Friday, January 24, 2014

DK KAMANI AFUNGUKA: AWATAKA WAFANYAKAZI WASIOENDANA NA KASI YAKE WAJIONDOE MAPEMA

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dr. Titus Kamani, amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya wizara hiyo, inahitajika dhana ya uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea kwa nguvu zote katika kufanya kazi.

Waziri Kamani, ameyasema hayo leo katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo, wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema kama kuna mtu ambaye ni kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya kuwafanya watanzania wajue wizara inafanya nini.

“Wewe upo ofisini, halafu unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani, kuweni wazi mambo yenu yawe hadharani, watanzania wa Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba, hakuna kufichaficha jambo katika wizara yangu.” Alisistiza Dk Kamani.

Amesema wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni wizara ya yenye migogoro na kuleta hasara maeneo mengine.

“N’gombe hawa wamekua wakiingia kwenye hifadhi, wanapigwa risasi, wanaaribu mashamba ya watu na kuleta njaa kwa wananchi, ngombe hawa wamekuwa wakiambiwa wanaleta uharibifu wa mazingira kwa wananchi kwa sababu ya kuhamahama, kama ngombe hawa ungepatikana utaratibu mzuri wa kuwatunza, kuwahifadhi basi, taifa hili lingeingiza kipato kikubwa ikiwemo kuuza nyama hadi nje ya nchi, maziwa na kuboresha afya za watanzania” alisema Dk Kamani.

Dk. Kamani, amesema anafahamu Wizara yake ina changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo bajeti kuwa ndogo, lakini kwa kutumia taaluma yake pamoja na ushirikiano wa wafanyakazi wote wa wizara hiyo, anaamini wizara hiyo badala ya kuonekana ni laana kwa watanzania, itakuwa ni wizara yenye neema kwa watanzania, yenye kueneza ajira na kipato kwa sababu hakuna jambo lisilowezekana kama kila   mmoja atafanya kazi kwa dhamira moja.

Akizungumzia juu ya ranchi za taifa, waziri Kamani amesema ana nia ya dhati ya kuona ranchi za taifa zinafufuka na kutengeneza uchumi imara wa taifa, kuzalisha Ngombe wenye ubora ambao watatoa mazao ya mifugo yatakayoliingizia taifa hili kipato kikubwa.

Akizungumzia sekta ya uvuvi, Waziri Kamani, amesema sekta hiyo ni tabu tupu, amesema leo tunaambiwa kuna uvuvi haramu, nyavu zisizokidhi viwango, huku wavuvi wakiendelea kuwa masikini, katika nchi yenye bahari, maziwa na mito mikubwa kila kona, ameuliza ni kweli wanahitaji bajeti kubwa ya kushughulika na mambo hayo?.

“Tunahitaji utashi wa kuwasadia wavuvi wetu, kwa kutoa elimu na kufanya mazungumzo nao ya mara kwa mara, kuwatembelea maeneo yao ya kazi na kubaini matatizo yao kisha kuyafanyia kazi” Alibainisha Dk Kamani.

Kuhusu zao la kuku, Waziri Kamani amesema sasa hivi kuna tatizo la mayai feki na chanjo feki, alihoji ni kweli kwamba wafanyakazi wa wizara hiyo haiwajui wahusika au kuna baadhi ya watumishi ndio miradi yao? ambapo aliagiza wizara kubaini wanaofanya biashara hiyo feki ambayo inaleta madhara hasa wakazi wa mjini ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa hizo.

Awali, kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo Dk Yohana Budeba alipongeza uteuzi wa Dk Kamani, kuingia katika wizara hiyo kwakuwa ajira yake ya kwanza mwaka 1982 alikuwa chini ya wizara hiyo kama afisa Mifugo wa kata ya Kisongo wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, hivyo changamoto nyingi anazifahamu, ni mwenzao na anaamini watashirikiana vyema katika kukabiliana nazo.

No comments: