Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini,Mh. Zitto Kabwe akiwahutubiwa wananchi wake leo.
HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013
Leo
nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto
nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za
kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na
uwajibikaji. Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma!
Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama
mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna
mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya
pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa
nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji
mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na
Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa
kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995.
Kabla
ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine
wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya
vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea
mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine
hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu.
Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani
bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na
inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na
nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana,
kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo
ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha
niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya
Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu
yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma.
Nimekuwa
nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa
kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu.
Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na
Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye
tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga.
Mama
Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la
hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili
kwenda la tatu. Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana,
upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji
kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona
kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote.
Jamii
hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa
bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili
katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa
kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya
juu sana.
Nikiwa
nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka
niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia.
Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya
kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha
mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na
miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa
kukosa ajira na kukuza umasikini.
Demokrasia
inahusu maendeleo. Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma
kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa
unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la
Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi
wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha
Usafirishaji Mwandiga.
Asije
mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa
Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila
kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu
kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya
uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima
ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma
katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea
maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa
makuu.
Lakini
tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha
utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka
kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa
Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna
watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini
watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na
sio Kigoma tu.
Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa
sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo
ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali
kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini
ya asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani.
Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya
Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana.
Hii
ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia
ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo
wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri
Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni
taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za
Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa
kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na
ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika
kuimarisha demokrasia yetu. Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini
bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana.
Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi
kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania
kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha
kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa
wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni
uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya
na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli.
Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa
zetu.
Itachukua
muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama
hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa
ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa
badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati
maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba
chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi.
Huu ulikuwa ni uongo. Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata
nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara
nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na
taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki
wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria.
Ni
uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina,
bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika
vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua
majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata
kupelekea mchakato mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu! Lakini hatua
hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano
uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi
ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA.
Lakini
mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na
mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni
uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama
imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na
uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa
mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na
waliojaa woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila
demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima
vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi
nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa
yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu.
Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni
vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule.
Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio
kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na
hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo
sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa
inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya
kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa.
Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. Ninasukuwa
kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina
mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao
hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi;
ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai
asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi
katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu
ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu.
Hebu
sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi
karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani
milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni 2,113,930,000,000
(sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania. Mwaka 2011 kiasi
cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo
trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo
inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi
katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526
(bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000
(trilioni 7.3).
Nimewatajia
hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana.
Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka
10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha
juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza
kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili
kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana
wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya
maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi
zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya
viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia
macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia
ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa
kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!
Lakini
naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa
jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila
sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo
haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo
yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje
ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza
kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake
zinakuwa huru.
Maisha
ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa
sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo.
Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta
matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki
kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero
za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni
siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo.
Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa
zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo
wananchi wa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment