Tuesday, December 17, 2013
NILIPOKUNYWA CHAI NA MWANAHARAKATI WA KISWAHILI- ABDILATIF ABDALLA - Na Freddy Macha
Angali kijana wa miaka 19, Abdilatif Abdalla alishiriki “harakati za kisirisiri” kupinga uongozi wa Rais Jomo Kenyatta, Kenya. Uongozi huo anaeleza leo, ulimnyima uhuru raia wa kawaida nchini humo (baada ya miaka mitatu tu ya utawala) uliopatikana Desemba 1963. Abdilatif alikuwa mwanachama wa chama cha upinzani, Kenya Peoples Union (KPU) kilichoongozwa na Jaramogi Oginga Odinga. Mchango wake mkuu ulikuwa kuandika. Alipofikisha makala ya saba iliyouliza “Kenya Twendapi?” alifungwa.
[caption id="attachment_2132" align="aligncenter" width="500"]
Jalada la kitabu maarufu cha mwandishi Abdilatif Abdalla[/caption] Akiwa jela mwaka 1969 hadi 1972, kijana huyu wa Mombasa alifanya urafiki na askari gereza. Askari alimletea penseli, aliyoiandikia hisia zake katika karatasi shashi ya kuchambia maana madaftari hayakupatikana jela. Mwaka 1973, maandishi yalitolewa diwani ya “Sauti ya Dhiki” na Oxford University Press. Diwani ilishinda tuzo la Jomo Kenyatta Prize, 1974 (aliyemfunga!). Hadi leo miaka 40 baadaye uzito wa tenzi hizi haujasinyaa, lugha ya thamani na madoido, maudhui kabambe : fasihi bab kubwa ya Kiswahili. Tazama busara iliyoko ndani ya shairi “Jana, leo na Kesho”, ubeti 27: “Leo ina tafauti, si sawa sawa na jana Leo ndiyo ithibati, ya kuijuwa bayana Ndiyo roho ya hayati, mfano wake haina Leo itungeni sana.” Tafakari. Kiswahili chake kina lahaja tofauti na tulichokizoea Tanzania; hiki ni Kimvita. Neno "itungeni" hapo ubetini, maana yake si kutunga. Huu ndiyo utajiri wa Kiswahili. Akiwa mfungwa wa kwanza wa Kiswahili, ilibidi Abdilatif Abdalla ahamie Tanzania, 1972. Aliajiriwa na kituo cha Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) hadi 1979. Mshairi Abdilatif Abdalla (kulia) alipotembelewa na mhakiki na mtafiti wa historia, Mohammed Said, nyumbani kwake, Ujerumani, mwaka 2011. Picha ihsani ya M Said. “Sauti ya Dhiki” kilivuma sana na mtunzi alifahamika, aghalabu. Miaka ya Sabini ilikuwa kawaida kumsikia Bwana Abdilatif, Radio Tanzania akishiriki majopo mbalimbali ya kukikuuza Kiswahili, yakiwepo maendeleo ya kamusi ya kwanza iliyoanza kuandaliwa na TUKI, 1997. Baadaye idhaa ya Kiswahili BBC- London ilimwajiri 1979 hadi 1986. Akiwa London aliendelea na harakati za maendeleo Kenya pamoja na wazalendo wenzake wengine maarufu mfano mwandishi nguli Ngugi wa Thiong’o na Yusuf Hassan. Alishiriki harakati za “Mwakenya” zilizopinga siasa za Rais Arap Moi. Kuna wakati utawala huu ulimtuma Waziri Elijah Mwangale, aishawishi serikali ya Uingereza iwafukuze lakini wakajibiwa Abdilatif na wenzake hawakuvunja sheria. Abdilatif Abdalla aliishi London ambapo kwa miaka kumi alifundisha Kiswahili chuo cha London mpaka 1994. Toka 1995 kufikia mwezi Mei mwaka 2013- alipostahafu –aliendeleza ualimu huu wa Kiswahili chuo kikuu cha Leipzig, Ujerumani. Sasa hivi ni babu mwenye wajukuu kumi na wawili!
Mtaa wa Camden Town- tulipokutana... Mwezi Septemba 2013 alipitia hapa London kwa safari fupi. Nilikuwa sijamwona miaka mingi. Maishani nimekumbana na watu tosha mashuhuri. Wasilolikosa wote ni mseto wa ucheshi, uchangamfu, akili iliyopevuka na maneno ya hekima. Kimombo hukumbuha neno “charisma”....Hukumbusha methali ya Kiswahili isemayo, Akili Ni Mali. Nimekutana na wanamuziki James Brown (Marekani), Miriam Makeba (Afrika Kusini), Fela Kuti (Nigeria), Remmy Ongala, Fadhil William (mtunzi wa "Malaika"), Francis Bebey (Cameroon), Wabrazili wakongwe Gilberto Gil na Caetano Veloso na mtunzi wa mashairi na jazz (aliyefariki 2011) Gill Scott Heron- niliyemhoji mara mbili. Nimesalimiana na kusogoa kifupi na Mwalimu Nyerere, Rais Robert Mugabe (Dar es Salaam, 1978) na Rais Jakaya Kikwete. Vile vile nimekutana na kuwahoji washairi maarufu wa Kijamaika, Mutabaruka na Linton Kwesi Johnson; pia Ngugi wa Thiong’o wa Kenya, mtengenezaji sinema wa maisha ya Wamarekani weusi , Spike Lee, mwanariwaya wa Kizanzibari Adam Shafi na sasa Abdilatif Abdalla. Wote wana sifa moja.
Mwandishi nikiwa na gwiji Abdilatif Abdalla, London 2013. Sifa gani? Muda wote nliokuwa naye Abdilatif hakuacha kufanya masihara,utani, kutafuta maana katika jambo hata liwe dogo kiasi gani. Tulipoingia mkahawani kupata chai, aliwasikiliza hata watu asiowajua wanasema nini, huku akijumuika kucheka au kutojitenga. Hiyo tabia ya kuchanganyikana kila nukta na wanadamu wenzake na jamii, nimeiona katika kila mtu mashuhuri niliyempa mkono wa salamu. Mathalan, nlipokuwa na Mwalimu Nyerere mjini Rio De Janeiro mwaka 1991, tuliongea utadhani rafiki wa karibu sana. Kawaida unapogongana na watu wa aina hii hukujia hisia kwamba wao ni wadudu wa sayari nyingine; lakini Mwalimu alikufanya ujisikie mtulivu kabisa kwa utani na matani. Hali kadhalika mwimbaji maarufu, marehemu Miriam Makeba (aliyefariki 2008). Nilikutana naye London, mwaka 1987, akiwa na mjukuu wake. Nilivyomsalimia wala hakushtuka. Aliongea kwa upole na tabasamu. Tabia yake ilijaa upole, unyenyekevu na ucheshi wa mwanamke wa kitongoji chochote cha Afrika. Kubali au usipokubali mtazamo wao, watu maarufu- (waliofanya ya maana) huwa na hilo.
Abdilatif Abdalla alikuwa mfungwa wa kwanza wa kisiasa Kenya baada ya Uhuru. Alifahamika kutokana na "Sauti ya Dhiki." Lakini keshaandika vingine yaani Utenzi wa Adam na Hawaa (1971) na karibuni kahariri mkusanyiko wa tenzi -“Kale ya Washairi wa Pemba”, (Mkuki Na Nyota, 2011). Nlimjuza vipi hajatoa vitabu vingi? Akajibu : “Ni vyema kuandika vitabu vichache vikasomwa kuliko vingi visisomwe.” Nilipomuuliza kama yeye ni msanii au mwanasiasa hakusita: “Mimi ni msanii kuliko mwanasiasa. Ubaya wa wanasiasa hawapendi siasa. Mimi napenda siasa lakini si mwanasiasa. Na siasa ni kitu ambacho mtu huwezi kujiepusha nacho. Siasa ni mfumo wa namna ya kuendesha jamii. Kula kwako ni siasa; elimu ni siasa, mahali pa kulala ni siasa; vyote hivyo vinakuja kufuatana na mfumo wa siasa uliopo katika jamii. Ikiwa siasa ya nchi ni mbaya mambo hayo yote yatakuwa mabaya kwa wanajamii. Mimi napenda siasa ; lakini sipendi wanasiasa. Sababu wanasiasa wanatumia siasa kwa maslahi yao binafsi. Ambapo siasa inatakiwa kutumiwa kwa manufaa ya jamii. Wao wanasiasa hawapendi siasa. Wanaitumia tu siasa kwa maslahi yao. Mimi naipenda siasa lakini sitaki kuwa mwanasiasa. Mimi ni msanii zaidi ambaye nazingatia zaidi siasa iliyopo katika jamii.”
Katika utangulizi wa Sauti ya Dhiki mtaalamu wa Kiswahili, marehemu Shihabuddin Chiraghdin aliandika: “Mashairi yake hayana maingilio ya miundo ya kigeni hata chembe. Mawazo yake yote yameambatana na Uswahili na Uafrika...” Abdilatif Abdalla ni sauti tukufu ya Kiswahili. Alipohutubia mhadhara wa chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2012, wengi walishangaa kumsikia akiongea muda mrefu bila kuweka hata neno moja la Kiingereza. Leo wasomi na baadhi ya wanasiasa wamejenga tabia ya kupachika maneno ya Kiingereza katika Kiswahili ili "waonekane wajuaji." Ukweli hiki Kiswanglishi kinakichuja na kukiangusha Kiswahili (na utambuzi wetu wa Kiingereza). Wanaotumia Kiswanglish wanaishia kutoongea Kiswahili au Kiingereza fasaha. Ni vyema sote tukawasikiliza magwiji kama Abdilatif Abdalla aliyemwambia mwana habari Hezekiel Gikambi wa Swahili Hub, Nairobi, karibuni : “Kiswahili kina nafasi kubwa ulimwenguni.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Nashukuru kwa taaluma hii uliyotupa
Post a Comment