Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa popote pale duniani.
Waziri Membe akiendelea na mahojiano yake na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten ofisini kwake leo, jijini Dar es Salaam.
Waziri Membe akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mahojiano na mwandishi Fredy Mwanjala (kushoto) na mpiga picha Bi. Fauzia Yusuph (kulia), wote wanatoka Kituo cha Televisheni cha Channel Ten.
Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO
Tanzania itaendelea kushiriki operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa popote pale duniani.
Msimamo huo wa Tanzania uliwekwa wazi na Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika mahojiano maalum na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, yaliyofanyika leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao yaliyolenga kutaka kufahamu msimamo wa Tanzania kufuatia vifo vya askari wake huko Darfur, Sudan na hivi karibuni huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), Waziri Membe alisema moja ya sera ya mambo ya nje katika awamu ya nne na Mhe. Rais Kikwete ni ulinzi na amani.
Hivyo, Tanzania itaendelea kushiriki katika operesheni hizo za kulinda amani ambazo zimeiletea Tanzania heshima kubwa katika medani ya kimataifa.
Waziri Membe alisema inawezekana kuwa wanajeshi wa Tanzania wanalengwa na kundi la waasi la M23, kwa kuwa Tanzania ni mwiba mkali kwa kikundi hicho kutokana na umahiri wake unaofahamika vyema katika nchi za Maziwa Makuu.
“Umwagikaji wa damu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) ni chachu kwa Watanzania dhidi ya kikundi cha waasi cha M23,” alisema Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hivi karibuni mwezi Agosti, kikosi cha M23 kilishambuliwa na kuteketezwa kwa mujibu wa taarifa za kiitelijensia zilizoripotiwa na vyombo vya habari. Lakini inasemekana kuwa kuna kundi lingine limezuka tena hivi karibuni kwa jina hilo hilo la M23 kama vile chem-chem ya maji, alieleza Waziri Membe.
“Ni muhimu ieleweke kuwa Tanzania haitosita kamwe kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupambana na hizi vita za nchi jirani zisizoisha,” alisema Waziri Membe. Aliongeza na kusema kuwa Tanzania imekuwa kinara cha medali za kimataifa katika kutetea na kulinda amani na usalama wa nchi yetu.
“Sisi ni taifa ambalo liko tayari kujitolea kupigana na kumwaga damu katika kutetea amani na kutatua migogoro ya majirani zetu,” alisema Waziri Membe. Alieleza kuwa Tanzania imeshiriki kwa namna moja au nyingine katika vita vya ukombozi wa amani barani Afrika katika nchi za Msumbiji, Afrika Kusini, Zimbabwe, Comoro, Uganda, Mashariki ya Kongo-DRC na nchi nyingine nyingi.
Akizungumzia kupoteza maisha kwa askari wa Tanzania nchini Kongo-DRC, Waziri Membe amesema kuwa ni msiba mkubwa wa kitaifa na wa Umoja wa Mataifa.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea salamu za rambirambi kutoka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Kongo, Serikali ya Angola, Serikali ya Afrika ya Kusini na nchi nyingine duniani.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea salamu za rambirambi kutoka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Kongo, Serikali ya Angola, Serikali ya Afrika ya Kusini na nchi nyingine duniani.
Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazounda Brigedi Maalum ya umoja wa mataifa (MONUSCO) kulinda na kusimamia amani huko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC). Kuna batalioni moja yenye askari zaidi ya 1,270 ambao wanaunda sehemu ya Brigedi hiyo Maalum ya MONUSCO.
No comments:
Post a Comment