Monday, October 7, 2013

Kambi ya vijana ya kilimo Mkongo ilete ukombozi - Kikwete

Rais Jakaya Kikwete akimsalimia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja wakati akiwasili kuzindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa Mkongo wilayani Rufiji hivi karibuni. Wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Profesa Lucian Msambichaka na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bw. Yamungu Kayandabila (kwanza kushoto).

Na Mwandishi wetu, Pwani

Rais Jakaya Kikwete amesema kambi ya vijana ya kilimo na Maarifa Mkongo iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani iwe moja ya mifano hai ya kuondoa umaskini na kuwakomboa wananchi kivipato.

Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo alipokuwa akifungua rasmi kambi hyo iliyobuniwa na Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) hivi karibuni wilayani Rufiji.

“Umasikini wa watu wetu utaondoka kupitia jitihada kama hizi zenye dhamira ya kuwakomboa kivipato,” alisema na kuongeza kuwa vijana hao wakitumia ujuzi waliopata kwa vitendo watabadilika kimaisha na watakuwa mfano kwa jamii yote. Alisema kambi hiyo ni nzuri kwa vijana na haina budi kutoa mafunzo ya kilimo ambayo yatawawezesha kwenda kujiajiri na siyo kusubiri ajira ili wakaeneze ujuzi huo katika maeneo wanayotoka.

Kambi ya vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo ni moja ya njia za utekelezaji wa azma ya serikali ya kuleta mapinduzi ya kijani Kupitia mpango wa Kilimo Kwanza.

Kambi hiyo imeanza na vijana 50, kati ya hao wavulana wakiwa 36 na wasichana 14. Rais alisisitiza kwamba vijana hao watakapomaliza mafunzo yao wawezeshwe ili watakaporudi katika vijiji vyao wakatumie ujuzi walioupata kwa vitendo kupata fedha.

“Hawa wakitoka hapa wasiachwe tu, mkiwaacha muda mfupi mtawakuta wanacheza pool…hivyo ufanyike utaratibu maalumu wa kuwawezesha kwa usimamizi maalumu ili mashamba yao yakawe kivutio kwa watu wengine kupenda kilimo,” alisema.

Akitoa mfano alisema mazao nyanya, tikitimaji na matango ya shamba darasa ya kambi hiyo yana soko kubwa, hivyo watakapomaliza mafunzo hayo wakatumie ujuzi huo kulima mazao hayo ili kufanikiwa.

Pia aliitaka RUBADA na Wizara ya Kilimo na Ushirika kuhakikisha wanatafuta aina bora ya mbegu inayozaa mazao mengi ili vijana hao wakafurahie kazi hiyo na kuwavutia wenzao na jamii nzima.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja alisema kambo hiyo pia ni utekelezaji wa mpango wa kukuza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ambao unalenga kuleta mapinduzi ya haraka ya kilimo kikanda unaojumuisha jitihada na nguvu za pamoja za wadau mbalimbali.

RUBADA inatekeleza mpango huu kwa mtindo wa “Hub and Spoke” ambapo mwekezaji mkubwa wa ndani au wa nje anakuwa “Hub” na wakulima wadogo wanakuwa “Spoke” wote kwa pamoja wakisukuma gurudumu la maendeleo.

Akifafanua zaidi alisema mtindo huu unahusu kuanzisha kambi za vijana kwa kila eneo lenye mwekezaji mkubwa katika bonde zima la mto Rufiji linaloanzia mkoa wa Pwani, Morogoro, Iringa, Mbeya, sehemu ya Dodoma, Singida, Ruvuma na Lindi.

Bw. Masanja alisema kufuatana na mkakati sa SAGCOT uliobainisha kongani sita za Rufiji, Kilombero, Ihemi, Mbarali, Ludewa na Sumbawanga; RUBADA, imeandaa mpango kabambe wa utekelezaji ambao utashirikisha vijana katika kila kongani. “Kwa mwaka huu wa fedha, tunategemea kuwa na vituo vitano vya vijana katika kilimo na maarifa na kila kituo kitakuwa na vijana wasiopungua 300 ambao watapata mafunzo katika kipindi cha mwaka mmoja,” alisema.

Vituo hivyo vya vijana vitakuwa na majukumu ya kutoa mafunzo kuhusiana na utekelezaji wa kilimo bora chenye tija; kuongeza thamani mazao; matumizi ya vifaa vya kisasa; utekelezaji wa kilimo bora bila uharibifu wa mazingira; kuandaa andiko la mradi ili kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha na uundaji wa vikundi vya ushirika.

Kwa mujibu wa Bw. Masanja, mafunzo katika kambi hizo yatajikita katika maeneo makuu matatu yakihusisha uzalishaji wa mazo ya kilimo kwa wingi na yenye thamani kubwa hasa mazao ya bustani, mboga mboga na matunda; ufugaji wa kisasa wa ng’ombe na kuku na ufugaji wa samaki pamoja na ujasiriamali.

“RUBADA inatarajia kuzalisha vijana 600 kutoka kituo cha Mkongo hadi 2015 ambao watakuwa na utaalamu na ujuzi wa kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa,” alisema Mkurugenzi huyo.

Kilimo ni moja ya sekta zinazolengwa katika mikakati mbalimbali ya serikali katika mapinduzi ya kiuchumi na kufikia malengo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Kulingana na sense ya watu ya 2012, asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania ni vijana.

No comments: