Sunday, January 19, 2014

MAALIM SEIF AHUTUBIA MKUTANO WA HADHARA WILAYANI KISARAWE,MKOANI PWANI

Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Msanga, Wilaya ya Kisarawe.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Msanga, Wilaya ya Kisarawe.
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa CUF Taifa bw. Abdul Kambaya, akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Msanga, Wilaya ya Kisarawe.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi baiskeli kwa nd. Khamis Salum mwenye ulemavu, mkaazi wa Kisarawe.
Wasanii wakitoa burdani kwenye mkutano wa CUF uliofanyika kijiji cha Msanga Wilayani Kisarawe.
Baadhi ya wananchi wakifuatilia mkutano wa CUF uliofanyika kijiji cha Msanga Wilayani Kisarawe. (picha na Salmin Said, OMKR).

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewashauri wananchi wa Kisarawe kuachana na vyama vilivyopoteza muelekeo, na badala yake kukiunga mkono chama chenye dira ya kuwaletea maendeleo.

Amesema hatma ya maendeleo ya wananchi iko kwa wananchi wenyewe, na kwamba ndio wenye maamuzi ya kuchagua uongozi wanaoutaka kwa maendeleo yao na taifa kwa jumla.

Akizungumza na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Msanga sokoni Wilaya ya Kisarawe, Maalim Seif amesema mabadiliko ya kiuongozi yanahitajika katika kuwakomboa wananchi kiuchumi na kijamii.

Amesema ni jambo la kushangaza kuona Tanzania imeachwa nyuma kimaendeleo katika kipindi cha miaka 53 ya uhuru, huku nchi nyengine zilizokuwa hadhi sawa na Tanzania zikipiga hatua kubwa za maendeleo.

Amezitolea mfano baadhi ya nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo kuwa ni pamoja Singapore na Malaysia, nchi ambazo zilikuwa maskini kuliko Tanzania, na kwamba Tanzania ina mengi ya kujifunzo kutoka nchi hizo.

“Singapore na Malaysia zilikuwa nchi maskini kuliko nchi yetu, lakini sasa zamepaa hadi dunia ya pili kuelekea ya kwanza kwa maendeleo. Hii imetokana na uongozi na mipango bora ya maendeleo waliyojiwekea”, alifafanua Maalim Seif.

Amefahamisha kuwa kitu cha kushangaza ni kuona Tanzania ina rasilimali nyingi zaidi kuliko nchi hizo lakini imedumaa kimaendeleo, jambo ambalo linapaswa Watanzania walitafakari kwa kina na kulitafutia ufumbuzi muafaka.

Amesema iwapo chama cha CUF kitapewa mamlaka ya kuongoza dola, kitahakikisha kuwa kinaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa Tanzania, ili kutoa fursa kwa wataalamu wa Itikadi tofauti za vyama vya siasa kushiriki katika serikali na kuwa kichocheo cha maendeleo.

“Nani mwana uchumi mzuri Tanzania kuliko Profesa Lipumba, lakini maskini hayumo kwenye serikali kwa sababu tu ni mpinzani, sasa sisi tukipata serikali hatutofanya makosa kama hayo”, alihoji na kusisitiza.

Mhe. Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametumia hiyo kuwaeleza wananchi wa Kisarawe juu ya mafanikio yaliyopatikana Zanzibar tangu kuanzishwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amesema kuundwa kwa serikali hiyo kumetokana na maamuzi ya wananchi wengi wa Zanzibar, na kuwabeza wale wanaoubeza mfumo huo ambao pamoja na mambo mengine umerejesha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari.

Ametaja mafanikio mengine ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa ni pamoja na kuongezwa kwa bei ya karafuu kutoka shilingi elfu tatu hadi elfu 15 kwa kilo moja, pamoja na  kupunguzwa kwa gharama za pembejeo za kilimo.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa CUF bw. Abdul Kambaya amesema bado Wilaya ya Kisarawe inakabiliwa na matatizo ya miundombinu ya barabara, elimu na afya.
Amewashajiisha wananchi wa Wilaya hiyo kubadilisha mfumo wa uongozi, ili kuwezesha rasilimali za nchi ziweze kutumika vizuri kwa maslahi ya wananchi wote.

Kabla ya mkutano huo Mhe. Maalim Seif alifanya ziara ya kichama katika Wilaya hiyo na kufungua matawi ya CUF, pamoja na kukabidhi baiskeli ya matairi matatu kwa ndugu Khamis Salum mwenye ulemavu, ili iweze kumsaidia katika harakati zake za kimaisha.

Hassan Hamad, OMKR.

No comments: