Tuesday, February 18, 2014

waathirika wa kimbunga makete wazidi kupata msaada

Mkuu  Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro (kulia) akipokea msaada huo kwa niaba ya wananchi kutoka kwa mkurugenzi wa shirika la SUMASESU lililopo wilayani hapo
 Mkurugenzi wa shirika la SUMASESU Bw. Egnatio Mtawa akizungumza wakati akikabidhi msaada wa bati 25 na misumari kwa ajili ya waathirika wa kijiji cha Ndulamo
 mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akizungumza wakati akipokea msaada huo kwa niaba ya wananchi

Na Edwin Moshi
Janga la kuezuliwa nyumba 11 katika kijiji cha Ndulamo wilayani Makete mkoa wa Njombe limeonesha kugusa wadau mbalimbali, ambapo shirika lisilo la kiserikali la SUMASESU lililopo wilayani hapo limetoa msaada wa bati 25 na kilo 5 ya misumari vyote vikiwa na thamani ya tsh. 325,000/=.
Akikabidhi msaada huo hii leo Mkurugenzi wa SUMASESU Bw. Egnatio Mtawa  amesema shirika lake limekuwa linafanya kazi kwa asilimia kubwa ndani ya wilaya ya Makete hasa na watu wazima (wasio na maradhi) hivyo wameguswa na janga hilo na kuona njia mojawapo ya kuwasaidia ni kutoa bati na misumari kulingana na uwezo wa shirika hilo.
Bw. Mtawa amesema kupitia matatizo mbalimbali yanayoigusa jamii ni vyema wanamakete wakawa na mshikamano na kuwasaidia wananchi pale wanapopata matatizo mbalimbali kwa kuwa hawajapenda kupata madhara hayo.

"Tumesikia kwenye vyombo vya habari maafa yaliyowakumba wenzetu wa Ndulamo, kwa kweli ni janga kubwa na hawawezi kulimaliza wenyewe ila kwa mshikamano wetu wa pamoja ni hakika tutaweza kuwasaidia kuondkana na kero hii iliyowakumba" alisema Mtawa.
Akipokea msaada huo mbele ya viongozi wa kijiji hicho Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro amemshukuru mkurugenzi  huyo kupitia shirika lake la SUMASESU kwa kutoa msaada huo na kuongeza kuwa msaada huo utakuwa msaada mkubwa kwa waathirika hao.
Amesema anaimani wapo wananchi wenye uwezo na wenye mapenzi mema ya kusaidia kuendelea kujitokeza kwani muda bado upo na unahitajika ili usaidie kutatua tatizo hilo mapema.
"Kwa kweli kitendo kilichofanywa na SUMASESU kama wadau wa maendeleo wilayani Makete, ni cha kuigwa na kimesaidia sana, naomba wanamakete, ama wananchi wenye mapenzi mema kuendelea kutoa misaada yao ya hali na mali, si lazima uwe msaada mkubwa, hata bati moja linatosha" amesema Matiro.
Naye mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Liliyo Tweve ameshukuru kwa kijiji chake kupatiwa msaada huo na kusema kuwa hivi sasa kazi ya kujenga nyumba hizo zilizoezuliwa inaendelea vizuri na msaada huo utarahisisha ujenzi kukamilika mapema
Amesema Maazimio ya mkutano uliofanyika jana kijijini hapo yanaendelea vyema na inategemewa ndani ya wiki mbili zijazo kazi hiyo iwe imekwisha

No comments: