I: UTANGULIZI
a)
Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye
wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma kwa
takriban siku 15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano
wa 14 wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi leo.
Mheshimiwa
Spika,
2.
Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa
kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na
Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu. Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt.
Asha Rose Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa
kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya Bunge lako
Tukufu.
Mheshimiwa
Spika,
3.
Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya
Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia fursa
hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika Mkutano huu,
Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu kuungana
na Nchi ya Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi wa
rangi, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela
kilichotokea tarehe 5 Desemba 2013. Wote
tunakubaliana kwamba huu ni msiba Mkubwa kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu
Mzee Mandela na historia yake.
4.
Aidha, nitumie fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania wote katika msiba huu mkubwa wa
Afrika na Dunia nzima. Hotuba ya
Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15
Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia nzima katika
ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika Karne ya
20. Ninaamini kwamba hiyo ni Historia
ambayo haitafutika vizazi vingi vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa
kuiga na kufuata nyayo zake.
b)
Maswali
Mheshimiwa
Spika,
5.
Katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170 na ya nyongeza 458 ambayo yote yalijibiwa na Serikali. Aidha, maswali 17 ya msingi na 15 ya
nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa
Mawaziri kutoa majibu ya maswali hayo kwa umahiri mkubwa.
Mheshimiwa
Spika,
6.
Pamoja
na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Bunge
lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];
Pili: Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za
Sekta Mtambuka.
Tatu: Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge
zinazosimamia Fedha za Umma; na
Nne: Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.
7.
Aidha, Bunge lako Tukufu
lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The
Excise (Management and Tariff) (Amendment)
Bill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria
ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa kwa mara ya kwanza.
8.
Nitumie nafasi hii kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa
uwazi mkubwa na kwa kina. Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge
umepokelewa na Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.
II: KILIMO
a)
Hali ya
chakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
9.
Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa
13, hali ya upatikanaji wa Chakula
Nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia
mavuno mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo mbalimbali hapa
Nchini. Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2013
katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla
ya Watu 828,063 wanakabiliwa na
upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi
Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga
jumla ya Tani 16,119 za chakula cha
mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe
16 Disemba 2013, jumla ya Tani 13,716
zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika. Tani
2,402 zilikuwa hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na Manyoni.
10.
Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za
Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho kufanya hivyo kabla ya tarehe 15
Januari 2014. Ambao hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria.
Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia
upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo
la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.
b)
Mwenendo
wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa
Spika,
11.
Kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha
mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni
kimeanza kupungua. Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi
na mchele katika soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa.
Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba,
2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 1,188.60 kwa kilo mwezi
Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10
kwa kilo mwezi Novemba, 2013.
12.
Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi
ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na
zile za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye
mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha
kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei
ya vyakula katika miji yetu. Halmashauri zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela
wa chakula kutoka mashambani na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la
kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.
c)
Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa
Spika,
13.
Serikali kupitia Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi
kufikia tarehe 11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499 za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa
kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala ya Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani 233,808 za nafaka. Kati
ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi
na Tani 493 ni za Mtama.
14.
Wakati huo huo, Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha chakula kutoka katika
maghala yake yaliyoko katika Mikoa iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala
yaliyoko kwenye Mikoa yenye upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya
chakula cha msaada kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe
9 Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129
za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara
kununua chakula katika Mikoa yenye ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa
yenye upungufu wa chakula.
d)
Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo
Mheshimiwa
Spika,
15.
Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa
Bunge, Serikali ilichapisha jumla ya vocha
2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa msimu wa Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia
zilikuwa zimekwishafikishwa katika Mikoa husika kulingana na aina
ya mazao yanayohitaji
mbolea hizo. Aidha, Maghala ya Wakala wa Mbolea
Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha ya mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito
kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa vocha zote zinatolewa kwa walengwa kwa
wakati sambamba na aina ya pembejeo inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia
utaratibu uliowekwa.
e)
Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.
Mheshimiwa
Spika,
16.
Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga
jumla ya Shilingi Bilioni 109.6 kwa
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kununua Tani 250,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 19
Desemba, 2013 NFRA ilikuwa imenunua jumla ya
Tani 218,499 zenye thamani
ya Shilingi
Bilioni 109.25 na kwa ajili hiyo.
Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri ya wastani wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na matokeo
mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na liliwavuta Wananchi
wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi sasa Serikali
imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa
ajili ya zoezi hilo na imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa
NFRA wamelipwa fedha zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala
kukusanya nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema katika Mkutano wa
13 wa Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka Mikoa ya Arusha, Dodoma,
Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala
wote wanaoidai Serikali kuendelea kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na
utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi cha deni lao lipo ndani ya bajeti
iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
III: MPANGO
WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA
Mheshimiwa
Spika,
17.
Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua
Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion Framework). Uzinduzi wa Mpango huu
ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa Máxima Zorreguieta Cerruti ambaye
pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Mpango wa
Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa
Spika,
18.
Lengo la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa
huduma za kifedha kwa jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto
zinazoikabili Sekta ya Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa
jamii pana zaidi ya Watanzania kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali
katika kufikisha huduma za kifedha kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na
Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo rasmi wa
kifedha. Teknolojia hizo ni pamoja na:
(a)
Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia
Wakala (Agent Banking);
(b)
Huduma za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali
kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL MONEY na Easy PESA.
(c)
Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of
Sales – POS).
19.
Aidha, Mpango huu utaweka mazingira linganifu
na yaliyo bora kwa kutumia Sayansi na
Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha Sekta ya Fedha
katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango huu pia utawezesha
kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya Lishe na Maendeleo Vijijini
kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika,
20.
Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika
Nchi mbalimbali Barani Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi
wa Taasisi za Kifedha ni Asilimia 24
tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye Mfumo rasmi wa Asasi za
Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo
(SACCOs) ni Asilimia 22. Asilimia 78
ya Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini hasa
Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga kufikia
Asilimia 50 ya Watu wazima
wanaotumia huduma rasmi za kifedha ifikapo mwaka 2016.
Mheshimiwa
Spika,
21.
Kiwango hiki kidogo cha Wananchi walio katika
Mfumo rasmi wa huduma za kifedha unatokana na changamoto zifuatazo:
Moja: Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha
Vijijini ni hafifu hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za
kiusalama;
Mbili: Wananchi wengi wa
Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua umuhimu na faida ya huduma za
kifedha. Aidha, utamaduni wa kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na.
Tatu: Taasisi
nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini ambao ni Wakulima
hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba katika Taasisi hizo na uwezo wao wa
kukopa mikopo ni mdogo, hivyo wakipeleka huduma zao huko hawatapata faida.
Mheshimiwa
Spika,
22.
Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi
za Kifedha kwa Wananchi wengi wa Vijijini hasa Wakulima. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
Moja: Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na
pia kupata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo na shughuli
nyingine za kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;
Mbili: Huduma za Kifedha Vijijini
zinawawezesha Wananchi wengi hasa Wakulima kupata mikopo ya pembejeo na mikopo
ya ununuzi wa mazao;
Tatu: Huduma za Kifedha
Vijijini ni Mkombozi wa Makundi maalum kama vile Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu.
Aidha, zinasaidia Wananchi kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa
mazao ya Kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na
ufugaji nyuki; na
Nne: Kuwepo kwa Huduma za
Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa Chakula, kulinda mazingira na kufanya
Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya kuishi.
Mheshimiwa
Spika,
23.
Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha
Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha Benki nyingi
Nchini. Tayari tunazo Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609 kote Nchini. Lakini pia tunazo huduma za Bima kwa
Makampuni Binafsi zaidi ya 27 na Mawakala wa Bima takriban 600. Ipo Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii ya Umma 5, Masoko ya Mitaji
na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban 5,600.
24.
Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma
za Kifedha kupitia mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia
Wakala (POINTS OF SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo Waajiriwa wa moja kwa
Moja (Direct Employment) wanakadiriwa
kufika takriban 100,000.
Mheshimiwa
Spika,
25.
Maisha bora kwa kila
Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia na kurahisisha maisha. Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake
zinawezesha malipo kwenye biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye Supermarket
na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa njia ya TIGOPESA,
AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za shule na Vyuo, Tiketi za
ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya
Makampuni haya yameunganisha huduma zao na Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered, Amana
Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za jumuishi za
kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki kwenda M- PESA,
TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala.
Kwa sasa Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga Ofisi
kufuata mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya
hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi unaongezaka.
Mheshimiwa
Spika,
26.
Ni kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya
kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini. Lakini ni ukweli kuwa Uzinduzi wa Mpango wa
Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una
manufaa makubwa na mengi ikiwemo kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na
Kuondoa Umaskini kwa kupeleka maendeleo
Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya Milenia. Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango
huu utatuwezesha kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi. Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha na
Vituo vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa
kutumia Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma za Kifedha Vijijini ambako
ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
IV: NISHATI NA MADINI
a)
Mradi wa
Gesi
Mheshimiwa Spika,
27.
Kama ambavyo Wananchi wengi wanafahamu,
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea
kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi Asilia katika
maeneo ya Madimba,
Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa. Pia ujenzi wa Bomba la kusafirishia Gesi
hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mradi
huu utakapokamilika utaunganisha maeneo yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi
Bay-Mtwara, Songo Songo, Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi
katika eneo la bahari ya kina kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi
Asilia mbali na matumizi mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa
sasa Asilimia kubwa unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa
kutoka Nchi za nje na hivyo kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za
kigeni.
Mheshimiwa
Spika,
28.
Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi
zifuatazo zimekamilika hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2013:
Moja: Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita
(6) ya Mabomba ya Mradi yapatayo 4,444
ya umbali wa Kilomita 51.169 katika
Bandari ya Mtwara. Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935 ya umbali wa kilomita 295.5;
Pili: Kusafisha
Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5
zimekamilika;
Tatu: Usafirishaji
wa mabomba kutoka kwenye yadi za kuhifadhia na kuyasambaza kwenye Mkuza tayari
kwa kuyaunganisha kwa kuchomelea. Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9 yamekwishasafirishwa;
Nne: Uchimbaji
wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0 umekamilika;
Tano: Uwekaji wa
mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita 21.1;
Sita: Kufukia
bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano. Tayari
Kilomita 7.30 za Bomba pamoja
na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na
Saba: Utafiti wa
njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika.
Hayo ni maeneo machache ambayo
nimeona niyataje.
Mheshimiwa
Spika,
29.
Ni kweli kwamba kazi za mradi huu ni kubwa
lakini kwa ujumla zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo za
mradi huu ambazo tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa
Mradi ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa
Gesi na Mafuta. Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na
Bomba la Gesi ni za kitaalamu sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC)
ni kuajiri wafanyakazi Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na kujifunza
kwa vitendo shughuli zote zinazohusiana
na ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi
hatua kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi. Utaratibu huu utasaidia
kupata wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha (operations) na kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi
kwa kipindi chote cha matumizi.
Mheshimiwa
Spika,
30.
Vilevile moja ya makubaliano katika Mkataba
wa utekelezaji wa Mradi huu, Mkandarasi anawajibika kuwapeleka Wafanyakazi
kwenye mitambo na mabomba yanayofanya kazi
kwa sasa kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja ili wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia
shughuli zote za kuendesha mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi.
Malengo ya TPDC ni kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti
wakati wa kipindi cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi
Wafanyakazi wote wawe wamekwishapata uzoefu wa kutosha.
Mheshimiwa
Spika,
31.
Kampuni nyingi zilizopo Mtwara
zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda
vinavyohusiana na matumizi ya Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa.
Kwa mfano, Mpango wa kujenga mitambo ya kutengeneza Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya British Gas Tanzania
utakuwa na utengenezaji
wa ajira nyingi za kiwango kuanzia Kada
ya Chini na Kada ya Kati ambayo itasomesha
Watanzania kupitia VETA katika fani mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika
fani ya Vyuma, wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na
umeme.
32.
Katika Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi Tanzania
wanatarajiwa kusomesha wataalamu 16,756
waliofaulu vizuri masomo ya Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu,
kumekuwapo ajira mpya 400, na
Watanzania wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa
na Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo
Nchini. Asilimia 30 iliyobaki ya watoa huduma inatolewa na Wageni.
33.
Katika Kada za Juu, Kampuni
itasomesha na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika
kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa
VETA 370 wamesomeshwa kuhusu Gesi na
Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi 12 wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na
Mafuta ndani na nje ya Nchi.
Mheshimiwa
Spika,
34.
Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba
Kampuni ya British Gas Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa na kuendesha mradi wa
uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri kwamba ajira zitapatikana kwa maelfu
ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi, mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika
uzalishaji (operations) ajira
nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika mnyororo wa
usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii kuwapa Watanzania
matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana, kuanzia
upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee
kuwaelimisha Wananchi wetu kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu. Ni fursa ya kipekee ambayo Wananchi wetu
wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.
V: MATUMIZI
YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)
Mheshimiwa
Spika,
35.
Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali
ililiarifu Bunge lako Tukufu kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato
ya Ndani. Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine
za Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic
Fiscal Devices- EFDs). Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta
moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali
kupata mapato stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa
kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye
Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.
Mheshimiwa
Spika,
36.
Katika utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka
huu, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000
ili waweze kutumia Mashine za Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni
Wafanyabiashara wenye biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika zoezi hili, Wafanyabiashara Wadogo
wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa
barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata kidogo.
Mheshimiwa
Spika,
37.
Katika utekelezaji wa zoezi hili kumejitokeza
malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa Mikoa ya
Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi
ya Mashine hizi. Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa
ya ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea
Risiti; Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa wa
kutumia Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.
Mheshimiwa
Spika,
38.
Kwa kuzingatia maendeleo ya Sayansi na
Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine
za Kielektroniki zinafanya kazi zifuatazo:
Moja: Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi
kwa urahisi na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha au kununua
vitabu vingi vya kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta
usumbufu;
Pili: Zina uwezo mkubwa wa kutunza
kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;
Tatu: Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi
taarifa za mauzo yake kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati
wowote kwa kipindi kisichopungua miaka mitano;
Nne: Humwezesha Mfanyabiashara kutuma
taarifa zake za mauzo moja kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya
Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;
Tano: Mashine zinaweza
kupokea maelekezo moja kwa moja
kutoka kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara
taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;
Sita: Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile Money”. Utaratibu huu
unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na huduma nyingine moja
kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu, n.k;
Nane: Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na
Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;
Tisa: Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya
Mapato Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza
Kodi halali.
Mheshimiwa
Spika,
39.
Msingi wa bei ya kununulia Mashine hizi za
Kielektroniki umezingatia pamoja na mambo mengine, manufaa na faida nyingi
nilizozitaja kwa mtumiaji na ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu wa
utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali Duniani
unaonesha kuwa mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu
zinauzwa na wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi 778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa
na bei za Mashine za Kielektroniki za Nchi nyingine zinazotumia mfumo
unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa bei kubwa za kati ya Dola za
Kimarekani 360 hadi 870. Pamoja na bei hizo, Mamlaka ya
Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na Wasambazaji wa Mashine hizo ili kuona
uwezekano wa kushusha bei hizo.
Mheshimiwa
Spika,
40.
Kuhusu bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi
unaonesha kuwa karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/=
kuzingatia ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina uwezo
wa kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200
hadi 1,000 kulingana na urefu wa “Paper Roll”! au Bunda. Bei ya Karatasi
hizi zinazojulikana kama “Thermal Paper”
umezingatia kwamba ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri
ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.
Mheshimiwa
Spika,
41.
Kuhusu utaratibu uliotumika kuwapata
Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa
karatasi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa
ushindani wa Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.
Mheshimiwa Spika,
42.
Katika kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji,
kwenye Awamu ya Kwanza Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6)
walipatikana kwa kutumia Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International Competitive Tendering) kama ilivyoainishwa kwenye
Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi
Desemba Mwaka 2009 mpaka Mei 2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila
Mtengenezaji na Msambazaji aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
chini ya “Memorandum of Understanding
(MOU).
43.
Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji wa
utaratibu huohuo wa Zabuni ya
Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African, Tovuti ya
TRA na Tovuti ya PPRA. Jumla ya Wazabuni
Kumi na Nne (14) walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa
Nne asubuhi tarehe 27 Septemba 2012.
Watengenezaji wa Mashine Wanne (4) walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14)
waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano (5) walipatikana kati ya Tisa
waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi, huo ndio utaratibu uliotumika
ambao ulikuwa wa wazi na ushindani.
Mheshimiwa
Spika,
44.
Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za
Kielektroniki, Watengenezaji wametoa “Guarantee”
ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika bila kukusudia na watawajibika
kutoa mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi ya mashine hizo.
Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya Wasambazaji na TRA,
Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila
zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengenezaji wao
wenyewe. Napenda kuwahakikishia
Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za
Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia
Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha
kulipa kodi stahiki Serikalini.
Mheshimiwa
Spika,
45.
Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizi katika
kuongeza Mapato ya Ndani; na ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya
Wafanyabiashara yaliyojitokeza, Serikali
imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine za Kielektroniki hadi tarehe
31 Desemba, 2013. Lengo ni
kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa kununua mashine hizi na
kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau
mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi endelevu na
faida za Mashine za Kielektroniki kwa Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na
huduma. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote
kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu
manufaa ya Mfumo huu wa Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane
kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.
VI: USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
46.
Tarehe 16 - 25 Oktoba
2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini China kufuatia mwaliko
wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Keqiang. Katika ziara
hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa
Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Asasi za Sekta Binafsi
Tanzania na Watendaji Wakuu wa Serikali
na Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa
upande wa Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa
Spika,
47.
Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu;
kukuza mashirikiano ya kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na
vyombo vya fedha ili kupata mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili
marafiki, kuona Sekta Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa
China na mwisho kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea
kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa
Spika,
48.
Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa
China ni miongoni mwa Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga
hatua kubwa sana katika maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa
yanayotokea katika Taifa la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili
kushirikiana na Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za
kiuchumi, utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni
pamoja na soko kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.
Mheshimiwa
Spika,
49.
Katika ziara hiyo nilipata fursa ya
kutembelea Miji ya Beijing, Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata
nafasi ya kukutana na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na
Mikutano hiyo, baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa
ajili ya kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili
kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.
Mheshimiwa
Spika,
50.
Kwa ujumla ziara hii
ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja na kuendeleza na kudumisha
ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi waasisi wa Nchi hizi mbili yaani
Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya
Watu wa China, kwenye ziara hiyo, niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa
China Bwana Li Keqiang, pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini
tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.
Mheshimiwa
Spika,
51.
Ziara yangu pia
ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya ushirikiano wa Tanzania na China
katika eneo la Sayansi na Teknolojia na katika Utalii. Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu
uuzaji wa bidhaa za baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa
Kisasa wa Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha,
Mikataba ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya
Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya Umeme -
TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo - NDC na Shirika la Taifa la Nyumba -
NHC ilisainiwa.
Mheshimiwa
Spika,
52.
Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni pamoja na
kuyashawishi Makampuni makubwa ya usafiri wa anga na Mawakala wa safari za
kitalii kuwekeza Tanzania. Katika
jitihada hizo nilikutana na Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na China Travel Service (Holdings) Hong
Kong Limited.
53.
Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa
kwa kiasi kikubwa Makampuni haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha
utayari wao wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na
China. Aidha,
Kampuni ya China Travel Service
(Holdings) Hong Kong Limited
ambayo inafanya biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani
wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za
Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings
International Limited ambayo imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na
Mji wa Shenzhen katika Jimbo la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia
ubia na Serikali yetu katika ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na
Mji wa Bagamoyo unaotarajiwa kuwa “Trade
Hub” ya Afrika.
Mheshimiwa
Spika,
54.
Tanzania imedhamiria kuendeleza uchumi wake
kwa lengo la kufikisha Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati kabla au ifikapo
mwaka 2025. Viashiria vyote vinaonesha
hivyo, na ndio sababu Makampuni yote niliyozungumza nayo wakati wa ziara hiyo
yameonesha shauku kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania katika Sekta mbalimbali na
mengine tayari yapo Nchini kutekeleza miradi mbalimbali. Napenda kuliahidi
Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kwa
upande wake tutajitahidi kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo
tunayotarajia. Aidha, tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na
uwekezaji ili kuweza kuvutia Mitaji na Wawekezaji wengi zaidi pamoja na Watalii
kutoka China na maeneo mengine duniani.
VII: JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika,
55.
Mtakumbuka tarehe 7 Novemba, 2013 Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihutubia Bunge
ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la Jumuiya ya Afrika
Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda kulijulisha
Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano
Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe
30 Novemba, 2013 Kampala Nchini Uganda, Wakuu wa Nchi hizo akiwemo Rais wetu Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete walikutana na waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki
ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki. Aidha, Viongozi hao walizitaka Nchi
Wanachama kukamilisha taratibu za kuridhia Itifaki
hiyo ifikapo mwezi Julai, 2014.
Mheshimiwa Spika,
56.
Manufaa
ya Umoja wa Fedha ni pamoja na: kupunguza gharama ya kufanya biashara katika
Nchi Wanachama; kuwezesha Nchi Wanachama kuwa na kiwango kidogo na tulivu cha
Mfumuko wa Bei; kuwa na viwango vidogo vya riba ya kukopa; na kuepusha athari
za ubadilishaji wa fedha ndani ya Jumuiya kwa kuwa na Sarafu Moja. Matarajio ni
kujenga ukanda tulivu wa kifedha (Monetary
and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na kusaidia ukuaji wa
biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.
Mheshimiwa Spika,
57.
Katika Mkutano huo wa Kampala Wakuu wa Nchi pia waliridhia
Mfumo wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kuagiza kuwa ifikapo mwezi Januari 2014, Nchi Wanachama ziwe zimeanza
utekelezaji wake na kuukamilisha ifikapo au kabla ya mwezi Juni 2014. Aidha,
Wakuu wa Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo ya Mpango Kazi wa kuelekea
kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Walitumia muda wa Mkutano
huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na
waliona kuna umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.
Mheshimiwa
Spika,
58.
Kwa ujumla Mkutano huo
ulikuwa na mafanikio sana hasa katika kuimarisha Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu
wa Nchi wote kwa pamoja walitumia muda huo kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha
kwamba mahusiano yetu kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanadumu na
tunaendelea kuijenga Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu zetu zote.
X: PROGRAMU YA KUBORESHA MIJI NCHINI (URBAN LOCAL GOVERNMENT STRENGTHENING
PROGRAMME-ULGSP)
Mheshimiwa
Spika,
59.
Wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge, nilieleza kuhusu Programu
ya Kuboresha Miji Nchini (Urban Local
Government Strengthening Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. Huu ni mwendelezo wa Programu
ya Uendelezaji na Uboreshaji Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities Programme-TSCP);
ambao kwa sasa unakaribia kumalizika utekelezaji wake. Programu hii ya ULGSP kwa sasa inahusisha
Manispaa 11 na Miji 7. Manispaa hizo ni Tabora,
Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga, Musoma, Songea, Singida, Iringa, Bukoba
na Moshi. Miji mingine inayohusika
ni Kibaha, Geita, Babati, Korogwe,
Mpanda, Njombe na Bariadi.
Halmashauri hizi zinazojumuisha Manispaa na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, ambavyo ni
pamoja na:
i.
Kuongeza Bajeti ya
mapato kila mwaka;
ii.
Kutokuwa na Hati Chafu
za Hesabu za Halmashauri,
iii.
Kuunda Kamati za
kushughulikia matatizo yanayotokana na Programu kwenye ngazi ya Halmashauri,
ngazi ya Kata na Mitaa;
iv.
Kuhakikisha Programu
hiyo imetangazwa na kueleweka na wakazi wa Halmashauri za Manispaa na Miji;
v.
Kuhakikisha kuna Wakuu
wa Idara wa kutosha;
vi.
Kuhakikisha Sheria za Manunuzi zinafuatwa;
vii.
Kuhakikisha Watu watakaohamishwa na Programu
na kulipwa fidia hawazidi nyumba 20;
viii.
Kuhakikisha miradi
iliyotekelezwa inalingana na thamani ya fedha iliyotumika;
ix.
Kutekeleza miradi ya
miundombinu iliyoko kwenye menu;
x.
Kupeleka taarifa za kila
robo mwaka za miradi kwa muda unaotakiwa;
xi.
Kuhakikisha kuna Master Plan ya Mji;
xii.
Kuhakikisha ukusanyaji
wa kodi ya majengo unaongezeka kati ya Asilimia 5 hadi 30; na
xiii.
Kuhakikisha taarifa za
Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye vikao vya Halmashauri kila robo mwaka.
Ukikosa hapa
fedha hizo hazipatikani.
Mheshimiwa Spika,
60.
Nimetaja baadhi ya Vigezo
kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila Sekta ya Halmashauri. Upimaji wa
vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa
mwaka; na Halmashauri zitakazoshindwa kufikia Alama (Marks) 60 na kuendelea,
watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na Mabaraza ya Madiwani lazima
yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu. Aidha,
TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria wale wote watakaozembea katika kutimiza
vigezo hivi na kuathiri maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa
Spika,
61.
Programu hii ambayo ni ya kwanza Afrika
itatumia Dola za Kimarekani 255, fedha
ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai mwaka huu, lakini kutokana na matatizo ya
ubadhirifu yaliyojitokeza kwa Wasimamiaji wa fedha zilichelewa kutolewa. Hata
hivyo, baada ya kuwapeleka wahusika wa ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria,
Wafadhili waliridhika na hatua zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013
Wafadhili walitoa fedha za Awamu ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri
hizo 18. Miradi iliyopo kwenye
Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na mifereji ya mvua,
uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi, upimaji viwanja,
utengenezaji wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka na uboreshaji wa
makazi. Hii ni baadhi ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa na Halmashauri zenyewe
kufuatana na matatizo ya Miji hiyo. Hivyo, ninawaomba TAMISEMI - wasimamie
Programu hii vizuri ili Miradi husika iweze kutatua matatizo ya Wananchi katika
maeneo yao na kuhakikisha Mapato ya Halmashauri yanaongezeka. Lengo ni kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya Miradi hiyo
kukamilika.
XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA
SERIKALI ZA MITAA
Mheshimiwa Spika,
62.
Kama ambavyo
itakumbukwa, wakati wa majadiliano ya Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali
za Mitaa kuhusu Hesabu zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa, kwa mwaka 2011/2012,
Waheshimiwa Wabunge walionesha masikitiko yao
kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na baadhi ya
Halmashauri Nchini. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia mjadala huo
walidai kuwa Serikali imekuwa haichukui hatua dhidi ya Watumishi wanaofanya
makosa katika Halmashauri. Napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba
pamoja na matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali
za Mitaa kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha za Umma, Serikali imejitahidi
kuimarisha usimamizi na utendaji katika eneo hili. Jitihada hizi
zimedhihirishwa na Matokeo ya Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ambayo yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi zinazotolewa
kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000 hadi sasa. Kwa
mfano, mwaka 2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifanywa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha kuwa Halmashauri
zilizopata Hati safi zilikuwa 16 sawa na Asilimia 14 ya Halmashauri zote. Aidha, Idadi ya
Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka
zilikuwa 23, sawa na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati Chafu zilikuwa 75
sawa na Asilimia 65 ya Halmashauri
zote.
Mwaka 2005/2006 Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Safi iliongezeka hadi kufikia 53, sawa na Asilimia 43 na
Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka
zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na Halmashauri zenye Hati Chafu zilikuwa Nne (4), sawa na Asilimia
Tatu (3).
Mwaka 2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi ambapo Halmashauri
zilizopata Hati Safi ziliongezeka
maradufu hadi kufikia 104, sawa na Asilimia 78 na zilizopata Hati zenye
Shaka zilikuwa 29, sawa na Asilimia 21 na hakukuwa na Halmashauri
iliyopata Hati Chafu.
Mheshimiwa
Spika,
63.
Jitihada hizi ni kubwa. Hivyo, Serikali itaendelea
kuimarisha Usimamizi na Udhibiti na Mapato na Matumizi ya Serikali katika Sekta
zote na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi na tija katika
utendaji na kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo ni kuongeza
kasi ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi kwa haraka.
Mheshimiwa Spika,
64.
Pamoja na jitihada hizo za Serikali zinazoonekana, napenda
kuwahakikishia kwamba Watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za Umma
wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo, na kufikishwa mahakamani. Aidha, kesi za Watumishi hao ziko katika Mahakamani
na katika Vyombo vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma
kulingana na makosa yao kuhakikisha kwamba tunajenga nidhamu. Kutokana na hatua
hizo kati ya mwaka 2011/2012 hadi Septemba,
2013 jumla ya
Wakurugenzi 52, Wakuu wa
Idara 65 na Watumishi wengine 749 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri mbalimbali Nchini. Hatua
hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:
i)
Waliofukuzwa kazi ni 232,
ii)
Waliosimamishwa kazi ni 186,
iii)
Waliovuliwa Madaraka ni 33,
iv)
Waliopunguziwa Mshahara ni 1,
v)
Walioshushwa Cheo ni 32,
vi)
Walipewa ONYO ni 113,
vii)
Waliofikishwa Mahakamani ni 233,
viii) Waliofikishwa Polisi na TAKUKURU ni 36.
Serikali itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha fedha za Umma
zinatumika vizuri.
Mheshimiwa Spika,
65.
Pamoja na hatua za
kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi hao mmoja mmoja, Serikali imeendelea
kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana
na tatizo la ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri. Juhudi hizo ni pamoja na kuongeza uwezo kwa
kuajiri Wahasibu wa kutosha katika Halmashauri zetu; kuanzisha Kamati za Mapato
na Matumizi katika ngazi zote za Halmashauri na kutoa mafunzo ya mara kwa mara
kwa Kamati za Mapato na Matumizi za Halmashauri zote. Mbinu nyingine zinazotumika ni kufanya
Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote uliojitokeza. Kwa mfano, Katika
mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika Kaguzi maalumu kwenye Mamlaka za Serikali za
Mitaa kumi na nne (14), ambazo ni Kilindi,
Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro,
Dodoma, Mbarali na Bunda. Kaguzi hizo zimesaidia sana katika kujenga
nidhamu ya Watumishi katika Halmashauri hizo.
Mheshimiwa
Spika,
66.
Serikali pia imeweza kubadili na kuweka Mfumo
wa ‘Lawson’ katika kila Halmashauri ili kumaliza tatizo la Mishahara kwa
Watumishi waliofariki, walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile kuna Mfumo wa
Epicor 9.05 ambao zinasaidia kudhibiti
Bajeti za Mapato na Matumizi katika Halmashauri Nchini. Mafunzo kuhusu matumizi
ya Mifumo hii mipya yanaendelea kutolewa ili kuweza kutumia mifumo hii kwa
ufanisi. Vilevile, Wakuu wa Mikoa walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao vya Baraza
za Halmashauri; katika kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo
hazikupata majibu kikamilifu, Sheria
zifuatwe na wenye kuhusika na ubadhirifu wowote wachukuliwe hatua
zinazostahili. Aidha, Maafisa
Masuuli (Wakurugenzi) wanaohusika na Hoja mbalimbali za Ukaguzi wanapaswa
kuitwa kwenye Halmashauri walizotoka ili kujibu hoja zinazowahusu bila kujali
wamehamishiwa wapi.
XI: HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
67.
Tumekuwa na muda mzuri wa kujadili masuala
muhimu yanayohusu maendeleo ya Nchi yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu
tulichokuwa katika Mkutano huu. Napenda niwashukuru wote waliosaidia
kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na
Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri.
Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza Vikao vya Bunge
lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena
Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu
wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi
zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma
mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa
kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi
mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi
nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi
mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
68.
Niwashukuru Wabunge wote kwa kujadili vizuri
hoja za zilizojitokeza hapa Bungeni. Lakini kipekee niwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri Wanne waliokubali kubeba jukumu ka kuwajibika kwa yote yaliyotokea.
Tunawashukuru kwa uzalendo wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila la kheri
katika maisha yao.
Mheshimiwa
Spika,
69.
Tunahitimisha shughuli za Bunge hili tukiwa
tumebakiza siku chache kabla ya kufika Mwisho wa Mwaka huu 2013. Tunamuomba
Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema atujalie katika siku hizi chache tuweze
kusherehekea Sikukuu njema ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa mwaka na
kuingia Mwaka Mpya 2014 kwa Amani na Furaha!.
Mheshimiwa
Spika,
70.
Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wote tunavyofahamu,
tutakuwa na Bunge la Katiba litakalofanyika mapema mwakani na kwa tarehe
itakavyopangwa. Kutokana na utaratibu
huo ni dhahiri kwamba wengi wetu tutakutana wakati wa Bunge la Katiba. Nitumie fursa hii kuwatakia safari njema
mnaporejea kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu
ya Krismas na Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa
Spika,
71.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako
Tukufu liahirishwe hadi litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na Tano wa
Bunge la Bajeti tarehe 06 Mei, 2014
saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa
Spika,
72.
Naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment