Wednesday, November 20, 2013

WAZIRI MKUU AZINDUA MIRADI YA SH. BILIONI 1.8 ARUMERU

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizindua mradi wa maji wa Moivaro na Mlangirini wilayani Arumeru akiwa katika ziara ya siku moja wilayani humo Novemba 19, 2013. Kushoto ni mkewe Mama Tunu Pinda.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na wazee kabla ya kuzindua mradi wa maji wa Moivaro na Mlangirini wilaya Arumeru akiwa katika ziara ya siku moja wilayani humo Novemba 19, 2013. . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua miradi ya maji na umeme wilayani Arumeru yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 1.8/- ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali  wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now).

Amefanya uzinduzi huo leo mchana (Jumanne, Novemba 19, 2013) katika vijiji vya Chekereni na Manyire wilayani Arumeru, mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa miradi kama hiyo katika mkoa mzima wa Arusha.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chekereni, wilayani Arumeru, Waziri Mkuu alisema katika kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Serikali imedhamiria kuvipatia maji safi vijiji 271 vya mkoa wa Arusha ifikapo mwaka 2014.

“Mwaka 2005, ni vijiji 121 tu kati ya vijiji 342 vya mkoa huu ndiyo vilivyokuwa vikipata maji safi. Mwaka 2012 tulifikisha vijiji 191, na jinsi tunavyokwenda tunataka tufikie vijiji 271 ifikapo mwaka 2014. Kwa hiyo tutakuwa tumebakiwa na vijiji 71, na Mungu akijalia tunataraji kuwa ifikapo mwaka 2015 tuwe tumevikamilisha vijiji vyote,” alisema huku akisangiliwa na mamia ya wakazi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo.

Aliwashukuru wadhamini wa mradi huo wa Chekereni ambao ni kampuni ya Kiliflora kwa kugharimia ujenzi wa mradi huo lakini akawataka wasiishie hapo bali waangalie zaidi namna ya kuwasaidia wananchi wajiongezee fursa zao za kiuchumi.

Kwa upande wa mradi wa umeme, Waziri Mkuu alimtaka mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kuhakikisha kuwa anakamilisha mradi huo katika muda muafaka na kwa kiwango cha juu.

“Hatutaki kusikia visingizio vya sababu za hali ya hewa au sababu za kijiografia... Miradi hii ni ya gharama kubwa kwa hiyo hatutaki visingizio. Meneja wa TANESCO hakikisha hakuna visingizio. Kama kazi hairidhishi, ondoeni huyo mkandarasi, tafuta mwingine,” alisema.

Akisoma risala kuhusu mradi wa maji wa Chekereni, Mhadisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bibi Joyce Bahati alisema mradi huo ambao umegharimu sh. bilioni 1.15/-, utawanufaisha wakazi wapatao 16,197 na kupunguza tatizo la maji katika vijiji vya Mlangarini, Moivaro Olkereian, na maeneo jirani ya Kijenge.

“Mfuko wa Maendeleo wa Wafanyakazi wa shamba la maua Kiliflora (KWDFL) umesaidia fedha na jamii imetoa nguvukazi pamoja na ardhi ya ujenzi wa miundombinu,” alisema.

Alisema mradi huo ambao ulianza kutekelezwa Septemba 2009, umehusiaha ujenzi wa kidaka maji; ujenzi wa matanki mawili yenye mita za ujazo 90 kila moja; ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 15 na utandazaji wa bomba km 21 kutoka kwenye chanzo cha maji chemchem ya Songota.

Mapema akitoa taarifa kuhusu mradi wa umeme vijijini (REA), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. George Simbachawene alisema mradi wa kupeleka umeme vijini katika maeneo ya Manyire kupitia Mlangarini, Seela Sambashamba, Timbolo, Ilkiding’a na Irkisongo wilayani Arumeru umegharimu jumla ya sh. 631,440,000/- .

Aliitaja miradi mingine ya umeme vijijini inayofadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo pia inayotekelezwa na TANESCO kuwa ni:- Mradi wa kupeleka umeme Halmashauri ya Wilaya ya Longido unaogharimu  sh. bilioni 1.45/-; Mradi wa kupeleka umeme Mji wa Loliondo Wilaya ya Ngorongoro ambao gharama yake ni sh. milioni 817/- na Mradi wa kupeleka umeme Vijiji vya Mto wa mbu Wilayani Monduli ambao pia gharama yake ni sh. milioni 342/-.

Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo usiku.

No comments: