Wednesday, January 15, 2014

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana inavyompa Kijana Fursa ya Kujitambua na kujiamini

Na Benjamin Sawe,WHVUM

“Vijana ni nguvu kazi ya Taifa”. Hii ni kweli na kwa mujibu wa utafiti wa Nguvu Kazi Nchini ya mwaka 2006 asilimia 68% ya nguvu kazi nchini ni Vijana ambao idadi yao kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni 15,587,621 sawa na asilimia 34.7% ya idadi ya watu wote nchini. Kati yao Vijana wa kike ni 8,273,505 sawa na asilimia 35.9% na Vijana wa kiume ni 7,314,116 sawa na asilimia 33.4%.

Kutokana na umuhimu huu, kumekuwa na jitihada mbalimbali za Serikali zinazolenga katika masuala ya maendeleo ya Vijana nchini hii ikiwa ni pamoja na kuwa na Sera, Mipango na Mikakati inayokidhi mahitaji mbalimbali ya vijana kama vile, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007,Sera ya Taifa ya Ajira 2008 (Iliyo chini ya Wizara ya Kazi na Ajira), Mpango Kazi wa Taifa wa Ajira kwa Vijana 2007 na Programu ya Kukuza Ajira zenye Staha kwa Vijana nchini inayoratibiwa kati ya Wizara Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi anasema Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 ni matokeo ya maboresho ya Sera ya Vijana ya mwaka 1996 ambapo, maboresho ya Sera hiyo yanatokana na mabadiliko, mahitaji au changamoto mbalimbali zinazojitokeza za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Vilevile, suala la ukuaji wa kasi ya Sayansi na Teknolojia huilazimu Serikali kufanya maboresho muhimu ili kuendana na wakati. Anasema Bwana Kajugusi. Anafafanua kuwa msukumo mwingine unaopelekea kufanyika kwa maboresho ya Sera ni pamoja na utekelezaji wa maazimio yanayofikiwa na Tanzania ikiwemo kama vile Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, EAC, SADC na AU.

Aidha kwa upande mwingine Sera hutoa Mwongozo na Dira kwa wadau mbalimbali kuweza kutekeleza yale ambayo yametamkwa kwenye Sera hiyo. Hivyo, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 inatoa fursa kwa vijana kujiamini na kujitambua.

Bwana Kajugusi anasema, Ibara ya 3(3), Sera inatamka kuwa “kutakuwa na utaratibu wa kutoa mwongozo kwa ajili ya kuwezesha malezi sahihi ya Vijana na kuendeleza vipaji vya Vijana”.

Hivyo katika kutekeleza tamko hilo la Sera, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya Vijana nchini imeweza kuandaa programu za kuwawezesha Vijana kujiamini na kujitambua kama vile “Programu ya Stadi za Maisha kwa Vijana Nje ya Shule”

Anasema Vijana wengi waliopata elimu hiyo, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadili fikra na kuchukua hatua ya maendeleo katika kufanyia kazi vipaji walivyokuwa navyo ambapo ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007. Pia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 vilevile inatambua umuhimu wa ushiriki na ushirikishwaji wa Vijana katika kubaini na kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya ustawi wa maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

Aidha ukirejea tamko la Sera Ibara ya 3(4) inasema kuwa “Kazi ya kuhamasisha upatikanaji wa ardhi na katika kutenga rasilimali nyingine itafanyika. Msisitizo utaelekezwa kwa vijana wa vijijini na usawa wa kijinsia kama ilivyoelezwa katika Sera ya Biashara Ndogondogo na za Kati, Mkakati wa Maendeleo Vijijini na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsi”.

Bwana Kajugusi anafafanua kuwa Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya Vijana nchini, katika kutekeleza tamko hilo Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za Vijana ikiwa ni sehemu mojawapo ya juhudi za Serikali za kutengeneza ajira zenye staha kwa Vijana nchini kulingana na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

Anasema changamoto zilizopo za ajira kwa Vijana si tatizo la Kisera kwani Sera inatamka wazi kwenye Ibara 3(9) kuwa; “Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi itaandaa mazingira yanayowezesha kujenga fursa za ajira kama ilivyoelezwa katika Sera ya Taifa ya Ajira, Mkakati wa Maendeleo Vijijini na Sera ya Maendeleo ya Kilimo”

“Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya sekta binafsi, vyama vya kiraia, vyama vya vijana na jamii ya wafanyabiashara itahimiza kujenga utamaduni wa ujasiriamali kwa kujenga mazingira yanayowezesha maendeleo ya biashara kwa vijana”

Kumekuwepo na jitihada mbalimbali za Serikali na wadau wa maendeleo ya Vijana nchini katika kutekeleza matamko haya ya sera, kwa mfano Uhamasishaji wa uundaji wa vikundi vya uzalishaji mali vya Vijana ambapo kupitia vikundi vya Vijana inakuwa ni rahisi kwa Serikali na kwa wadau mbalimbali wa Vijana kuweza kuwafikia Vijana na kuwawezesha

Aidha Serikali imetoa na inaendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwenye vikundi vya Vijana ambapo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 jumla ya viongozi wa vikundi vya vijana 905 waliweza kunufaika na mafunzo hayo. Mafunzo haya yaliratibiwa na Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo.

Jitiada nyingine zinazofanywa na Serikali ni pamoja na Utoaji wa mikopo na ruzuku yenye masharti nafuu kwa vikundi vya Vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo na “Youth to Youth Fund” inayoratibiwa kati ya Wizara ya Kazi na Ajira na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Ruzuku kupitia Benki ya CRDB kwa Vijana wahitimu wa Vyuo Vikuu.

Jitihada zote hizo zinalenga katika kufikia malengo na mikakati mbalimbali ya kukuza ajira kwa Vijana nchini kama zilivyoainishwa kwenye Sera ya Maendeleo ya Vijana 2007, Sera ya Ajira 2008, Mpango Kazi wa Taifa wa Ajira kwa Vijana 2007, MKUKUTA II na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Takwimu za Nguvu Kazi Nchini za mwaka 2006 zinaonesha kuwa, kiwango cha tatizo la ajira kwa Vijana lipo kwa asilimia 13.4% ambapo Sensa ya Watu na Makazi 2012 inabainasha kuwa:-Vijana walioajiriwa katika Sekta ya Umma ni 188,087 ,Vijana walioajiriwa katika Sekta Binafsi ni 1,028,634, Vijana waliojiajiri wenyewe ni 1,102,742 na Vijana wanaojishughulisha na kilimo ni 13,200,200.

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 pia inatambua umuhimu wa Vijana wa kuwa na utambulisho wa Taifa kupitia Sanaa na Utamaduni na inatamka wazi kwenye Ibara ya 3(20) kuwa; “Kutakuwa na utaratibu wa kulinda taratibu za kiutamaduni zinazokubalika na kuhamasisha na kutunza maadili ya utamaduni wa Kitanzania miongoni mwa vijana, wakati huohuo ukiwalinda watoto na athari mbaya za utamaduni wa kutoka nje”.

Ni wazi kuwa jukumu la kuhakikisha kuwa maadili ya Vijana nchini yanaboreshwa si ya Serikali peke yake bali ni ya kila mtu mmoja mmoja kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 4.0 hadi Ibara ya 4(5) ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007.

Sio kweli kuwa hadi kufikia mwaka 1996 hapakuwa na Sera ya Vijana. Ukweli ni kuwa, kila Sekta ilikuwa na Sera na utaratibu wake wa kuwahudumia vijana. Mfano, katika sekta ya elimu Vijana walihudumiwa kupitia Sera na sheria za elimu.

Alikadhalika, Sekta ya maendeleo ya jamii walitumia Sera ya maendeleo na ustawi wa jamii katika kuwahudumia vijana. Kwahiyo, Sera ya Vijana ya 1996 ilikuwa ni Sera jumuishi (harmonized policy) ambayo ililenga kuboresha maisha ya Vijana na kuwaendeleza katika nyanja za Kiuchumi, Utamaduni, Siasa, Malezi na Elimu.

Tanzania ni nchi mwanachama wa Jumuiya mbalimbali za kikanda ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Katika Jumuiya hizi, masuala ya Vijana yanapewa kipaumbele kikubwa. Tumejiunga katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki tukiamini kuwa tunayo Sera ya kumlinda kijana.

Ibara ya 3(26) ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 2007 inatamka kuwa “Serikali itaweka utaratibu wa kuimarisha programu za kimataifa za maendeleo ya vijana na kuhimiza ushirikiano wa kimataifa”.

Katika kutekeleza tamko hilo la Sera, Serikali imebuni programu za kuwezesha Vijana wa Kitanzania kupata fursa ya kubadilishana uzeofu na Vijana wenzao kupitia Jumuiya mbalimbali ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mantiki hii, si kweli kama jinsi ilivyojengeka dhana kuwa Vijana wa Kitanzania hawatakuwa na uwezo wa kushindana na Vijana wenzao katika soko la ajira kupitia Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Kwa mfano mwaka 1995 hapakuwa na Sera ya Vijana, bali Sera hii ilianzishwa mnamo mwaka 1996. Sera ya Vijana ya mwaka 1996 iliendeleza jitihada zilizoanzishwa za kuwahimiza Vijana kushiriki kwenye shughuli za kujitolea kupitia Azimio la Arusha ya mwaka 1967 kuhusu Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Pia Kumekuwa na mafanikio mengi kupitia programu za kujitolea zilizoanzishwa na Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya Vijana nchini ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii, kama vile afya na elimu.

Hivyo ni wazi suala la kujitolea kwa Vijana limepewa msisitizo wa kutosha na Serikali kwa kutambua kuwa kupitia programu za kujitolea, zitasaidia kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.

Aidha Wadau wa Maendeleo ya Vijana Nchini wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa programu hizi za kujitolea zinaendelea kuboreshwa ili mabadiliko haya yaweze kuonekana katika jamii zote nchini.

Mwisho, ni muhimu kufahamu kuwa Sera ni kitu hai, Sera hufanyiwa mapitio mara kwa mara ili kubaini ufanisi katika utekelezaji wake, kubaini mapungufu na kubaini mahitaji mapya ili kuendelea kuwa na Sera inayokidhi haja kwa walengwa.

No comments: