Monday, December 23, 2013

MH. REHEMA NCHIMBI AFUNGUA MKUTANO WA UHAMASISHAJI AFYA YA UZAZI NA MTOTO MKOA WA DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi akisisitiza kwa wadau mikakati ya kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano (5) na vifo vitokanavyo na uzazi wakati akifungua mkutano wa uhamasishaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoani Dodoma mapema jana. Kushoto ni kaimu katibu Tawala wa mkoa Dodoma Bw. Felix Mwedipando na kulia ni Mganga Mkuu wa mkoa Dodoma Dr Ezekiel Mpuya.
Baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Dodoma wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa kwenye mkutano wa uhamasishaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoani Dodoma mapema Jana, kutoka Kushoto Mkuu wa wilaya kongwa Alfred Msovela, Mkuu wa wilaya kondoa Omary Kwaangw' Mkuu wa wilaya Bahi Betty Mkwassa na Mkuu wa wilaya Chamwino Fatma Ally.
Wataalam na wadau wa huduma za afya kutoka wilaya za mkoa wa Dodoma wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mkutano wa uhamasishaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Dodoma. Mkutano huo ulifanyika mapema Jana.
Picha ya pamoja baina ya viongozi wa mkoa na wilaya za Dodoma na wadau wa kutoa huduma za afya mkoani Dodoma muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa uhamasishaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi ametaka mikakati iliyowekwa katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoani Dodoma kuhakikisha inatekeleza azma ya kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano (5) kwa asilimia 75 na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa theluthi mbili ifikapo mwaka 2015.

Dr. Nchimbi ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa uhamasishaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto katika mkoa wa Dodoma, mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa wilaya zote za mkoa wa Dodoma, wataalamu wa afya na wadau wanaochangia kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto katika mkoa huo.

Amesema katika kutekeleza azma hiyo changamoto lazima zitajitokeza na ametaka itambulike kuwa baadhi ya changamoto zinafanana sehemu na sehemu na nyingine hazifanani, cha msingi ni kubadilishana uzoefu wa kila wilaya namna inavyokabili changamoto hizo kwa kushirikiana wadau wa Afya.

Dr. Nchimbi ametoa wito kwa jamii na familia kuhakikisha akinamama wajawazito wanajifungulia katika vituo afya, vilevile watoto chini ya mwaka mmoja (1) na wajawazito wanapatiwa huduma za chanjo bila kusahau lishe bora. Aidha wilaya za mkoa wa dodoma zihakikishe zinaweka utaratibu mzuri na rahisi wa rufaa kuanzia ngazi za chini na ziongeze vituo vya afya vinavyotoa huduma za dharura kwa akinamama wajawazito.Wanajifungulia

Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa dodoma Dr. Ezekiel Mpuya Amesema kuwa kwa sasa mkoa umejikita katika kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto na kuimarisha mfumo wa afya ili vituo vitoe huduma zenye viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Amezitaja changamoto kuu zinazokabili utoaji huduma bora za afya kuwa ni idadi isiyokidhi mahitaji ya watumishi wenye sifa ambapo kwa sasa watumishi waliopo ni asilimia 48% ya mahitaji yote, madaktari asilimia 49%, maafisa tabibu asilimia 50% na wauguzi asilimia 41% ya mahitaji.Yote

Changamoto nyingine ni kasi ndogo ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya afya ya msingi (MMAM), kutofanya vizuri kwa mfumo wa rufaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya halmashauri za wilaya kuwataka wajawazito kuchangia mafuta kwa ajili ya rufaa, vilevile kukosekana kwa nyumba/wodi za wajawazito kujingojelezea kujifungua.

Nae meneja wa mradi wa joining hands initiative (JHI )ulio chini ya shirika la Aghakani Dr. Anitha Murube amesema kuwa mradi wa JHI 2012 - 2015 umejikita katika kusaidia afya ya uzazi na mtoto na unafanya kazi katika mikoa mitano mwanza, Dodoma, Morogoro,Iringa, na mbeya na kuwa unafadhiliwa na idara ya mambo ya nje na maendeleo ya biashara ya serikali ya Canada DFAATD.

Amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia sera ya ushirikiano baina ya sekta ya umeme na binafsi (PPP) na pia unalenga kuboresha usawa wa huduma za afya katika vituo vya umma, kujengea uwezo wa utoaji huduma na mfumo wa rufaa halikadhalika kusaidia kuinua ufahamu wa jamii katika kuwa wadau wa kusaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto. (PICHA NA HABARI NA JEREMIA MWAKYOMA OFISI YA MKUU WA MKOA DODOMA)

No comments: