo.
Kongola alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu kidogo cha 294 kidogo cha (1) upande wa Jamhuri unaomba ridhaa ya mahakama ya kumuongeza mshtakiwa Fuime katika hati mpya ya mshitaka.
Hakimu Kisoka alisema mahakama haina pingamizi na maombi ya Jamhuri ya kubadilisha hati ya mashitaka dhidi ya washtakiwa.
Jamhuri ilidai kuwa katika shtaka la kwanza, Machi 29, mwaka 2013 mtaa wa Indira Gandh, Wilaya ya Ilala washtakiwa kwa pamoja walimuua kwa makusudi Yusuph Khari.
Alidai katika shtaka la pili na la tatu, Machi 29, mwaka 2013 washtakiwa waliwaua kwa makusudi Kulwa Alfani na Hamada Musa.
Katika shtaka la nne na la tano, ilidaiwa kuwa Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Kessy Manjapa na Khamis Mkomwa.
Kongola alidai katika shtaka la sita na la saba, Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa waliwaua kwa makusudi Boniface Bernad na Suhail Karim.
Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la nane na la tisa, Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Salmani Akbar na Selemani Haji.
Wakili wa serikali Maugo aliendelea kusoma hati hiyo ya mashtaka alidai katika shtaka la 10 na 11, Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Selemani Mtego na Sikudhani Mohamed.
Ilidaiwa katika shtaka la 12 na 13, Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Ahmed Milambo na Salum Mapunda.
Shtaka la 14 na 15, ilidaiwa kuwa Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Suleimani Mnyani na John Majewa.
Shtaka la 16 na 17, ilidaiwa kuwa Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Mussa Mnyamani na David Herman.
Kweka alidai katika shtaka la 18 na la 19 kwamba Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo washtakiwa waliwaua kwa makusudi William Joakim na Abdulrahman Mwiha.
Alidai katika shtaka la 20 na 21 kwamba Machi 29, mwaka 2013 mtaa wa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Jumanne Athuman
na Advai Mpinge.
Wakili huyo aliendelea kusoma hati hiyo, shtaka la 22 na la 23, alidai kuwa Machi 29, mwaka 2013 mtaa huo washtakiwa wote kwa mapoja waliwaua kwa makusudi Emmanuel Wahai na Agustino Chuma.
Katika shitaka la 24 na 25, ilidai kuwa Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Phillipo Kusimala na Said Abbas.
Maugo aliendelea kudai katika shitaka la 26 na 27, Machi 29, mwaka 2013 katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua kwa makusudi Bethod Mwanengule na Gabriel Kamwela .
Kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), mashitaka yanayowakabili washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote hadi pale upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusikilizwa.
Hakimu Kisoka alisema kesi hiyo itatajwa Machi 26, mwaka huu na washtakiwa dhamana yao imefutwa wapelekwe mahabusu.
Jana saa 3:00 asubuhi upande wa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Mmbando uliwasilisha hati ya Nole kutoka kwa DPP ikieleza kwamba hana nia ya kuendelea kumshitakiwa Fuime na kuomba kumfutia mashtaka hayo.
Hakimu Mmbando alifuta mashitaka hayo, lakini askari kanzu wa jeshi la Polisi walimuweka chini ya ulinzi na baadaye alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Kisoka na kuunganishwa na wenzake.
No comments:
Post a Comment