DAR ES SALAAM, Tanzania.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amecharuka na kusema kwamba Wana-CCM ambao wameanza sasa kutangaza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani, ni wasaliti wakubwa ndani ya Chama.
Mangula, ametoa karipio hilo, leo (jana) wakati akitoa Salamu za Mwaka Mpya wa 2014 katika mkutano wa dharura wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Tawi la Ofisi Ndogo ya Makao Makuu jijini Dar es salaam.
Huku akinukuu kanuni zinalzolinda Maadili ya Uchaguzi na uteuzi wa wagombea ndani ya Chama, Mangula, alisema hadi sasa hakuna kikao chochote cha ngazi ya juu cha Chama, kilichoruhusu wanachama kuanza kutangaza nia za kugombea uchaguzi hadi pale itakapofika mwaka 2015.
Makamu huyo wa CCM (Bara), alisema, wanachama wanaojipitisha sasa kwa wananchi kwa namna moja au nyingine kwa lengo la kutangaza nia ya kuwania nafasi katika uchaguzi mkuu ujao, ilihali muda wa kufanya hivyo haujafika ni wasaliti au waasi ndani ya Chama.
Mangula alisema, wanaofanya hivyo ni waansi na wasaliti wakubwa kwa sababu wanaibua na kuendeleza makundi mapemba huku wakijua kwamba hali hiyo hukifanya chama kuwa na wakati mgumu wakati wa uchaguzi.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza kuwa Chama, hakipo tayari kuona au kuwavumilia watu wachache ndani ya Chama wanaoendelea kuvuruga umoja, mshikamano na misingi ya Chama kwa sababu tu ya umangimeza na uroho wa madaraka uliokiuka kiwango.
Mangula aliwataka wana-CCM na kwa jumla wakiwemo hao wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, kuzingatia wakati wote misingi mizuri ambayo itawezesha kupatikana viongozi wazuri ambao hawatokani na mianya ya rushwa ili kuwa na dira nzuri kuelekea katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika 2015.
CHANGAMOTO
Wakati Mzee Mangula akiendelea kutoa karipio hilo kwa wanaojitangaza kabla ya wakati kuwania uongozi katika nafasi mbali mbali kabla ya wakati katika uchaguzi mkuu ujao, wapo viongozi kadhaa, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli Edward Lowassa wamekuwa wakifanya matukio na kuzungumza kauli ambazo huonyesha wazi wanajipigia chapuo la kwania Urais 2015.
Akizungumza katika Ibada mwaka mpya kwenye kanisa la KKKT Monduli, Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikaririwa akisema kuwa mwaka 2014 ni mwanzo wa safari ya kutimiza ndoto zake za kuona Watanzania watapata elimu bora na bure, na pia kuondokana na umasikini na kwamba ana imani kwa nguvu na msaada wa mungu atafika.
"Safari hii ina miba, milima na mabonde, lakini kwa msaada wa Yesu nitafika", alikaririwa Lowassa huku mwandishi akisema kiongozi huyo alisema bila kufafanua ni safari ya Kuelekea wapi.
"Hata hivyo Lowassa amekuwa miongoni mwa wana CCM wanaotajwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, ingawaje hajatangaza rasmi", alifafanua mwandishi huyo.
Lowassa alikaririwa zaidi akisema, "Safari hii tumeianza yenye matumaini, yenye ndoto za mtanzania za kuwa na elimu bora na bure,ndoto ya mtanzania kuwa na elimu makini,ndoto ya mtanzania kuwa na maji safi, ndoto ya mtanzania kuwa na matumaini ya maisha".
Kwa mujibu wa mwandishi huyo, kwa upande mwingine, Lowassa aliwataka wale wanaomuunga mkono kutokuogopa kufanya hivyo hadharani, na kuongeza kuwa wakati ndiyo huu wa kufanya hivyo.
Wakati Viongozi wa CCM, kama Mzee Mangula wakipaza sauti kupinga wana-CCM kujinadi kabla ya wakati kuwania au kugombea nafasi mbali mbali katika uchaguzi mkuu ujao, baadhi ya viongozi wa CCM wakiwemo Wenyeviti wanaonekana kushabikia kinachokatazwa.
Katika karamu ya cha kila ambayo Lowassa anadaiwa kuwa huifanya kila mwaka, ambayo aliifanya mwaka mpya, Monduli, viongozi kadhaa wa CCM waliudhuria na kuzungumza, ambapo Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM nchini, Mgaya Msindai ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Singida, alikaririwa akitangaza rasmi kuwa Wenyeviti wa Chama hicho wako nyuma ya Lowassa katika safari yake hiyo.
"Napenda kuwaumbua ndugu zangu kuwa sisi wenyeviti wa CCM tuko pamoja na Mh Lowassa katika safari yake hiyo, kwa sababu tunajua nguvu na uwezo wake katika kuwatumikia wananchi ", alikaririwa Msindai akisema.
Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Umoja wa Vijana wa CCM Nchini, Manko Hiru ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mara alikaririwa pia akitangaza kwenye chakula hicho kuwa Vijana wanamuunga mkono Lowassa.
"Sisi Vijana ni wapiganaji wako (Mh Lowassa ) wewe ni jemedari kwa hiyo jemedari hua wa mwisho kufa, sasa Kama kufa sisi Vijana ndiyo tutakuwa wa kwanza kufa kabla yako, tutakukinga, sisi UVCCM ni ngao yako" alikaririwa akisema.
Mbali na viongozi hao, mbunge wa kuteuliwa UWT mkoa wa singida, Diana Chilolo ambaye ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM, Tanzania, naye alikaririwa akisema wanawake wana matumaini makubwa na Lowassa.
"Tuna matumaini makubwa sana na wewe Mh Lowassa kwani uwezo wako unajua Ilani na kila mtanzania, wanawake wanakuunga mkono kwa dhati katika safari yako"alikaririwa Diana akisema katika hafla hiyo inayoelezwa kuhudhuriwa na wageni zaidi elfu nne kutoka kila pembe ya Tanzania.
RASIMU YA PILI KATIBA MPYA
Akizungumzia kuhusu msimamo wa Chama Cha Mapinduzi katika muundo wa serikali tatu uliomo katika rasimu ya Pili ya Rasimu ya Katiba mpya, iliyowasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete hivi majuzi, Mangula alisema msimamo wa CCM kuhusu hili unajulikana lakini hakuna sababu ya kuzungumzia kwa kina kwa sasa kwa kuwa mchakato bado mrefu.
Alisema, alisema, licha ya kwamba msimamo wa CCM unajulikana hadi sasa kuhusu hilo la serikali tatu, bado uamuzi wa mwisho ambao upataswa kuheshimiwa na kila mtu ni wa mwananchi wenyewe baada ya kufanyika kura ya maoni ya katiba.
"Nataka kanuni za uchaguzi na uongozi na maadili ziheshimiwe ili kupata viongozi ambao hawatatokana na rushwa, na hakikisheni katika vikao vyenu vya chama mnasimamia agenda mbili ambayo ni uchaguzi na kujadili mwenendo wa katiba mpya” Mangula aliiasa Kamati ya Siasa ya Ofisi Ndogo na kuongeza.
“Mkifualia hatua moja hadi nyingine katika mchakato wa kuipata katiba kuanzia ushiriki wa wajumbe wa bunge maalum hadi katika mjadala wa wajumbe wakipitia kifungu kimoja hadi kingine mtakuwa na nafasi kubwa ya kutoa maoni yenu pale itakaporudi kwa wananchi".
Mbali na kuwapongeza tume ya katiba mpya kwa kufanya kazi kwa uwazi, amewapongeza wanachama wa CCM kwa jinsi walivyoshirikia mmoja mmoja au katika makundi katika kuhakikisha wanatoa maoni yao katika rasimu ya katiba ambayo tayari imewasilishwa kwa Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment