Saturday, March 1, 2014

MAMBO 6 YANAYOMFANYA MTU AWE KIONGOZI BORA NA SIO BORA KIONGOZI

Tukiacha mbali picha ambayo mara nyingi au kwa miaka mingi imekuwa ikijengwa  vichwani mwa wengi wanapoona na kudhani kwamba fulani ni kiongozi bora [pengine kwa muonekano tu], au kwa sababu anashuka kutoka kwenye gari kwa mbwembwe, tabasamu baada ya kufunguliwa mlango na mkanda na kisha kupokelewa briefcase yake, yapo mambo kadhaa ambayo yanamfanya mtu awe kiongozi bora na sio bora kiongozi. Na kadri siku zinavyokwenda, taswira ya kiongozi kwa muonekano tu inazidi kupotea. Vitendo,maadili,mafanikio, uvumbuzi na maendeleo vinachukua mstari wa mbele.

Tofauti na miaka ile ambayo picha ya kiongozi bora ilikuwa kama hiyo hapo juu, siku hizi viongozi bora wapo na wanajitokeza katika hali tofauti tofauti kabisa. Anaweza kuwa asiyevaa suti kama Dalai Lama na akawa kiongozi bora. Au asiyevaa suti bali t-shirt na jeans tu kama alivyokuwa Steve Jobs wa Apple au Mark Zuckerberg boss wa Facebook. Mifano ya viongozi hawa ipo mingi.

Kituo cha utafiti na mafunzo ya uongozi cha Dale Carnegie cha jijini New York nchini Marekani kinasema katika utafiti wao wamegundua kwamba kinachomfanya mtu awe kiongozi bora sio suti, briefcase, tabasamu[ hususani lile la uongo] bali uwezo na nia ya dhati katika kuamsha ari, kuwawezesha unaowaongoza, kuwafanya wajiamini na kuwapa motisha watu unaowaongoza.

Pamoja na hayo, na kutokana na ukweli kwamba leo hii tuna kila aina ya viongozi, yapo baadhi ya mambo yanayowatofautisha viongozi bora na bora viongozi. Haya hapa ni baadhi yake;
  • Aweze Kuyakabili Matatizo au Changamoto
Kiongozi bora ni yule ambaye ana ujasiri wa kutosha wa kukabiliana na kila aina ya changamoto au matatizo ambayo yanaweza kujitokeza iwe aliyatarajia au hakuyatarajia.

Dunia ya leo imejaa changamoto za kila aina. Kila kukicha kuna jipya na gumu zaidi. Uchumi umeporomoka, fedha haina thamani tena, kimbunga kikali kimekuja na kuipindua juu chini shule ya kijiji. Kiongozi bora anafanyaje? Anapotelea mjini kwa kisingizio cha kuwa “bize” au anakuwepo bega kwa bega kutatua tatizo?

Jibu lipo wazi. Kiongozi bora atakuwepo na kuwasiliana na kila mtu anayemuongoza iwe ni ofisini au jimboni kuhusu ukweli halisi na ukubwa wa tatizo na jinsi ambavyo yeye kama kiongozi analishughulikia [kwa kushirikiana na kila mtu wakiwemo anaowaongoza] tatizo au changamoto husika.
  • Awe Muaminifu
Kiongozi bora lazima awe muaminifu. Uaminifu unaanzia kwenye kuwa mkweli. Anaposema atafanya hili au lile, alifanye. Asipolifanya, awe muwazi na kuwaeleza wale anaowaongoza ukweli wa sababu zilizofanya asitimize ahadi yake na jitihada anazofanya kutimiza ahadi yake.

Kwa mfano wananchi wanapomchangua “kiongozi” kutokana na sera na ahadi za kutatua tatizo la ukosefu wa maji safi jimboni kwao kisha miaka mitano baadae ahadi hiyo ikawa haijatimia, ni wazi kwamba imani kwa kiongozi huyu itafifia kama sio kupotea kabisa. Mbaya zaidi pale atakapokuja na sababu ambazo hazina mashiko huku kila mtu akiona wazi kwamba ahadi yake ilikuwa ahadi hewa au ya kisiasa.

Onyesha kwamba unawajali na kuwathamini unaowaongoza. Yaelewe matatizo na changamoto za unaowaongoza. Shirikiana nao bega kwa bega kuyatatua. Usiwe kiongozi wa ofisini tu bali nenda kule walipo. Na usiende kwa nia ya kupigwa picha tu. Ili wakuamini ni muhimu wakaona kwamba wewe sio “mwizi” tu wa fursa.
  • Kuwa Halisi [Asiwe Feki]
Mojawapo ya mambo ambayo sio tu yanamfanya mtu awe bora kiongozi bali apoteze kabisa hata nafasi ya kuongoza ni pamoja na kuwa “feki”. Ni rahisi sana kwa mtu/watu kutambua kwamba huyu si yeye. Anajifanya kuwa mtu ambaye siye.

Kwa bahati mbaya hakuna mtu anayependa “feki”. Viongozi wanasiasa huanguka sana kwenye mtego huu. Wengi wanadhani wananchi hupenda kusikia mashairi na ngonjera tamu tamu pekee. La. Labda zamani. Siku hizi ukiwa kitimbakwila utajulikana kirahisi na utakuwa nje ya ulingo. Wenzetu wanasema Walk The Walk and Talk The Talk.

Hata kama wewe ni kiongozi wa ofisi au mfanyabiashara, pindi tu utakapokuwa “feki” wateja wako watajua. Watakukimbia. Watahisi hata vitu unavyouza ni “feki” kwa sababu wewe mwenyewe unaonekana feki au unajibeduisha kuwa sivyo. Kuwa orijino. Unapenda kucheka au kuchekesha? Cheka. Wachekeshe unaowaongoza. Unapenda muziki? Usihofu kuonyesha wazi kwamba unapenda muziki. Tumia vitu unavyovipenda au maarifa unayoyamudu zaidi kutengeneza aina yako ya uongozi.
  • Ajiheshimu
Kiongozi bora lazima ajiheshimu. Na dhana ya kujiheshimu ni pana. Kuna kujiheshimu katika nyumba na mahusiano yako iwe na wanao, mkeo, wazazi wako, ndugu, jamaa na hata marafiki. Kuna kuiheshimu ofisi yako na watu unaowaongoza. Kiongozi ambaye kila siku anakabiliwa na tuhuma za ulaji rushwa, uongo, umalaya ni wazi kwamba hajiheshimu na hivyo ni ngumu kuwafanya watu wengine wamheshimu. Nawajua baadhi ya “bora viongozi” ambao wametumbukia huko kutokana na tabia zao za ufuska ambazo ingawa wanahisi watu hawajui, kwa kiasi kikubwa zimewapotezea heshima ya uongozi na hususani uongozi bora.

Unapojiheshimu, inakuwa rahisi kuongoza wengine. Hakuna mtu anayependa kujishirikisha na mtu asiyejiheshimu. Watu hujisikia faraja kuhusiana au kufanya biashara na watu wanaojiheshimu. Pia hata kama unaongoza ofisi au biashara tu,wateja wenye akili timamu wanataka kutumia hela zao mahali ambapo ofisi au biashara inaheshimu na kutimiza ahadi zao kufuatana na misingi. Ukisema kwamba ninyi ndio duka lenye bei chee zaidi na bidhaa halisi, basi iwe ni kweli. Vinginevyo inaashiria kwamba hamjiheshimu. Ni waongo. Uongo ni sehemu ya kutojiheshimu.
  • Jifunze/ Taka Kujua Zaidi/ Nenda Na Wakati
Kiongozi bora ni yule ambaye anataka kujifunza zaidi na ni mtafiti. Mwisho wa darasa sio mwisho wa kujifunza kwa kiongozi bora. Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini aliwahi kunieleza katika mahojiano yangu naye jinsi ambavyo alishangaa wakati fulani kusafiri na viongozi fulani kutoka Tanzania mpaka Ujerumani na asione wakisoma hata vipeperushi vinavyokuwa kwenye viti achilia mbali vitabu,magazeti nk.Viongozi bora wanauliza maswali. Wanauliza maswali kwa nia ya kujifunza, kupata maarifa na taarifa. Ni wasikivu na wapo tayari kufundishwa.

Kwa bahati nzuri dunia ya leo ina kila nafasi na uwezekano wa kujifunza. Hizi ni zama za sayansi na tekinolojia. Kiongozi bora atataka kujua…hicho kitu kinachoitwa Twitter ni nini? Kinafanyaje kazi? Atajiunga. Atataka kujua jinsi watu wanavyowasiliana siku hizi. Atataka kujua jinsi nchi za wenzetu wanavyofanikiwa katika masuala mbalimbali. Atajitahidi na kuchunguza mpaka mwisho kuona kama sayansi hiyo au maarifa hayo yanaweza pia kutumika nchini kwake,jimboni kwake, ofisini kwake nk. Kiongozi bora atasoma vitabu,majarida,magazeti, nk kwa nia ya kujifunza zaidi.
  • Kuwa Mtendaji
Yote niliyoyataja hapo juu yanakamilishwa au kuhusishwa moja kwa moja na utendaji. Kiongozi bora haishii kwenye kuongea tu huku akijizungusha kwenye kiti na kuagiza chai. La.Anatenda. Ananyanyuka, kwenda na kutenda kama mfano. Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere kama kiongozi bora aliyewahi kutokea ni kwa sababu alikuwa mtendaji. 

Aliongea,kuelekeza,kuonya lakini mwisho wa siku alikuwa mtendaji.
Nyanyuka na enenda ukaifanye kazi. Onyesho kwa vitendo kwamba wewe ni kiongozi bora na sio bora kiongozi.
Jeff Msangi ni mwandishi, mchunguzi wa masuala mbalimbali na mmiliki wa mtandao wa www.bongocelebrity.com. Unaweza kuwasiliana naye kupitia jeffmsangi at gmail dot com

No comments: