Sunday, November 10, 2013

TAMKO rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE (MB) kuhusiana na kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema"

Ndugu Wanahabari,

NILIPOKUWA katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

 “Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema.

Ripoti hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia kwenye akaunti yake binafsi.

Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.

Taarifa hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika nje za nje na pia kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi zetu.

Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.

Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja na uanasiasa wangu.

Hata hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.

Raia huyo wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai kwamba nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.

Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama.

Kutokana na uchafuzi huu wa wazi dhidi ya taswira yangu binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa ya chama au kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.

Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA endapo nitaendelea na jitihada zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania wote pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila na kidini.

Natarajia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii. Nitahakikisha kwamba wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na kuchafuana.

Ni matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”

Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah

Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013

18 comments:

Anonymous said...

Dr. Kimei anaongoza benk yenye asset nyingi za kibenk na amana nyingi za watu na makundi mbali mbali Tanzania. Right away hiyo report inamapungufu huyo aliyemtaja dr. Kimei hajui thamani yake katika tasnia ya mabenki na uchumi kwa ujumla.

Anonymous said...

Pamoja na tamko la bwana Zitto,mimi bado nimeshindwa kumuelewa Mh Zitto na hasa anaposema kwamba alipokea taarifa kwa njia ya barua pepee.Swali linakuja" Je, bwana Zitto uliamini kwamba ripoti hiyo imetoka CHADEMA?.

noelsiay said...

Ni ngumu sana kukanusha taarifa kama Ile kwa maneno mepesi kiasi hicho Zitto be of the serious person kwa ripot Hyo kujibu hvyo

Anonymous said...

Nani ni nani katika hili?!ebu kla upande ujisafishe ili wananchi tuweze kuelewa nn knaendelea!

Anonymous said...

Mh zitto, kukanusha ripoti iliyosheheni data kama zile kwa maneno mepesi ya kisiasa, sidhani kama unatambua huu ni mwaka 2013! Je hizo M-pesa na Tigo pesa zilizotajwa ulituma kweli? Na pesa zilitoka wapi? Be serious!

Anonymous said...

Kwa kweli sikutarajia majibu mepesi namna hii kutoka kwa Mh. Zitto kwa taarifa yenye details kiasi kile. Nilitarajia angezungumzia kuhusu zile akaunti kama ni zake kweli ama la. Pia anataja fedha kiwango cha dola 250,000 pekee wakati katika ile taarifa kuna fedha kiwango hicho mara kadhaa na wala sio mara moja kama Mh. anavyoeleza. Mh. Zitto tulitarajia majibu mazito kwa taarifa nzito!

Anonymous said...

Ni wakati wake wa kuchuma, nafasi nzuri anayo ya kujihusisha na rushwa iliyonona, maneno tu hayamtoi nyoka pangoni.

Anonymous said...

kaka umeniacha njia panda tuhuma inayo kukabili ina details zenye kuthibitika kama vile matumiz ya M-PESA & TIGO PESA .Kwan katika hil wametoa kuanzia tarehe mpaka saa uliyo tuma kiasi tajwa cha pesa , kwa upande wangu bado hoja yako haina mashiko. Lakin nao CDM watoe uthibitisho katika hili maana kwenye blog yao hakuna taarifa hii.

JOSHUA ISRAEL from TEKU said...

Ukitaka wadau tukuelewe vizur anza na mitandao ya voda na tigo watuthibitishie kama namba zako tajwa zilihusika kuwatumia wenzio kiasi tajwa cha pesa au la!.Halafu chadema nao wathibitishe uwepo wa tuhuma hizi na hazipo basi mtoaji taarifa ashughurikiwe ipasavyo la sivyo tumain la wanyonge litakuwa limepotea.

Anonymous said...

Mh. Zitto unasema ipokea ujumbe kea email who was the sender anyway....and why did u mentkon Dr. Kimei only while tbe list included even our dearest Presidaa...we need the truth..here..so struggle for tfuth and not life

Anonymous said...

Kujitetea kwa Mh. Zito hakukuhitaji mzani, kulingana na upande wa ulalamikaji.Hvyo nashangaa kuona watu wakimbeza kwamba amekanusha tuhuma kirahisi rahisi! Basi wamletee mzani utakaopima uzito husika wa maelezo unaolingana na tuhuma.

Anonymous said...

Doooh! kaka ZITO kwa mtazamo wangu hili suala umelichukulia poa sana, kwan umelitolea maneno mepesi ya kipropaganda.Mie nilidhan utayashinikiza makampun ya SIMU yathibitishe kama nikweli pesa tajwa zilitumwa kwa wahusika tajwa kwa muda uliotajwa na kwa namba zilizotajwa kuwa nizako. Mimi nadhan ungefanya hivyo wengiwetu tungejua yakwamba hukuhusika hata kidogo na ndio maana ulikuwa jasiri kushinikiza makampun ya simu husika.

Anonymous said...

Worry not brother... That is the so called political propaganda...ALUTA CONTINUA...

Anonymous said...

Kwani ambacho hujui nini? hutakiwi CHADEMA ni chama cha watu wa Arusha na Moshi HUTAKIWI, zote hizo ni njia tu za kukuondoa na sie wanachadema tunalijua hilo tupo safarini kuondoka kama akina Mwigamba na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara , tuwaachie wenye chama chao, na bado siku si nyingi utayaona mengine lukuki

Anonymous said...

Hakuna ukweli wowote CHADEMA imejaa majungu sana na fitina kuna watu wamejimilikisha chama kwa maslahi yao ukigusa maslahi yao vita inaanza. Mhe. Zito jitoe utaona na wengine wanaondoka wapo wengi.

kato j said...

Ndege mjanja unaswa katika tundu bovu. Zamu yako Zitto now on defensive, bahati mbaya hapo CCM watakaa kando wanachekelea na ole wako u defect,watashangilia after one year,unakuwa Dr Kaburu, Dr.Lamwai, Nyaruba, Msabaha NZANZUKWAGO,SHITAMBALA NK yetu macho

Anonymous said...

Nilikuwa najiuliza HUMMER Zitto kainunuaje wakati hapokei posho? Kama ni salary ya 11m mbona vijana wengi wanapokea ila wanaishia kwenye X-trail tu? Nimeanza kuamini ule waraka! Kama sivyo bro come up again with strong details against the accusation! Sio tu kusema chama cha kikabila kumbe wenyewe mnachemka kweli

Anonymous said...

zito komaa mwanangu hawa watu wa kaskazini wameumbwa na ubinafsi ubaguzi na umangimeza,wanataka wao sikuzote waabudiwe na kujilimbikizia msdaraka ndo maana hata baba wa taifa aliwaogopa kama ukimwi. hawa ni kikuyu wa Tanganyika.Aluta kontinua mwanangu.