Wednesday, October 2, 2013

WAZIRI MKUU ATAKA SOKO LA KAGUNGA LIKAMILISHWE

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kuhakikisha kuwa anafuatilia suala la mkopo kwa ajili ya ujenzi wa soko la Kagunga hadi alikamilishe.
 
Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Oktoba mosi, 2013) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kagunga mara baada ya kuweka jiwe la msingi la soko la kimataifa la Kagunga ambalo liko umbali wa kilometa 1.5 kutoka mpakani mwa Tanzania na Burundi kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika.
 
Waziri Mkuu alisema kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutatoa fursa za kibiashara baina wakazi wa Kagunga na vijiji jirani pamoja na nchi ya Burundi ambayo milima yake inaonekana kutokea mahali soko lililojengwa. Mji wa karibu na Kagunga ni Nyanza Lac ulioko kwenye jimbo la Makamba, nchini Burundi.
 
“Msingi wa ujenzi wa soko hili ni makubaliano baina ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Benki ya Rasilmali Tanzania (TIB). Mkurugenzi simamia hilo zoezi, lifukue kila mahali ulete kwa Waziri Ghasia ili tukamilishe taratibu za mkopo na soko liweze kukamilika,” alisema.
 
Alisema umuhimu wa soko hilo ni ka pande zote mbili kwani litafungua milango ya biashara baina ya Tanzania na Burundi. “Kukamilika kwa soko hili pamoja na barabara ya Kigoma hadi Kagunga kutasaidia sana kuharakisha upatikanaji wa bidhaa za kuuza nchi jirani ya Burundi,” alisema Waziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu ambaye alilazimika kusafiri kwa boti kwa zaidi ya saa moja kutoka Kigoma mjini hadi Kagunga umbali wa kilometa 49 kwenda tu (sawa na nautical miles 26.5) alisema anatambua umuhimu wa barabara hiyo na kuahidi kufuatilia upatikanaji wa fedha ili iweze kukamilika mapema. Kwa njia ya kawaida, Kagunga iko umbali wa kilometa 130 kutoka Kigoma mjini  na msafiri analazimika kupitia kwanza Burundi ndipo aweze kuingia Kagunga.

Mapema, akisoma risala kuhusu ujenzi wa soko hilo, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Bi. Miriam Mmbaga alisema mradi huo wa soko uliibuliwa na wananchi mwaka 2008 ili wapate soko la kuuzia mazao ya kilimo, mifugo, samaki na dagaa. “Mwaka 2008/2009 zilitengwa sh. milioni 365 na ujenzi ulianza mwaka 2009 ambapo fedha zote zimetumika,” alisema.
 
Kabla ya kuibuliwa kwa mradi huo, eneo hilo lilikuwa likitumika kama gulio kati wajasiriamali wa Tanzania na Burundi.
 
Alisema hadi kukamilika kwake, mradi huo utagharimu sh. bilioni 2.6 na kwamba hivi sasa inahitaji sh. bilioni 2.24 ambapo kati ya hizo sh. bilioni 1,57 zitakuwa ni mkopo kutoka TIB na sh. milioni 668 zitatolewa kwenye bajeti ya maendeleo ya Halmashauri kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Kwa mwaka 2013/ 2014, Halmashauri imetenga kiasi cha sh. milioni 245.9 kwa ajili ya mradi huu,” alisema Mkurugenzi huyo.
 
Katika ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia, Naibu Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge pamoja na Naibu Waziri Nishati na Madini, Bw. George Simbachawene.

No comments: