Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa upigaji kura wa Azimio nambari A/68/L4 linaloitaka Marekani kuiondolea Cuba Vikwazo vya Kiuchumi, Kibiashara na Kifedha. Pembeni ni Naibu Muwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Mwinyi. Nchi 188 kati ya nchi 194 ambazo ni Mwanachama wa Umoja wa Mataifa zilipiga kura ya ndiyo kuunga mkono azimio hilo katika mkutano uliofanyika siku ya Jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa zikiwamo nchi zote za Jumuiya ya Ulaya ilihali Marekani na Israel zilipiga kura ya hapana huku nchi tatu ambazo ni Marshall Island, Micronesia na Palau zilipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.
Na Mwandishi Maalum
Licha ya Jumuiya ya Kimataifa kwa mara nyigine tena kupiga kura ya ndiyo kuunga mkono Azimio namba A/68/L4 linalosisitiza umuhimu wa Marekani kuiondolea Cuba vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha. Marekani kwa upande wake imetetea msimamo wake huo kwa kusema inafanya hivyo kutetea maslahi ya wananchi wa Cuba.
Akizungumza kabla ya azimio hilo kupigiwa kura muwakilishi wa Marekani, Bw Ronald Godard alisema kwamba wakulaumiwa ni serikali ya Cuba na si Marekani kwa kile alichoeleza kwamba watu wa nchi yake wanaurafiki mkubwa na watu wa Cuba na ndiyo maana Marekani imekuwa ikitetea maslahi ya wananchi wa Cuba ya kujiamlia mambo yao na hatima yao.
Akaongeza kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu, mbinyo wa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza pamoja na mifumo na sera mbaya za kiuchumi na uwezekaji ndiyo vinavyorudisha nyuma maendeleo ya Cuba na watu wake na kwamba bila masuala hayo na mengine kurekebishwa itakuwa ndoto kwa wananchi wa Cuba kijiletea maendeleo yao. Na akawataka wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutounga mkono azimio hilo.
Pamoja na rai hiyo ya Marekani ya kutaka jumuiya ya kimataifa isiunge mkono azimio hilo, nchi wanachama 188 walipiga kura ya ndiyo, huku Marekani yenyewe na Israeli zikipiga kura ya hapana wakati Marshall Island, Federated States of Micronesia na Palau zikipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.
Katika upigaji kura hiyo, nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Ulaya ( EU) nazo zilipiga kura ya ndiyo kuunga mkono Azimio hilo licha ya kwamba zilikuwa hazikubaliana na baadhi ya mambo yakiwamo ukiukwaji wa haki za binadamu katika taifa hilo la Cuba.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya mataifa yaliyopiga kura ya ndiyo kuunga mkono azimio hilo ambalo kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita liliwasilishwa mbele ya Baraza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bw. Bruno Rodriquez Parrila.
Akiwasilisha Azimio hilo, Waziri Parrila alianisha athari za kiuchumi, kifedha, kimawasiliano na kudumazwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi ya Cuba na watu wake, adhari ambazo zimetoka na miaka mingi ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani.
Akiungana na wazungumzaji wengi waliotoa wito wa kutaka kuondolewa kwa vikwazo hivyo, Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi alitoa rai kwa mataifa hayo mawili kukaa mezani na kumaliza tofauti zao.
Akasema licha ya vikwanzo hivyo kudumu wa miaka 50 ukweli wa mambo ni kwamba athari zake zimekuwa zaidi kwa wananchi wa sio kuwa na hatia. Akasema Tanzania kama rafiki wa mataifa hayo mawili ilikuwa ikitoa rai kwa pande hizo mbili kukaa meza moja na kumaliza tofauti zao kwa manufaa ya wananchi wa pande hizo mbili.
Wazungumzaji wengi, walieleza kwamba kuendelea kwa vikwazo vya kiuchumi nchini Cuba ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa pamoja na kanuni za msingi ambazo zimeainishwa katika katiba ya Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya wasemaji walieleza kwamba vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea Cuba havikuwa na maana yoyote zaidi ya kuendeleza tofauti zilizojiri wakati wa vita baridi na kwamba Cuba kama taifa huru lilikuwa na haki ya kujiamulia mambo yake yenyewe.
Aidha wasemaji kadhaa waliitaka Marekani ifikie mahali sasa isikilize wito wa mataifa mengi, wito wa kuitaka kuondoa vikwazo hivyo kwa manufaa na ustawi wa wananchi wengi wa cuba.
Wazungumzaji wengine walibainisha kwamba haikuwa haki kwa Marekani kuwachukulia hatua nchi au makampuni ya kimataifa ambayo yanataka au yamethubutu kushirikiana kiuchumi na Cuba na kusisitiza kwamba Marekani inatakiwa kuachana na utaratibu huo.
No comments:
Post a Comment