Balozi wa China Liu Jieyi ambaye nchi yake ni Rais wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Novemba, akielezea yale yaliyojiri wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama uliofanyika jana alhamisi na kujadili hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia. Tamko la Rais wa Baraza ambalo limeridhiwa na wajumbe wote 15 wanaounda Baraza la Usalama, wametoa wito kwa makundi ya waasi katika DRC kuweka chini silaha zao, makundi hayo ni pamoja na kundi la M23. Mbali ya kuweka silaha chini yametakiwa pia kuvunjika. Vivile Baraza hilo pamoja na kutambua kwamba kundi la waasi la M23 limemwaga damu ya wananchi wengi wa DRC pia limepoteza maisha ya walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni ya MONUSCO na kwa sababu hiyo Baraza limerejea wito wake kwamba litaendelea kuunga mkono walinzi wa amani maarufu kama Blue Helmet katika utekelezaji wa majukumu yao.
Na Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa jana alhamis limetoa wito linaolitaka kundi la wapiganaji la M23 kuvunja kundi hilo mara moja ikiwa ni pamoja na kuweka silaha zao chini.
Aidha Baraza hilo limekaribisha tamko la awali la kundi hilo la M23 kwamba limeamua kumaliza uasi wake na umwagaji damu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika mkutano wake ulIojadili hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Balozi Liu Jieyi wa China ambaye ndiye Rais wa Baraza Kuu la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba na akizungumza kwa niaba ya wajumbe 15 wa Baraza amesema.
“Baraza linatoa wito wa hitimisho na utekelezaji wa makubaliano ya mazungumzo ya Kampala ambayo pamoja na mambo mengine yanatoa fursa ya upokonyaji wa silaha na kuvunjwa kwa kundi la M23 na uwajibikaji kwa wakiukaji wa haki za binadamu.
Mazungumzo hayo ya Kampala maarufu kama ‘Kampala Talks’ yanafanyika chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu, ( ICGLR), Rais Yoweri Kaguta Museven pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Crispus Kiyonga.
Kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa Baraza Kuu la Usalama ( Presidential Statement ) Baraza hilo limeonyesha wasi wasi kuhusu mwendelezo wa tishio la usalama kutoka kundi la Forces Democratique de Liberation du Rwanda ( FDLR).
Kutokana na wasi wasi huo, Baraza Kuu linahimiza umuhimu wa kusambaratishwa kwa kundi hilo pamoja na makundi mengine yenye silaha.
Aidha Baraza Kuu la Usalama , limelaani kwa nguvu zake zote kuhusu kuendelea kwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, unaofanywa na makundi yenye silaha yakiwamo mauaji ya papo kwa papo, unyanyasaji wa kijinsia na matumizi makubwa ya watoto katika vita.
Vile vile Baraza hilo pia limetambua kuwa katika kipindi cha miezi 19 ya uasi wa kundi la M23, kundi hilo limeua walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu katika DRC kupitia Misheni ya Kutuliza Amani maarufu kama MONUSCO inayoongozwa na Bw. Martin Kobler, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika DRC.
Na kwa sababu hiyo Baraza Kuu la Usalama limerejea tena wito wake kwamba litaendelea kuwaunga mkono walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa, maarufu kama Blue Helmet katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kundi la M23 ambalo hivi karibuni lilipata kichapo cha aina yake kutoka MONUSCO linaundwa na wanajeshi ambao waliasi kutoka jeshi la kitaifa la DRC mwezi wa Nne,kundi ambalo pamoja na makundi mengine yenye silaha yamekuwa mara kwa mara yakipambana na majeshi ya serikali (FRDC).
Katika mwaka uliopita mapigano kati ya makundi ya waasi na majeshi ya serikali yalisababishwa zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makazi yao na hivyo kuongeza uzito wa jukumu la kutoa misaada ya kibinadamu katika eneo ambalo tayari zaidi ya watu 2.6 milioni ni wakimbizi wa ndani huku wengine 6.4 milioni wakihitaji msaada wa chakula na huduma za dharura.
Aidha Baraza Kuu linahimiza Umoja wa Mataifa, na washirika wake wengine kuendelea na jitihada zake katika utekelezaji wa Mpango Mpana wa Kisiasa kwaajili ya DRC na Maziwa Makuu uliosainiwa na nchi 11 na wadhamini wanne mapema mwaka huu , mpango unaolenga katika kuleta Amani ya kudumu katika eneo la Maziwa Makuu.
No comments:
Post a Comment