Friday, November 29, 2013

MKUU WA MKOA WA MOROGORO AFUNGUA MAFUNZO YA UTAALAMU WA KILIMO CHA MAZAO YA MATUNDA, MBOGA NA MAUA YALIYOWASHIRIKISHA BAADHI YA WAKUU WA WILAYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, Imelda Ishuza ( kulia) akipokea cheti ya kuhitimu matunzo toka kwa RC Moro, Joel Bendera.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ( kulia) akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo Mkuu wa Wilaya ya Makete, Josephine Matiro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ( kushoto) akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigalla.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera (aliyesimama) akitoa hutuba ya kufunga mafunzo ya Utaalamu wa kilimo cha mazao ya matunda, mboga na mauwa , mjini Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Joel Bendera ( wanne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo ya utaalamu wa kilimo cha mazao ya ' Horticulture' mjini Morogoro, wakiwemo pia Wakuu wa Wilaya.

Na John Nditi, Morogoro

TAASISI  Kilele ya Mazao ya Matunda, Mboga na Maua ‘ Horticulture’( TAHA),imewapatia  mafunzo Wakuu wa Wilaya na Wataalamu wa kilimo  wa  Mikoa ya Kanda ya Kati, Mashariki na Nyanda za Juu kusini juu ya  mbinu bora na sahihi za  kuboresha na kuendeleza kilimo cha mazao hayo ili kuongeza uzalishaji , kukuza soko la ndani na nje ili kuinua uchumi wa taifa.

Maneja wa Ufundi wa TAHA, Isack Ndamanyere, alisema hayo  Novemba  21, mwaka huu  mjini hapa , kabla ya kukaribishwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, kufunga mafuzo  ya nadharia na vitendo yaliyochukua muda wa  tatu ambayo  yalindaliwa na Taasisi hiyo na kuwashirikisha washiriki 25.

Wakuu wa wilaya waliopatiwa mafunzo hayo na wilaya zao  katika mabano ni Dk Norman Sigalla King ( Mbeya), Crispin Meela ( Rungwe), Josephine Matiro ( Maketa) na Gerald Guninita ( Kilolo) pia  na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo , Imelda Ishuza.

Mbali na kundi hilo wengine ni wataalamu na maofisa  katika sekta ya Kilimo kutoka  Halmashauri za wilaya za Mkoa wa Dodoma, Njombe, Iringa,Pwani na Morogoro.

Kwa mujibu wa Meneja Ufundi wa TAHA, alisema , lengo la mafunzo hayo ni juhudi za kuendeleza mazao hayo kwa kuwa yanaweza kupatia mkulima mapato ya haraka ya kukuza uchumi wake na wa taifa na ndani ya muda mfupi kutokana na kuwepo kwa soko la uhakika la mazao hayo ndani na nje.

 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Bendera, wakati akifunga mafunzo hayo , ameziomba Halmashauri za wilaya kutenga bajeti kwa ajili ya  kuwagharamia mafunzo  ya vitendo maofisa ugani wa ngazi za vijiji, kata na Wilaya ili nao waisambaze kwa wakulima wa mazao hayo.

Pia aliipongeza Taasisi hiyo kwa uwajibikaji wao wa kuhakikisha tasnia inasonga mbele katika  kuboresha maisha ya wananchi pia kuongeza pato la taifa ambapo ameitaka kuzidi kushirikiana na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo hayo kwa kila Halmashauri nchini.

Mkuu huyo wa Mkoa, aliwapongeza Wakuu wa Wilaya hizo kwa kutenga muda wao na kuhudhuria mafunzo hayo , na kusema huo ni moyo wa kizalendo na utatoa dira ya kusonga mbele katika kuinua hali ya maisha ya wananchi wetu kupitia kauli mbiu ya Kilimo Kwanza.

Naye Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Mbeya , Dk Sigalla,aliisgukuru TAHA kwa kuwashirikisha katika mafunzo hayo na kwamba wao watakuwa watu wa mfano wa kuwa na mashamba ya aina hizo na watatumia fursa hiyo kuwasimamia viongozi wa chini yao.

Hata hivyo alisema  , msingi mkubwa wa kufikia mafaniko na malengo hayo ni  kuendeleza kilimo hicho, ni kwa wakulima kupatiwa elimu na faida ya kilimo cha aina hiyo.

 Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya , wakulima wengi licha ya kuwa na maeneo mazuri yenye rutuba , bado wanashindwa kutofautisha aina ya kilimo , kile cha mazao yanayochuka muda mrefu kukomaa na cha  mazao ya yanakomaa kwa muda mfupi.

No comments: