Mhe. Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa mkutano wa pembezoni uliokuwa umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Sayani ICSU), Balozi Manongi alikuwa kati ya wanajopo wanne walioongoza majadiliano hayo.Wengine kutoka kushoto ni Bi. Vibeke Jense ambaye ni Mkurugenzi wa UNESCO Ofisi ya New York, katikati ni mwedesha majadiliano na kulia kwa Balozi Manongi ni Bw. Gisbert Glaser Mshauri Mwandamizi kutoka Baraza la Kimataifa la Sayansi ( ICSU).
Bw. Hassan Mshinda, ambaye ni Kamishna kutoka Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia akichangia katika majadiliano hayo.
sehemu ya washiriki wa mkutano huo.
Washiriki wengine wakifuatili kwa makini majadilianyo hayo kuhusu nafasi ya sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu, majadiliano hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa UNESCO na ICSU.
Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akibadilishana mawazo na Bw. Gisbert Gladser ambaye katika majadiliano hayo, alitaka kufahamu Tanzania inatumiaje uzoefu wake na mafanikio yaliyoainishwa katika majadiliano hayo kuzisaidia nchi nyingine za Afrika akilenga katika uhusiano na ushirikiano baina ya nchi za Kusini ( South- South Cooperation ).
Na Mwandishi Maalum
Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesema, kwa kuwa sayansi na teknolojia ni suala mtambuka basi tafiti na uvumbuzi unaofanywa na wanasayansi na wataalamu mbalimbali hauna budi kujielekeza katika kujibu hoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili watu hususani katika kuondokana na umaskini na kujiletea maendeleo endelevu.
Ametoka kauli hiyo siku ya jumatatu wiki hii, wakati aliposhiriki katika majadiliano ya pembezoni ( side event) yaliyokuwa yakijadili kuhusu ‘Sayansi kama tegemeo la baadaye la malengo ya maendeleo endelevu: changamoto na fursa zake zake’.
Balozi Maongi alikuwa kati ya wanajapo wanne katika majadiliano hayo yaliyoandaliwa kwa pamoja baina ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO) na Baraza la Sayansi la Kimataifa ICSU). Wanajopo wengine walikuwa Mkurugenzi wa UNESCO katika Umoja wa Mataifa, Bi Vibek Jensen, Bw. Gisbert Glaser ambaye ni Mshauri Mwandamizi kutoka ICSU, na Bi. Paula Caballero, Mkurugenzi wa masuala ya Uchumi, Jamii na Mazingira katika Wizara ya Mambo ya Nje nchini Colombia.
“ Ninapozungumza na wazee wangu kule kijijini kwangu nilikozaliwa kuhusu athari za uharibifu wa mazingira kwa kukata ovyo miti, swali wanaloniuliza je unatupa mbadala gani . Hii ni sehemu ya changamoto ambazo sayansi kupitia kwa wataalamu wetu wanatakiwa kutoa majibu au kutoa njia mbadala za kuwafanya watu wanaotegemea miti kwa shughuli zao wasiendele kufanya hivyo” akasema Balozi Maongi.
Na kuongeza kwamba Tanzania kama iliyo kwa nchi nyingine zinazoendelea inaamini kwamba sayansi na teknolojia inayonafasi na mchango mkubwa sana katika kusimamia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu kutokana na ukweli kwamba suala hilo linagusa kila nyanja ya maendeleo ya binadamu.
Hata hivyo akabainisha kwamba licha ya mataifa mengi yakiwamo yaliyoendelea kukiri umuhimu wa sayansi na teknolojia katika maendeleo, suala hilo halikupewa umuhimu wakati wa utekelezaji wa Malengo ya Maendele ya Millenia ( MDGs) yanayofika ukingoni mwaka 2015.
Na kwa sababu hiyo akasema kwamba Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi 30 ambazo zimeteuliwa kushiriki katika majadiliano ya kiserikali ya kuandaa malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 (SDGs) inatajitahidi kuchagiza suala la sayansi na teknolojia liingizwe katika malengo hayo mapya hasa kipengere cha utekelezaji.
Mkutano huo wa pembezoni umefanyika wakati ambapo wajumbe kutoka mataifa mbalimbali duniani wapo hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ( New York) kuhudhuria awamu ya sita ya majadiliano ya kiserikali , (Intergovenmental negotiations ) kuhuhusu Maandalizi ya Malengo Mapya ya Mendeleo Endelevu ( SDGs) baada ya 2015.
Katika majadiliano hayo Balozi Manongi alielezea uzoefu wa Tanzania katika siyo tu utungaji wa serĂ¡ zinazosimamia masuala ya sayansi ya teknolojia bali hata namna serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje iliyoweza kupanua wigo wa matumizi ya sayansi na teknolojia, uongezaji wa ufadhili katika masomo ya juu katika eneo hilo pamoja na uwezeshaji wa wanawake.
Akataja pia changamoto mbalimbali ambazo Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika inakabiliana nazo, baadhi ya changamoto hizo ni pengo la teknolojia katika ya mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea, tatizo la ubadilishanaji wa maarifa na wimbi la wataalam wa Afrika kukimbili nje kutafuta maisha bora.
Na kwa sababu hiyo akasema, pamoja na jitihada mbalimbali ambazo Tanzania imezifanya na inaendelea kuzifanya katika eneo hilo la sayansi ya teknolojia bado itaendelea kuhitaji misaada na ushirikiano wa karibu hasa katika eneo la uwezeshaji na ubadilishanaji wa maarifa.
Katika awamu hii ya sita ya majadiliano washiriki wanajikita pamoja na masuala mengine kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu za utekelezaji katika eneo la sayansi, teknolojia, ubadilishaji wa maarifa na uwezeshaji na uhusiano wake na malengo mapya ya maendeleo endelevu.
Ujumbe wa Tanzania katika majadiliano unaongozwa na Balozi Tuvako Manongi ukiwahusisha Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestin Mush na Bw. Hassan Mshinda ambaye ni Kamishna kutoka Kamisheni ya Sayansi na Teknlojia ( COSTECH).
No comments:
Post a Comment