Sunday, January 26, 2014

BALOZI SEIF ATEMBELEA Vijiji vya Uzi na N’gambwa, Unguja

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuifanyia utafiti wa kina na hatimae kusaidia kugharamia ujenzi wa kudumu wa Bara bara itokayo Unguja Ukuu kuelekea Uzi Kisiwani yenye urefu unaokadiriwa kufikia Kilomita Mbili Nukta Sita ambayo hivi sasa bado iko katika kiwango cha mawe matupu. 
Ombi hilo limetolewa na Wananchi wa Vijiji vya Unzi na N’ambwa mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ndani ya Jimbo la Koani kuangalia maendeleo na matatizo yanayowakabili wananchi wa Jimbo hilo liliomo ndani ya Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. 
Balozi Seif Ali Iddi akipata wasaa wa kuikagua kwa kina Bara bara hiyo ya Unguja Ukuu hadi uzi ambapo Wananachi wa Vijiji hivyo chini ya Mwenyekiti wao wa Ujenzi wa Bara bara hiyo Mzee Shaya Mohd hawakuchelea kumuelezea kadhia wanayopambana nayo wanapovuka sehemu hiyo hasa wakati wa maji Makuu. 
Mzee Shaya Mohd alifahamisha kwamba Wananchi wa Vijiji hivyo wamefikia hatua ya kukata tamaa kutokana na kadhia ya maji yanayosababisha kupangua mfumo wa mawe licha ya juhudi kubwa wanazozichukuwa katika kupanga mawe hayo katika kila baada ya kipindi kifupi. 
Alisema baadhi ya wananachi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa hasa akina Mama wajawazito wakati mwengine hulazimika kujifungulia njiani kutokana na kadhia ya Bara bara hiyo jambo ambalo huleta hatari kwa mazingira ya mzazi na motto mwenyewe. 
“ Bara bara yetu iliwahi kufanyiwa Utafiti na hatimaye kujazwa mchanga katika katika Bara bara hii katika miaka ya thamanini lakini kilichojitokeza mara baada ya kupunguwa kwa kiwango cha maji makuu mchanga wote uliowekwa umekwenda na maji hayo “. Alifafanua Mzee Shaya Mohd Haji. Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu hadi Uzi - N’gambwa alifafanua kwamba njia pekee ya kukabiliana na tatizo hilo kulingana na mfumo wa maji ya bahari yanayokata katika eneo hilo ni kutumiwa kwa saruji,kokoto na mawe kwenye ujenzi wa Bara bara hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu katika matumizi yake. 
Akielezea kadhia ya ukosefu wa huduma ya Maji safi na Salama ndani ya Kijiji cha N’gambwa naye Mzee wa Kijiji hicho Bwana Khatib Mussa alimsikitikia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Wananchi wa Kiji hicho wanashindwa kuendelea vyema na harakati zao za kimaisha kutokana na muda mwingi kuutumia katika kutafuta huduma hiyo. 
Mzee Khatib Mussa alifahamisha kwamba huduma za maji safi ambazo ziliwahi kufika Kijijini hapo katika miaka michache iliyopita lakini hivi sasa zimekatika kabisa na kuifanya jamii ya kijiji hicho kuwa katika mazingira ya hatari kiafya. Akizungumza na Wananachi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa kwa nyakati tofauti Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Miundo Mbinu Zanzibar kuiweka katika Bajeti yake ya Mwaka Ujao Bara bara hiyo ili Serikali ipate fursa ya kuitengea fedha za ujenzi. Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona matatizo yanayowakabili wananchi wake katika maeneo mbali mbali hapa Nchini yanapatiwa ufumbuzi wa kina. 
“ Kwa kweli tunataka kuona Vijiji vya Uzi na N’gambwa ndani ya Jimbo la Koani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja vinabadilika na kuwa vya kisasa ili vilingane na vijiji vyengine hapa Nchini “. Alieleza Balozi Seif. Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kuchangia Matofali 1,000 pamoja na saruji Mifuko 10 kwa ajili ya kuongeza nguvu za ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Uzi linalotayarishwa kwa ajili ya wanafunzi watakaoingia Elimu ya Sekondari hapo mwakani. Balozi Seif pia akaahidi kuzipatia seti moja moja na mipira miwili kwa kila Timu za Soka za Wanawake wa Vijiji vya Bungi na Kidimni pamoja na kuitaka Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu Uzi kufanya makisio ya ujenzi wa Banda la Hifadhi wakati wa kujaa kwa maji liliopo kwenye jiwe kubwa la Kihistoria kati kati ya Bara bara hiyo. Naye Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdullah Shaaban akitoa ufafanuzi katika Mkutano wa Hadhara wa Wananachi hao juu ya tatizo la Maji safi na Salama Uzi na N’gambwa alisema Wizara hiyo iko katika hatua za mwisho kutafuta Pampu kubwa itakayokuwa suluhu ya tatizo hilo. Hata hivyo Waziri Shaaban alifahamisha kwamba katika juhudi za kuisaidia nguvu Pampu hiyo wataalamu wa Wizara hiyo wanatarajia pia kujenga Tangi la Maji kati kati ya Vijiji vya Uzi na N’gambwa ambalo litakuja kusaidia kusambaza kwa uhakika huduma hiyo. Akisoma Risala ya Wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Vijiji hivyo Ndugu Abdu Mohd Khamis alisema Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu hadi Uzi tayari umeshagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni Mia 166,019,000/- hadi sasa. Ndugu Abu Mohd alisema kati ya fedha hizo Shilingi Milioni 124,633,000 ni nguvu za Wananchi, Shilingi Milioni 25,786,000 zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Koani na Shilingi Milioni 15,600,000 zikatolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo la Koani. Alisema wananchi wa Vijiji hivyo wameishukuru Idara ya Ujenzi wa Bara bara Zanzibar { UUB } kwa hatuzake za mashirkiano na wananachi hao yaliyopelekea kwa kiasi kikubwa kuwawezesha kuitumia kwa unafuu Bara bara hiyo. Mjumbe huyo wa Kamati ya Maendeleo alisema Vijiji hivyo pia vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za Umeme ambalo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif tayari ameshaiagiza Wizara inayohusika na masuala ya Umeme kulibeba jukumu hilo kwa kutafuta nguzo 10 na waya zake ili kuliondosha tatizo hilo. Othman Khamis Ame Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 26/1/2014.
  Baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa  wadogo kwa wakubwa wakiendelea na harakati za matengenezo ya barabara yao itokayo Unguja Ukuu hadi Uzi kila baada ya kupungua kwa kina cha maji.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja     Ukuu – Uzi Bwana Shaya Mohd akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif eneo lenye kupitisha maji mwengi ambayo huleta kadhia kwenye barabara yao.
 Balozi Seif akikagua barabara ya Unguja Ukuu hadi Uzi ambayo iko katika kiwango cha mawe ambayo inatengenezwa na Wananachi wenyewe.
 Moja ya Visima vichache vilivyomo ndani ya Kijiji cha N’gambwa ambavyo vina upungufu mkubwa wa maji kiasi kinachochangia kuleta usumbufu wa huduma hiyo ndani ya Kijiji hicho.
 Mzee Khatib Mussa wa Kijiji cha N’gambwa akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  juu ya kadhia ya  muda mrefu  inayowasumbua ya ukosefu wa huduma za Maji safi na salama kijijini pao
 Katibu wa Kikindi cha Ushirika cha Hapa Kazi chenye wanachama 48 katika Kijiji cha Uzi ambae ni Mlemavu Bibi Mwanajuma Harufu Haji akimnon’oneza Kitu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kuzungumza na wananachi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika Picha ya Pamoja na wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Uzi mara baada ya kuzungumza na wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa. Kulia ya Balozi mwenye kilemba ni Mbunge wa Jimbo la Koani Mh. Amina Andrew na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Nd. Ramadhan Abdulla Ali. 
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

No comments: