Friday, September 6, 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA MBILI WA BUNGE, DODOMA TAREHE 06 SEPTEMBA, 2013



I.                      UTANGULIZI:

a)            Maswali
                                                                                        
1.            Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kutekeleza na kukamilisha majukumu yetu katika muda uliopangwa. Katika Mkutano huu Maswali 120 ya Msingi na 305 ya Nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, jumla ya Maswali 12 ya Msingi ya Papo kwa Papo na 11 ya Nyongeza yalijibiwa na Waziri Mkuu.
b)           Miswada

2.            Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu lilijadili na kupitisha Miswada Mitatu (3). Miswada hiyo ni:
i)             Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa Mwaka 2013 [The National Irrigation Bill, 2013];

ii)            Muswada wa Sheria wa Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 [The Cooperative Societies Bill, 2013]; na

iii)           Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013 [The Constitutional Review (Amendment) Bill, 2013].

3.            Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kujadili na kukubali kupitisha Miswada hiyo kwa umahiri mkubwa. Aidha, niwapongeze Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wataalam wote waliohusika na Maandalizi ya Miswada hiyo. Kipekee niwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kupitia Miswada yote na kutoa maoni yao, ambayo sehemu kubwa yamezingatiwa na Serikali katika kuboresha Miswada hiyo.

4.            Mheshimiwa Spika, asubuhi ya leo Bunge lako Tukufu lilipokea Kauli za Mawaziri wa Fedha na Uchukuzi. Wote tunawashukuru kwa maelezo yao.

II.            UTEKELEZAJI WA MFUMO WA MATOKEO MAKUBWA SASA “BIG RESULTS NOW”

5.            Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge uliomalizika mwezi Juni, 2013 Serikali iliahidi kwamba, katika Bajeti ya mwaka 2013/2014 itaanza kutekeleza Mfumo Mpya wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji  wa  Miradi  ya Maendeleo ambao unajulikana kwa dhana mpya ya ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now-BRN). Napenda kuliarifu Bunge   lako  Tukufu  kwamba,   Mfumo  huo  mpya   umeanza  kutekelezwa  kama  ilivyokusudiwa.Utekelezaji wa Mfumo huu mpya umekuwa  unatekelezwa katika mikondo (streams)  mikuu  miwili,  inayoenda  sambamba. Mkondo wa Kwanza ni kujenga na kuimarisha mfumo utakaohakikisha kuwa matokeo Makubwa tarajiwa katika mikakati yetu ya kuleta maendeleo endelevu Nchini yanapatikana (Strengthening the Delivery System). Mkondo wa Pili ni kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mikakati iliyoainishwa katika Awamu ya Kwanza ya uchambuzi wa Kimaabara (LABs).  

6.            Mheshimiwa Spika,  hadi  kufikia  mwishoni  mwa  mwezi  Juni,  2013  maandalizi muhimu ya Awamu ya Kwanza  ya uchambuzi wa kina wa kimaabara wa maeneo sita (6) yaliyochaguliwa Kitaalam ulikuwa umekamilika. Napenda   kuwakumbusha    kuwa,  maeneo   hayo   sita   ni: Nishati ya Umeme, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato. Kazi zilizotekelezwa katika kipindi hiki kifupi cha kuanzia Julai 2013 hadi sasa ni pamoja na zifuatazo:
a)    Serikali imemteua Mtendaji Mkuu wa Taasisi Mpya ya President’s Delivery Bureau (PDB) na amekwishaanza kazi tayari. Vilevile, Naibu Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo anayehusika na masuala ya Mageuzi ya Kilimo ameteuliwa hivi karibuni;

b)    Watendaji wa Wizara husika pamoja na Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote Nchini wamepata mafunzo kuhusu Mfumo Mpya wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa;

c)    Mawaziri wa Wizara Sita zilizoanza kutekeleza Mfumo Mpya wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) wameingia Mikataba ya Utendaji na Mheshimiwa Rais (Performance Contract) yenye Viashiria vya Utekelezaji (Key Performance Indicators). Aidha, Makatibu Wakuu wa Wizara Sita pamoja na Watendaji wao, Wakuu wa Mikoa yote, Makatibu Tawala wa Mikoa, pamoja na Watendaji wao, wote wameingia Mikataba hiyo ya utendaji kazi ili kufikia malengo yaliyowekwa;

d)         Muundo wa Taasisi ya President’s Delivery Bureau na ule wa Vitengo vya Kusimamia Utekelezaji katika Wizara (Ministerial Delivery Units – (MDUs)) umeidhinishwa tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2013. Aidha, tangu mwezi Julai 2013 Wizara zinazohusika na matokeo ya awali zimeunda timu za muda za kusimamia na kufuatilia utekelezaji ili usimamizi stahiki wa utekelezaji uweze kuendelea wakati taratibu za kupatikana kwa watumishi wa kudumu zikiendelea;

e)         Wizara zote sita zenye Miradi ya Kipaumbele chini ya Mfumo wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) ambazo ni Nishati, Kilimo, Maji, Elimu, pamoja na Uchukuzi zimeanza utekelezaji wa Miradi husika; na

f)             Wizara zote Sita zimeanza kuandaa ripoti za utekelezaji za kila wiki na kuziwasilisha kwenye President’s Delivery Bureau kama mfumo unavyoainisha.

7.            Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni kuundwa na kuanza kazi kwa Kamati Maalum za Kuratibu na Kusimamia Utekelezaji wa Miradi ya ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo  Makubwa’ (Big  Results Now) zinazojulikana kama National Key Results Areas (NKRA) Steering Committees. Kamati hizi zimeundwa na Wawakilishi wa Wadau muhimu katika kuhakikisha mikakati ya utekelezaji inatekelezwa  na  matokeo  tarajiwa yanapatikana kwa wakati. Kamati hizi zinaongozwa na Mawaziri husika na zinakutana mara moja kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji, ili kutatua vikwazo na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji.

8.            Mheshimiwa Spika, vilevile, Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Mageuzi na Utekelezaji (Transformation and Delivery Council – (TDC)) imeundwa na kuanza kazi. Kamati hii ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Rais ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia utekelezaji katika Mfumo wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now).  Kamati hii itakuwa inakutana mara moja kila mwezi kutathmini maendeleo ya utekelezaji na vilevile kuzipatia ufumbuzi changamoto na vikwazo ambavyo vitakuwa vimeshindwa kupatiwa suluhisho stahiki katika ngazi za Wizara.  Kamati hiyo itafanya kikao chake cha kwanza baadaye mwezi huu ambapo itapokea muhtasari wa taarifa ya utekelezaji wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) na kisha kutoa maamuzi na muongozo stahiki wa hatua za utekelezaji zinazofuata pale itakapohitajika. Katika maandalizi ya Kikao hicho, nilikutana na Mawaziri wote Sita wanaohusika tarehe 21 Agosti, 2013 kujadili hatua za utekelezaji na changamoto zilizopo na mikakati ya kuzipatia ufumbuzi. Aidha, kuanzia tarehe 7 hadi 8 Septemba, 2013 Ofisi yangu inatarajia kukutana na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kupitia na kujadili Taarifa za Utekelezaji katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

9.            Mheshimiwa Spika, muda ambao utekelezaji wa mfumo wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) umeanza kutekelezwa rasmi ni mfupi mno, lakini dalili zinaonesha kuwa, matokeo mazuri yataanza kuonekana muda si mrefu kuanzia sasa na yatakuwa yakianishwa kadri yanavyojitokeza. Serikali kwa ujumla imejipanga kuhakisha Miradi ya ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now) inatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu kwa kuzingatia Viashiria vya Utekelezaji (Key Performance Indicators - KPIs) vilivyoainishwa wakati wa uchambuzi wa kimaabara kwa mwaka huu wa fedha.

III.                   KILIMO

a)            Hali ya Chakula

10.         Mheshimiwa Spika, tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2012/2013 iliyofanyika kati ya Mwezi Julai na Agosti 2013 kwa Mikoa 25 imeonesha kuwa Mikoa 8 ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Kagera, Geita na Njombe itazalisha ziada ya chakula. Aidha, Mikoa 8 ya Kigoma, Simiyu, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani, Manyara, na Tanga itajitosheleza kwa chakula. Aidha, Mikoa 9 ya Dar es Salaam, Dodoma, Tabora, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Singida, Kilimanjaro na Mara itakuwa na uhaba wa chakula na kwamba Halmashauri 60 katika Mikoa 19 zitakuwa na maeneo tete yatakayokabiliwa na uhaba wa chakula.

11.         Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya uzalishaji na upatikanaji wa Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Agosti 2013 ni ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno ya msimu wa 2012/2013 kuanza kuingia sokoni. Bei za wastani za vyakula sasa hasa kwa mazao ya mahindi na mchele zimeanza na zinaendelea kushuka kufuatia uvunaji wa mazao hayo katika maeneo mbalimbali ya Nchi. Uchambuzi unaonesha kuwa bei ya wastani ya Mahindi Kitaifa imeshuka kutoka bei ya kilele ya Shilingi 774 kwa Kilo mwezi Februari, 2013 hadi Shilingi 513 kwa Kilo mwezi Agosti, 2013. Aidha, bei ya wastani ya mchele Kitaifa imeendelea kushuka kutoka Shilingi 1,825 kwa Kilo mwezi Februari, 2013 na kufikia Shilingi 1,215 kwa Kilo mwezi Agosti, 2013.

12.         Mheshimiwa Spika,  Wakala wa Hifadhi ya Chakula ilianza kazi ya ununuzi wa Nafaka (Mahindi na Mtama) Mwezi Julai, 2013 katika Vijiji kwa Shilingi 450 kwa kilo na katika Miji kwa Shilingi 480 kwa kilo. Aidha, ili kuufanya Wakala kupata chakula cha kutosha kinyume na ilivyokuwa mwaka jana 2012/2013, na kuwawezesha kushindana na wafanyabiashara, Serikali iliamua kuongeza bei watakayotumia Wakala kununulia nafaka hiyo hadi kufikia Shilingi 500 kwa Kilo katika vituo vyote vya ununuzi.

13.          Hali ya ununuzi na akiba ya chakula kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) inaendelea vizuri, na kwamba katika msimu wa mwaka 2013/2014, Wakala umepanga kununua Tani 200,000 za nafaka kupitia kanda zake kama ifuatavyo: Makambako (Tani 40,000); Sumbawanga (Tani 50,000); Songea (Tani 50,000); Dodoma (Tani 15,000); Arusha (Tani 20,000); Dar es Salaam (Tani 10,000); na Shinyanga (Tani 15,000). Hadi kufikia tarehe 03 Septemba, 2013 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula umenunua kiasi cha Tani 159,602 za Nafaka ambapo Tani 159,421 ni Mahindi na Tani 181 ni Mtama. Akiba ya nafaka katika Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kwa sasa ni Tani 182,587 zikiwemo Tani 182,406 za Mahindi na Tani 181 za Mtama. Kiasi hiki kinajumuisha Tani 22,985 zilizokuwepo katika Maghala kabla ya kufanyika kwa manunuzi hayo.

14.         Napenda kuwahakikishia Wananchi wote kupitia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imejipanga vizuri. Chakula cha kutosha kipo kwa maeneo yanayoelezwa kuwa na uhaba wa chakula; na hakuna Mwananchi atakayepoteza maisha yake kutokana na kukosa chakula. Nitumie fursa hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zenye chakula cha ziada kuwahimiza Wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao. Aidha, Halmashauri za Wilaya ziweke Mikakati madhubuti ya kuzuia ununuzi holela wa chakula kutoka katika mashamba ya Wakulima.

b)           Maandalizi ya Pembejeo za Kilimo kwa Msimu wa 2013/2014

15.          Mheshimiwa Spika, tutakumbuka kuwa katika Mkutano wa 11 wa Bunge nilieleza changamoto zilizoukumba Mfumo wa kusambaza Pembejeo kwa njia ya Vocha. Serikali iliamua kutafuta Mfumo tofauti ili kuondokana na changamoto hizo. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuweka utaratibu na uwiano wa Asilimia 80 kwa Vocha na Asilimia 20 kwa mikopo. Aidha, Serikali imeidhinisha Bajeti ya Shilingi Bilioni 112.46 kati ya kiasi hicho Shilingi Bilioni 19.97 za ufadhili wa Benki ya Dunia na Shilingi Bilioni 92.49 za Serikali kwa ajili hiyo.

16.          Mheshimiwa Spika, taratibu za zabuni za kuchapisha Vocha kwa ajili ya Mfumo huu wa ruzuku ya Vocha zimekamilika na hadi kufikia tarehe 29 Agosti 2013, Awamu ya Kwanza ya Vocha 300,000 kati ya Vocha 523,000 zinazohitajika kwa ajili ya maeneo yanayowahi msimu zilishawasili Nchini na zinaanza kusambazwa kwenda katika Mikoa ya Njombe, Mbeya, Katavi, Kigoma na Mwanza. Kiasi cha Vocha zilizobaki zinategemewa kusambazwa mara zitakapowasili baadaye mwezi Septemba, 2013.

17.         Mheshimiwa Spika, katika kujiandaa na utekelezaji wa utaratibu huu mpya wa upatikanaji wa mikopo ya pembejeo kwa njia ya Vikundi vya Wakulima, Serikali imeteua Mikoa Saba (7) ya Ruvuma, Njombe, Mbeya, Iringa, Manyara, Geita na Shinyanga kuanza na Vyama vya Ushirika vya Mazao (AMCOS) na Ushirika wa Kifedha (SACCOS) ambavyo vina Mikataba na Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA). Aidha, Serikali imeona ni vyema kuvishirikisha pia Vikundi vingine kama vya Umwagiliaji Maji ambavyo vina sifa ya kukopesheka.

18.         Ili kuhakikisha Mfumo huu mpya unasimamiwa na unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa, Serikali katika kipindi cha mwezi Septemba 2013 itaendesha Semina ya kutoa elimu ya mpango huu kwa watendaji wa Kilimo na Ushirika katika ngazi za Mikoa na Wilaya na Wawakilishi wa Vyama vya Ushirika katika Mikoa husika.

19.         Napenda kulieleza Bunge lako Tukufu na Wananchi wote kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu upatikanaji na usambazaji wa Pembejeo na Vocha za Ruzuku kwa mfumo huu. Nitumie nafasi hii kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, kusimamia kwa karibu upatikanaji na usambazaji wa Vocha na pembejeo hizo ili kuwasaidia Wakulima kuzipata mapema na kwa kiwango cha ubora unaotakiwa.

IV.                  NISHATI
                    
a)            Ujenzi wa Miundombinu ya Gesi Asilia

20.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya Kitaifa ya Kipaumbele katika Sekta ya Nishati katika Mfumo Mpya wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now). Miongoni mwa Miradi hiyo ni ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam pamoja na kujenga Mitambo miwili (2) ya kusafisha gesi hiyo katika maeneo ya Mnazi Bay-Madimba (Mtwara) na Kisiwa cha Songo Songo (Lindi).

21.         Mheshimiwa Spika, hadi sasa Meli nne (4) kati ya meli 12 zimewasili Nchini zikiwa na shehena ya  jumla ya Vipande 16,623 vya mabomba ambayo yameanza kusambazwa katika maeneo husika. Mabomba hayo yatawezesha ujenzi wa bomba wa umbali wa Kilomita 194 kati ya Kilomita 532 za umbali wa mradi wote. Kazi ya ujenzi wa nyumba za Wafanyakazi wa Mradi inaendelea, Mfereji wa Mabomba (Mkuza) umesafishwa kwa umbali upatao Kilomita 293 na kazi ya kuunga bomba (welding)  imeanza tangu tarehe 26 Agosti, 2013. Kazi ya kulaza bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam inategemewa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2014 na kukamilika kwa mradi wote kunatarajiwa kuwa Desemba, 2014.

22.         Mheshimiwa Spika, Bomba hilo la Gesi linatarajiwa kusambaza Gesi katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa, Somanga Fungu, Mkuranga, Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania kwa matumizi mbalimbali. Bomba litakuwa na uwezo wa kusafirisha Gesi Asilia futi za ujazo Milioni 784 kwa siku. Aidha, Bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha kiasi cha futi za ujazo Milioni 1,002 baada ya kujenga vituo viwili vya  kushindilia Gesi Asilia vitakavyojengwa maeneo ya Madimba (Mtwara) na Songo Songo (Lindi). Ni dhahiri kwamba kukamilika kwa Mradi huu mkubwa wa ujenzi wa Miundombinu ya Gesi Asilia ni kichocheo kikubwa cha Maendeleo kwa Wananchi wa maeneo hayo na kwa Uchumi wa Taifa letu kwa ujumla.

b)           Usambazaji Umeme Vijijini

23.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia imedhamiria kuendeleza Miradi ya kusambaza Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (Rural Energy Agency – REA). Tayari Miradi kumi (10) ya usambazaji umeme ipo katika hatua mbalimbali. Zabuni za kutafuta Wakandarasi zimetangazwa, wakati Miradi minne (4) ipo katika hatua za utekelezaji (Implementation Phase). Miradi iliyoanza kuwaunganishia wateja umeme wa Gridi ya Taifa ni; “Pending and New Application for Customer Connections” ambao unatekelezwa na TANESCO. Mradi huu kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka Agosti 2013, jumla ya Wateja 91,199 waliunganishiwa umeme. Kati yao wateja wapatao 17,355, sawa na Asilimia 19 waliunganishwa katika kipindi cha mwezi Julai mpaka Agosti, 2013 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mfumo mpya wa ‘Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa’ (Big Results Now). Jitihada za kuendeleza vyanzo vya Nishati Jadidifu (Renewable Energy) bado zinaendelea kwa kasi kwani Mradi wa “Sustainable Solar Market Packages (SSMP I)” ambao unatekelezwa Wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa chini ya msaada wa Benki ya Dunia pamoja na Serikali ya Tanzania. Tayari Taasisi za Umma 300 pamoja na Kaya 250 za Watu Binafsi zimefungiwa mifumo ya umeme-jua.

24.         Mheshimiwa Spika, miradi ya umeme itokanayo na maporomoko madogo ya maji ya Mawengi, (Njombe) utakaozalisha Megawati 0.3, Mwenga,  (Iringa)  utakaozalisha Megawati 4.0 na Mbagamao, (Ruvuma) utakaozalisha Megawati 1.0 nayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji  na uunganishaji wateja ambapo hadi kufikia tarehe 30  Agosti, 2013, jumla ya Wateja 1,510 kati ya 4,922 wanaolengwa wameunganishiwa umeme. Aidha, uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa “Electricity V Package III” ulifanyika tarehe 18 Julai, 2013, huko Ushirombo Bukombe. Mradi huo utatekelezwa kwenye Mikoa minne ya Kanda ya Ziwa ambayo ni: Geita, Mwanza, Simiyu na Shinyanga. Mradi utakapokamilika unatarajiwa kufikisha umeme katika Vijiji na kuunga wateja wa awali wasiopungua 18,600. Mradi huu unagharimiwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Tanzania.

25.         Mheshimiwa Spika, taratibu za kuwapata Wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza Mradi Kabambe wa kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili kwa njia ya Turnkey katika Mikoa ya Tanzania Bara chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency – REA) umekamilika na tayari Mikataba ya kutekeleza Mafungu ya Kazi kwa ajili ya kupata Wazabuni (Lots) 15 zilizopata Wakandarasi  imesainiwa. Mikataba hiyo 15 ni kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya kusambaza umeme vya Misongo ya Kilowati 11/33 vya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru; usambazaji umeme Vijijini katika Mikoa ya Katavi, Ruvuma, Mtwara, Njombe, Iringa, Dodoma, Singida, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mwanza, Mara, Arusha na Kilimanjaro. Aidha, Mafungu ya Kazi kwa ajili ya kupata Wazabuni (Lots) 10 hazikupata Wakandarasi zimetangazwa upya tarehe 16 Agosti, 2013. Zabuni zitakazopokelewa zinatarajiwa kufunguliwa tarehe 2 Oktoba, 2013. Mafungu ya Kazi kwa ajili ya kupata Wazabuni (Lots) hizo 10 ziligawanywa zaidi na kupata Lots ndogondogo 20 ili kuwezesha utekelezaji wa haraka na kwa muda mfupi. Mikoa ambayo inahusika katika Mafungu ya Kazi kwa ajili ya kupata Wazabuni (Lots) 10 ni Geita, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Pwani, Kagera, Manyara, Tanga, Lindi na Morogoro. Utekelezaji wa miradi yote ya Mafungu ya Kazi kwa ajili ya kupata Wazabuni (Lots) 25 unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2015.

26.         Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Wananchi wote na Watekelezaji wa Mradi huu kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha kwamba Miradi hii yote inakamilika.






V.                   MAJI

a)            Mfuko wa Maji

27.         Mheshimiwa  Spika, Wizara  ya  Maji  imekuwa  ikipokea maoni na ushauri  kutoka  kwa  Waheshimiwa  Wabunge na Wadau  mbalimbali kuhusu Bajeti na  utekelezaji  wa   Miradi   na   Programu   mbalimbali   za   Sekta  ya   Maji. Serikali inaendelea na mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Maji (National Water Investment Fund) ili kuongeza fedha za uwekezaji katika Sekta ya Maji kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 12 ya mwaka 2009 kwenye kifungu cha 44. Vyanzo vya mapato kwa utekelezaji huo ni fedha zilizoidhinishwa na Bunge na zitakazotolewa na Washirika wa Maendeleo. Hata hivyo, uanzishwaji wa Mfuko huo unahitaji pia maboresho kwenye Sheria za maji zilizopo. Aidha, katika Bajeti ya mwaka 2013/2014, jumla ya Shilingi Milioni 100 zimetengwa kama kianzio (seed money) cha Mfuko wa Maji. Hata hivyo, kutokana na umuhimu na ukubwa wa uwekezaji unaohitajika kwenye Sekta ya Maji, Wizara imebaini kuwa vyanzo vya fedha vilivyobainishwa kwenye Sheria ya Maji havitoshelezi. Hivyo, Wizara itaanza mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria hii ili kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato ya Mfuko.

b)           Nyongeza ya Bajeti ya Maji Shilingi Bilioni 184.5

28.         Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa, katika hatua za mwanzo za mchakato wa Bajeti ya mwaka 2013/2014, Serikali ilikuwa imetenga fedha za Miradi ya Maendeleo jumla ya Shilingi Bilioni 379.4 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maji Nchini. Miradi hiyo ililenga kuimarisha huduma za Maji Mijini na Vijijini, ikiwa ni pamoja na uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji. Pamoja na fedha hizo za Miradi, Serikali pia ilikuwa imetenga fedha za Matumizi Mengineyo Shilingi Bilioni 4.8 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Nchi nzima.
                                                                     
29.         Hata hivyo, kutokana na mahitaji makubwa ya huduma za maji Nchini, fedha zilizotengwa awali zilikuwa hazitoshi kufikia malengo yaliyowekwa. Kwa kuzingatia hilo, Serikali iliiongeza Bajeti ya Wizara ya Maji kwa jumla ya Shilingi Bilioni 184.5 ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 173.8 zilielekezwa kwenye Miradi ya Maendeleo na Shilingi Bilioni 10.7 zilielekezwa kwenye shughuli za uendeshaji. Hivyo, baada ya nyongeza hiyo, fedha za maendeleo sasa ni Shilingi Bilioni 553.2. Utekelezaji wa Miradi ya Maji iliyopangwa mwaka 2013/2014 kwa kutumia Bajeti hii mpya utawezesha kuwapatia Wananchi wa Vijijini huduma ya maji hadi Asilimia 60 ifikapo mwezi Juni 2014 kutoka Asilimia 57.8 za sasa.

30.         Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kutoa huduma ya maji kulingana na malengo ya Milenia na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa Wananchi waishio Vijijini wanapata huduma ya maji hadi kufikia Asilimia 65 ifikapo mwaka 2015. Hivyo, kwa fedha hizi za nyongeza, Vijiji Vitatu (3) vimeongezwa kwa kila Halmashauri ili kukamilisha jumla ya Vijiji Vitano (5) vya Awamu ya Pili. Fedha hizi za nyongeza zitatumika pia kugharamia baadhi ya Miradi ya Maji Vijijini inayoendelea kutekelezwa na Halmashauri kama ujenzi wa Mabwawa, uchimbaji wa Visima na kuendelea kugharamia Kampeni ya Usafi wa Mazingira.
                  


c)            Utekelezaji wa Miradi ya Maji baada ya Nyongeza

31.          Mheshimiwa Spika, fedha za nyongeza kwenye Miradi ya Maendeleo Shilingi Bilioni 173.8 zitaelekezwa katika Miradi kama ifuatavyo:
a)            Shilingi Bilioni 65 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Vijiji 10 kwa kila Halmashauri;

b)            Shilingi Bilioni 65.6 kwa ajili ya kutekeleza Miradi mbalimbali ya Maji Vijijini itakayoleta matokeo ya haraka;

c)             Shilingi Bilioni 18.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza Maji katika Mabwawa yaliyojengwa Iguluba, Sasajila, Habiya, Kirurumo, SekeIdidi, Matwiga, Kidete, Kawa, Mwanjoro na Wegero;

d)            Shilingi Bilioni 11.7 kwa ajili ya kukarabati na kujenga Miradi yenye kutoa huduma kwa Wananchi wengi na Vijiji vingi zaidi; na

e)            Shilingi Bilioni 12.9 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ugala kwenda Miji ya Urambo na Kaliua na kugharamia uboreshaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa mipya.

32.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Matumizi Mengineyo (OC), nyongeza ya Shilingi Bilioni 10.7 imefanya OC kufikia Shilingi Bilioni 15.5. Fedha hizo zitasaidia Wizara kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Programu ya Maji inayotekelezwa Nchi nzima, kulipia umeme wa Mamlaka za daraja B, C na miradi ya Kitaifa, kulipia stahili za Watumishi wa Wizara wanaofikia 1,541, kulipia huduma mbalimbali na Sekta Binafsi, kugharamia uendeshaji wa Chuo cha Maji kwa kulipia gharama za ufundishaji na chakula cha Wanafunzi, na kulipia ada za Taasisi za nje kulingana na mikataba na maridhiano na Nchi yetu.

33.          Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa Watumishi wote watakaohusika katika utekelezaji wa Miradi hii kutumia fedha hizi kulingana na mipango iliyowekwa ili Wananchi wawe na imani na juhudi hizi  za Serikali za kuongeza Bajeti ya Maji.

VI.                  MAANDALIZI YA KATIBA MPYA
                                     
a)            Maendeleo  ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba

34.         Mheshimiwa Spika, kama sote tunavyofahamu, tarehe 3 Juni 2013, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal alizindua Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
35.         Mheshimiwa Spika, baada ya kuzinduliwa kwa Rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilichapisha nakala za kutosha na kuzisambaza Nchini kote katika Ofisi za Watendaji wa Vijiji, Mitaa, Kata, Vitongoji na Shehia kwa upande wa Zanzibar ili kuwawezesha Wananchi kuisoma, kuijadili na kutoa maoni. 

36.         Mheshimiwa Spika, mara baada ya Uzinduzi wa Baraza, Tume ilianza mchakato wa kuandaa Mabaraza ya Katiba. Mabaraza hayo yamegawanyika katika makundi mawili: Kundi la Kwanza, ni Mabaraza ya Katiba ya Wilaya katika ngazi ya Serikali za Mitaa na Kundi la Pili ni Mabaraza ya Katiba ya Taasisi, Asasi, Taasisi na Makundi yenye Watu wenye malengo yanayofanana.

37.         Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yalisimamiwa na kuendeshwa na Tume kuanzia tarehe 12 Julai 2013 hadi tarehe 2 Septemba 2013. Jumla ya Wajumbe 10,932 wa Mabaraza ya Wilaya walipatikana. Vilevile, nakala za kutosha za Rasimu ya Katiba zilisambazwa kwa Asasi, Taasisi na Makundi ya watu wenye malengo yanayofanana. Pamoja na usambazaji huo, Rasimu ya Katiba iliwekwa katika tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) ili kuwawezesha Wananchi wengi zaidi kupata Rasimu ya Katiba kwa urahisi na hivyo kushiriki katika mchakato huu muhimu kwa Taifa letu.

38.         Mheshimiwa Spika, Tume kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), kwa upande wa Tanzania Bara na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), iliandaa na kuendesha mikutano miwili ya Mabaraza ya Katiba ya Watu wenye Ulemavu Mjini Zanzibar tarehe 5 Agosti, 2013 na hapa Dodoma tarehe 15 Agosti, 2013. Mikutano hii ilitoa fursa kwa Wawakilishi wa Watu wenye Ulemavu wa aina zote kushiriki na kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba.

39.          Mheshimiwa Spika, Sambamba na Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Tume iliruhusu Asasi, Taasisi na Makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kuunda na kuendesha Mabaraza ya Katiba kwa lengo la kuijadili na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni yao Tume. Mabaraza haya yalikuwa na uhuru wa kuanza kuijadili Rasimu ya Katiba mwezi Juni, 2013 na yalipaswa kuwasilisha maoni na mapendekezo yao kwa Tume kabla au ifikapo tarehe 31 Agosti, 2013.

40.         Mheshimiwa Spika, kwa sasa Tume inachambua maoni yaliyotolewa na Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Asasi, Taasisi na Makundi ya watu wenye malengo yanayofanana. Baada ya uchambuzi huu kukamilika, Tume itandaa Ripoti ambayo itaambatisha Toleo la Pili la Rasimu ya Katiba iliyoboreshwa kutokana na maoni ya Mabaraza ya Katiba na kuiwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inavyoelekeza.

41.         Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Wananchi wote, Asasi, Taasisi na Makundi yote ya Watu wenye malengo yanayofanana kwa namna walivyoshiriki katika Mabaraza ya Katiba na kutoa maoni yao. Ni matumaini yangu kuwa maoni yao yataisaidia katika kuiwezesha Tume kuboresha Rasimu ya Katiba kwa maslahi ya Taifa letu.  Wito wangu kwa Wananchi wote ni kuendelea kushirikiana na Tume ili kukamilisha zoezi hilo kama ilivyopangwa.

VII.                 AJIRA KWA VIJANA NA WASOMI

a)            Miradi ya Vijana Wilayani Sikonge

42.         Mheshimiwa Spika, mwishoni mwa mwezi Agosti 2013 nilipata fursa ya kuhudhuria Mahafali katika Chuo cha Nyuki Mkoani Tabora. Nikiwa Mkoani hapo nilipata pia fursa ya kutembelea Miradi kadhaa inayoendeshwa na Vijana; wengi wao wakiwa ni wahitimu wa Vyuo Vikuu hapa Nchini. Chimbuko la Miradi hii ya Vijana ni agizo la Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa mwaka 2012 kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote Nchini kutenga maeneo ya ardhi kwa ajili ya kuwasaidia Vijana wanaohitimu kutoka katika Vyuo mbalimbali. Lengo likiwa ni kuanzisha Miradi ya Kilimo ili waweze kujiajiri na baadaye kuwaajiri wenzao katika shughuli za kuzalisha mali. Aidha, Vikundi hivi vinalenga kuwapatia Vijana nguvu ya pamoja, kubadilishana uzoefu na kuwafanya kuwa na moyo wa kujiendeleza, na kuwa chachu ya mabadiliko kwa Vijana wengine na jamii kwa ujumla.

43.         Mheshimiwa Spika, nikiwa Wilayani Sikonge nilitembelea Mradi wa Kilimo chini ya kikundi cha Vijana wapatao 86 wa Kijiji cha “Pathfinders Green City” katika Vijiji vya Tumbili na Lufwisi Wilayani Sikonge. Mradi huu unalenga kutekeleza Miradi Midogo takribani 9 ikiwemo ya Ufugaji nyuki, Kilimo cha Bustani na mbogamboga kwa kutumia umwagiliaji kwa njia ya matone, ufyatuaji tofali, uhifadhi wa mazingira n.k. Tayari Miradi Mitano (5) imeanza na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na Minne (4) itaanza baada ya kukamilika kwa miundombinu ya Jengo la Utawala, Karakana ya Ufundi, mabanda ya Mifugo na Nyumba 12 za kuishi Vijana hawa.
                          
b)           Mradi wa Vijana – Igunga

44.         Mheshimiwa Spika, nilipata pia fursa ya kutembelea vikundi vya Vijana katika Wilaya ya Igunga. Nilielezwa kuwa kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi Julai, 2013 Wilaya ya Igunga imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 92.5 kwa Vikundi 56 vya Vijana. Mojawapo ya Vikundi hivyo ni Kikundi cha Graduates Integrated Youth Association (GIYA) ambacho kimepatiwa Ekari 300 na Wilaya kwa ajili ya kilimo cha alizeti na vitunguu. Vijana hawa wameshalima mashamba matatu yenye jumla ya Ekari 150 za Alizeti na Ekari Nne (4) za Vitunguu na wamekwishavuna Tani 30 za Alizeti ya thamani ya Shilingi Milioni 36.0. Wanatarajia kuuza mashudu Tani 18 ya thamani ya Shilingi Milioni 5.4, wanatarajia mauzo kuwa Shilingi Milioni 41.4, na kwa vile gharama ya uzalishaji zilikuwa Shilingi 14.5 wanatarajia kupata faida ya Shilingi Milioni 26.9. Ni dhahiri kuwa matarajio yao ni kufanya vizuri zaidi kwa miaka inayofuata kwa kuwa gharama za uzalishaji zitakuwa zimepungua.

45.         Mheshimiwa Spika, nilipata pia fursa ya kutembelea Shamba la kikundi cha Vijana 30 cha ELIBARIKI KILIMO lenye ukubwa wa Ekari 14 la kilimo cha mahindi, vitunguu, matikiti maji na mboga za majani katika Kijiji cha Mwanzugi. Walinieleza kuwa kwa Ekari 8 walizolima Vitunguu wanatarajia kuvuna Tani 11 zenye thamani ya Shilingi Milioni 27.5 kwa bei ya sasa ya Shilingi 2,500/= kwa Kilo.

46.         Mheshimiwa Spika, kwa ujumla nimevutiwa sana na Mfumo wa maisha ya Vijana hawa ya kuishi katika Makambi, kwa Mfumo wa Maisha Plus. Niliona juhudi za Mkoa za kuwaletea watu watakaowapa Vijana hawa stadi za maisha ambapo walimwalika Mwanzilishi wa Maisha Plus Bw. Masoud Ally (maarufu kwa jina la Masoud Kipanya) ili akae na Vijana hawa kwa muda. Nimemwambia Bw. Masoud kuwa sasa Wananchi wanataka kuona Maisha Plus ya kweli na si ya kuigiza itakayowafanya Vijana wengi kuvutiwa na kujiingiza katika vikundi vya uzalishaji. Aidha, nilimwomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora apeleke watu wa kuwatia moyo Vijana hawa ili wasikate tamaa.

47.          Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuupongeza sana Uongozi  wa  Mkoa  wa  Tabora  pamoja  na Wilaya zake  kwa  juhudi  kubwa  za kuwawezesha Vijana kujitambua, na kuthubutu  kuanza miradi hii na kuwasaidia kuondoa dhana kuwa wasomi ni lazima wapate kazi za kuajiriwa.  Niupongeze  pia  Uongozi  wa Mkoa wa Tabora kwa kutumia vyema Ushuru wa Mazao, yaani Crop Cess katika kuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwa Vijana wetu. Niliambiwa kuwa Asilimia 20 ya Crop Cess katika Halmashauri za Wilaya Mkoani Tabora zinarudishwa Vijiji na Asilimia 80 inatumika kwa shughuli za maendeleo kama vile, kusaidia Vijana. Niliambiwa kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ilitumia Ushuru wa Mazao, yaani Crop Cess kuwapatia Vijana wa Pathfinders jumla ya Shilingi 488,230,500/= katika msimu wa mwaka 2012/2013 na Shilingi 300,000,000/= zimetengwa katika Bajeti ya mwaka 2013/2014. Wilaya ya Igunga kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi Julai, 2013 imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 92,500,000/= kwa Vikundi 56 vya Vijana. Nawapongeza sana!

48.         Kutokana na kazi hiyo nzuri katika Mkoa wa Tabora, nichukue fursa hii kuiagiza Mikoa ambayo haijatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wafanye hivyo mapema kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo katika maeneo yao. Nitapenda kupata taarifa kutoka katika kila Mkoa kuhusu utekelezaji wa agizo hili mapema iwezekanavyo.

c)            Kutumia Vijana Wasomi kuanzisha Miradi (Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperative - SUGECO)

49.         Mheshimiwa Spika, mwaka 2008 nilipokuwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine kama mgeni Rasmi katika siku ya Maadhimisho ya Kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, nilipata nafasi ya kuzungumza na Wakufunzi na Wanafunzi kuhusu Maendeleo ya Kilimo Nchini na changamoto zake. Nilitoa changamoto kwa Jumuiya ya Wanafunzi na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine kwamba Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine wanaotaka kuonyesha kwa vitendo namna ya kutumia vizuri elimu waliyoipata, kujitokeza na kuchangamkia shughuli na fursa nyingi zilizopo kwenye Kilimo/Mifugo ili wawe mfano bora wa kuigwa na Wakulima Vijijini katika kuleta mabadiliko chanya ya kuongeza tija na uzalishaji katika Kilimo, Ufugaji Nyuki, Mifugo na Uvuvi. Niliwaahidi kuwa iwapo watajitokeza, Serikali ipo tayari kuwasaidia. Aidha, nilishauri waandae Maandiko ya Miradi mizuri wanayopenda kuanzisha na kuiwasilisha Serikalini ili Miradi hiyo itafutiwe fedha kutoka kwenye Vyombo vya Fedha.

50.         Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Julai, 2013 nilipata fursa ya kukutana na wawakilishi wa Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperative - SUGECO) ambao wanaendesha takriban Miradi ya Kilimo 11 Nchini ikiwemo ya ufugaji wa samaki, kuku, nguruwe na nyuki. Ipo pia Miradi ya kukausha mbogagamboga na matunda na kukamua mafuta ya alizeti. Changamoto kubwa wanazokabiliana nazo Vijana hawa ni pamoja na kutopata mitaji, kushindwa kumiliki ardhi, kukosa masoko ya uhakika na hata kushindwa kupata nembo za ubora kwa bidhaa zao.

51.         Niliwaalika baadhi ya Mawaziri wakiwemo wa Wizara za Uwezeshaji na Uwekezaji, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi; Kazi na Vijana; Kilimo, Chakula na Ushirika; Viwanda na Biashara; Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; na Fedha ili kupata fursa ya kuwasikiliza Vijana hao. Kwa pamoja tulishirikiana na kuweka mikakati ya kuwawezesha Vijana hawa wa (Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperative - SUGECO) kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. Nimewaelekeza Waheshimiwa Mawaziri kuweka mikakati ya kuwawezesha (Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperative - SUGECO) kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.


52.          Mheshimiwa Spika, kutokana na mifano hiyo mizuri niliyoiona katika Mkoa wa Tabora na kutoka kwa Vijana wa (Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperative - SUGECO) nimeona kuna umuhimu wa kuwasaidia Vijana wanaohitimu Vyuo Vikuu na wengineo wanaopenda kujiingiza katika Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, n.k. ili wawe chachu ya maendeleo Vjijini. Ni dhahiri kwamba, tukiamua kwa dhati na kujipanga vizuri tunaweza kuwasaidia Vijana hao kuleta mabadiliko makubwa katika Kilimo Nchini. Wito wangu sasa ni:

Kwanza:        Watanzania wote tuweke nguvu zetu katika kuwasaidia Vijana ambao tayari wamejiajiri kwa kuwawezesha kupata huduma muhimu zikiwepo chakula na miundombinu muhimu ikiwemo umeme na maji. Aidha, Wizara na Taasisi zenye dhamana ya Kilimo wawasaidie kupata pembejeo na zana bora za uzalishaji ili Miradi hii iweze kuongeza uzalishaji na hatimaye  kufikia kiwango cha kujitegemea.

Pili:                 Viongozi wa Halmashauri kuwajibika ipasavyo na kutumia fedha za Umma kwa manufaa ya Taifa letu.

Tatu:              Viongozi wanaohusika na Ushirika wawasaidie na kuwaongoza vijana hawa waliojiunga pamoja kujisajili Kisheria ili waweze kukopesheka.

Nne:               Uongozi wa Wilaya na Mkoa kuwashirikisha makundi yote ya Taasisi mbalimbali zikiwemo Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini na Watendaji wengine katika kuwasaidia Vijana na kuhakikisha kuwa Wananchi wanaozunguka maeneo yenye Miradi ya Vijana wananufaika na ujuzi wa Vijana na hatimaye kubadilisha maisha yao kwa ujumla.

Tano:             Viongozi wa Mikoa na Halmashauri katika ngazi zote kutambua kuwa Vijana hawa bado wanahitaji kulelewa kimaadili, hivyo wawe karibu na Vijana kwa kuwapatia semina za malezi ikiwemo michezo na burdani.

Sita:                Vyuo vingine vya Elimu ya Juu viweke Mipango madhubuti ya kuwasaidia Wahitimu wa fani zilizopo katika Vyuo hivyo kuanza Ushirika kama wa (Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperative - SUGECO).


VIII.               MAHUSIANO YA TANZANIA NA NCHI ZA NJE

a)            Ujio wa Viongozi na Faida Zilizopatikana

53.         Mheshimiwa Spika, tangu mwezi Machi 2013, Nchi yetu ilipata heshima kubwa ya kutembelewa na Viongozi Mashuhuri  Duniani.  Ujio wa Viongozi hao ni uthibitisho wa kuimarika kwa  Mahusiano na Ushirikiano baina ya Serikali yetu na Nchi za Nje. Viongozi waliotutembelea  ni pamoja; na
i)             Rais wa China  Mheshimiwa Xi Jinping

54.         Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa  Xi Jin Ping  alifanya ziara Nchini kuanzia tarehe 24 - 25 Machi, 2013.  Ujio wa Rais Xi Jinping uliwezesha kusainiwa Mikataba na makubaliano 17 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.  Baadhi ya Makubaliano hayo ni Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, itakayojengwa na Kampuni ya Merchants Holding ya China.  Mkataba mwingine ni ule wa kujenga barabara itakayounganisha Bandari hiyo  na Reli ya kati na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zanzibar. Mkataba mwingine ni  kuendeleza Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Rais Xi Jin Ping pia alizindua na kukabidhi  rasmi Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kituo hicho kimejengwa mahsusi ili kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ziara hiyo ilikuwa muhimu  kwani imeimarisha uhusiano wetu na Nchi ya Watu wa China. 

ii)            Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama

55.         Mheshimiwa Spika, tarehe 1 - 2 Julai 2013, Nchi yetu ilipata heshima ya kumkaribisha Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama. Lengo la ziara ya Mheshimiwa Barack Obama  lilikuwa  kuimarisha  uhusiano  katika Nchi hizi mbili katika nyanja za Ushirikiano wa Kidiplomasia, Kiuchumi na Kibiashara n.k. Manufaa yanayotarajiwa kutokana na ujio wa Rais wa Marekani ni pamoja na:

a)            Kuimarika zaidi uhusiano wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani katika nyanja za Kibiashara na Uwekezaji;

b)            Kuongezeka kiasi cha Misaada ya Maendeleo na Ufundi kitakachotolewa katika  Nyanja za Afya, Elimu, Kilimo, Barabara, Nishati, na Maendeleo ya Vijana;

c)            Katika kuhakikisha Sekta ya Umeme inaimarishwa, Mheshimiwa Obama alizindua Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Umeme unaojulikana kama “Power Africa Initiative”.  Chini ya Mpango huu, Serikali  ya Marekani itatoa  jumla  ya  Dola  za  Kimarekani Bilioni 7 na Makampuni Binafsi yatawekeza Dola Bilioni 9.  Lengo la Mpango huu ni kuimarisha upatikanaji wa umeme Barani Afrika.  Kwa kuanzia mpango huu utatekelezwa katika Nchi Sita za Bara la Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo.  Nchi nyingine ni Ethiopia, Ghana, Nigeria, Liberia na Kenya.

iii)           Rais Mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush

56.         Mheshimiwa  Spika, vilevile, tulipata  fursa ya kumpokea Rais Mstaafu wa Marekani Mheshimiwa George W. Bush, aliyefanya   ziara   kuanzia  tarehe  1 hadi 3 Julai 2013.  Kupitia Asasi yake ya George Bush Foundation waliandaa Mkutano wa Kimataifa wa Wake wa Marais wa Afrika. Aidha, katika Mkutano huo, ulizinduliwa Mpango wa Kuimarisha Mapambano Dhidi ya Kansa ya Shingo ya Kizazi na Matiti. Aidha, kupitia Mpango huo Serikali ya Marekani ilitoa Dola Milioni 3 na Mashine 16 za CryoTherapy zinazotumia baridi kali kuua chembe chembe za Kansa.

iv)        Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair

57.         Mheshimiwa Spika, tarehe 23 mwezi Julai, 2013 Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Mheshimiwa Tony Blair alitembelea Nchini mwetu. Kupitia Taasisi yake ya Africa Governance Initiative aliahidi kusaidia kusambaza umeme wa jua katika Shule za Sekondari Vijijini, kuboresha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kusaidia uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Programu za Maendeleo (President’s Delivery Bureau - PDB).

v)         Waziri Mkuu wa Nchi ya Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra

58.         Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra alifanya ziara ya siku tatu Nchini kuanzia tarehe 30 Julai, 2013. Lengo la ziara hiyo ilikuwa kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia, Kiuchumi na Kibiashara kati ya Thailand na Tanzania. Serikali pia ilitiliana saini Mikataba  Mitano ya Ushirikiano katika Nyanja za Kukuza na kulinda vitega uchumi; kubadilishana wafungwa; kukuza ushirikiano wa kiufundi; na ushirikiano kwa masuala ya madini.

59.         Serikali ya Thailand kupitia Waziri Mkuu huyo, imeahidi kutoa ufadhili kwa vijana 10 kusoma Shahada ya Uzamili Nchini humo. Vilevile, Nchi hiyo itaanza kuleta wataalamu wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana na Wataalam wetu kuimarisha huduma ya afya Nchini.

vi)        Rais Mstaafu wa Marekani Mheshimiwa Bill Clinton

60.         Mheshimiwa Spika, Rais wa 42 wa Marekani, Mheshimiwa  Bill  Clinton  alifika  Nchini  tarehe 3 Agosti 2013.  Kupitia Taasisi yake ya Clinton Foundation na Mradi wa Maendeleo wa Clinton Development Initiative (CDI), alisaini  makubaliano na Serikali ya kuendeleza Sekta ya Kilimo na kuwasaidia Wakulima wadogo wadogo kuboresha  Kilimo na kiwango bora cha uzalishaji wa mazao.

61.         Mheshimiwa Spika, kimsingi, ujio wa Viongozi hao Mashuhuri katika kipindi kifupi, pamoja na wengine wengi kutoka Nchi za Afrika na sehemu nyingine ni uthibitisho thabiti wa kuimarika kwa  Demokrasia ya ndani, kuwepo kwa Amani na Utulivu, kuimarika kwa utawala bora na kuwepo kwa mazingira bora ya uwekezaji. Kwa ujumla Mafanikio yanayotarajiwa kupatikana  kutokana na Ujio wa Viongozi ni mengi lakini kwa kutaja machache ya jumla ni pamoja na:
·                     Kuimarika kwa ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania na Nchi hizo na Nchi nyingine;

·                     Tanzania kufaidika na mitaji ya maendeleo kutoka Nchi hizo kwa ajili ya kujenga miundombinu; na

·                     Kufunguka milango ya uwekezaji katika Sekta mbalimbali.  Ziara za Viongozi hao imetoa fursa kwa Wawekezaji kote Duniani kuona mazingira mazuri na fursa za uwekezaji zinazopatikana Nchini.

b)           Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya wote (Global 2013 Smart Partnership)

62.         Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, na kama nilivyogusia wakati nafunga Mkutano wa 11 wa Bunge lako Tukufu, tarehe 28 Juni hadi  tarehe 1 Julai 2013, Nchi yetu ilipata heshima ya kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote mwaka 2013 (Global 2013 Smart Patnership Dialogue).  Mkutano huo wa Kimataifa ambao Agenda yake kuu ilikuwa ni “Matumizi ya Teknolojia kama Nyenzo ya Kuleta Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi Barani Afrika” (Leveraging Technology  for Africa’s Social Economic Transformation.  The Smart Partnership way) ulihudhuriwa na Washiriki zaidi ya 800 kutoka Mabara yote Duniani. Idadi hiyo ilijumuisha Wakuu wa Nchi, Serikali, Wanadiplomasia, Wawakilishi wa Makampuni ya Ndani na Nje ya Nchi, Wasomi, Wafanyabiashara n.k.

63.         Mheshimiwa Spika, manufaa yaliyopatikana kutokana na Mkutano huo ni pamoja na:
·                     Kuhimiza matumizi ya Sayansi na Teknolojia pamoja na kujenga uwezo wa ndani katika uvumbuzi, ubunifu, umiliki na uendelezaji katika maendeleo endelevu ya Kijamii na Kiuchumi kwa njia shirikishi;

·                     Mkutano huo pia umetoa fursa kwa Nchi yetu kujifunza na kupata uzoefu wa dhana ya ushirikiano kwa manufaa kwa wote (Smart Partnership) na kuweza kusaidia kuibua fursa zilizopo za kukuza uchumi na kuondoa umaskini; na

·                     Kutokana na idadi kubwa ya Washiriki waliohudhuria kutoka Nchi mbalimbali Duniani, Nchi yetu iliweza kutangaza fursa za Uwekezaji na Utalii zilizopo Nchini.

64.         Mheshimiwa Spika, napenda niungane na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwashukuru Wananchi wote, hususan wa Mkoa wa Dar-es-Salaam kwa kushiriki kikamilifu katika mapokezi ya Viongozi wote waliotembelea Nchi yetu na kuhakikisha kwamba inadumu katika hali ya Amani na Utulivu. Nawasihi Wananchi wote tuendelee kudumisha Amani na Utulivu pamoja na Mshikamano tuliouonesha.
                           
IX.                  UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA

65.         Mheshimiwa Spika, Vita dhidi ya Dawa za Kulevya Nchini vilianza siku nyingi. Kwa kutambua uzito wa Vita hii, mwaka 2006, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Kikosi Kazi cha Taifa cha kushughulikia Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini. Kikosi hiki kinaundwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama  kikijumuisha  Maafisa  kutoka  Jeshi  la  Polisi,  Idara ya Uchumi na Forodha, Idara ya Uhamiaji, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na Idara ya Usalama wa Taifa.

66.         Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumetokea matukio ya usafirishaji wa Dawa za Kulevya Nchini, hasa kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Kambarage Nyerere. Kwa upande wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, kazi za kudhibiti Dawa za Kulevya hufanywa kwa utaratibu wa Kikosi Kazi (Task Force) kwa Polisi wa Kudhibiti Dawa za Kulevya, Polisi wa Viwanja vya Ndege, Uhamiaji, Idara ya Ushuru wa Forodha na Idara ya Usalama wa Taifa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).

67.         Mheshimiwa Spika, Kikosi Kazi cha Taifa cha kushughulikia Dawa za Kulevya pamoja na Vyombo mbalimbali vya kudhibiti usafirishaji na matumizi ya Dawa za Kulevya licha ya changamoto zilizopo, vimefanya kazi kubwa kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini. Kwa mfano, Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini tarehe 8 Machi, 2010 huko Kabuku – Mkoa wa Tanga, Watuhumiwa 5 walikamatwa wakiwa na Kilo 95 za Dawa za Kulevya aina ya Heroin. Watuhumiwa hao wamefungwa miaka 25 na kulipa faini ya Shilingi Bilioni 1.5  kila mmoja. Tarehe 19 Desemba, 2010 huko huko maeneo ya Kabuku tena Mkoa wa Tanga Watuhumiwa 2  walikamatwa  wakiwa  na  Kilo  50 za Dawa za Kulevya aina  ya  Heroin  zilizokuwa  zinasafirishwa  kutoka  Dar es Salaam  kwenda  Sudan kupitia Kenya. Tarehe 21 Februari, 2011 huko Mbezi Jogoo Wilaya ya Kinondoni, Watuhumiwa 4 walikamatwa wakiwa na Kilo 179 za Heroin.

68.          Tarehe  04 Machi, 2011 huko Kawe, Wilaya ya Kinondoni  walikamatwa  Watuhumiwa  4 wakiwa na Kilo 81 za Heroin. Tarehe 07 Septemba, 2011 huko Mbuyuni, Kinondoni Watuhumiwa 4 walikamatwa wakiwa na Kilo 97 za Heroin  na  tarehe 12 Januari, 2012 huko Mchinga Mbili, Mkoa wa Lindi,  Watuhumiwa  4 walikamatwa  wakiwa  na Kilo 211 za Heroin. Haya ni  baadhi  tu  ya  Mashauri  yaliyopo katika Mahakama mbalimbali Nchini. Upelelezi wa Mashauri hayo yote umekamilika na yapo katika Mahakama Kuu kwa hatua ya kusikilizwa. Mashauri haya ni kielelezo tosha cha kutoa picha kwamba, Kikosi Kazi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya hufanya kazi kwa uadilifu mkubwa kwa kushirikiana na Vyombo vingine kutoka Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali.

69.         Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2010 hadi Julai, 2013, Mashauri 368 yanayohusu Dawa za Kulevya yalipelekwa Mahakamani na Mashauri 91 kumalizika kwa mafanikio kwa watuhumiwa kufungwa na wengine kutozwa Faini. Kwa sasa kuna takriban Mashauri 245 ambayo bado yako Mahakamani. Changamoto inayotukabili katika Vyombo vyetu vya Mahakama na Jeshi la Polisi ni katika kuharakisha Mashauri  hayo.  Pamoja  na changamoto hiyo ni maoni yangu kuwa “Task Force” iliyoundwa na Mheshimiwa Rais, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinafanya kazi nzuri sana katika vita hii. Tunachotakiwa ni kuwapa Moyo wale wote waliohusika katika kuwakamata Watuhumiwa wote wa Dawa za Kulevya, ili waweze kufanya kazi kwa bidii zaidi. Aidha, ni vizuri ikibidi kuwapandisha Vyeo Maafisa kadhaa kutokana na juhudi hizo.

70.         Mheshimiwa Spika, tukio la Uwanja wa Ndege wa JNIA la tarehe 05 Julai, 2013 ambapo wako Watu waliokamatwa na Dawa za Kulevya, mara baada ya taarifa hizo kupatikana, Kamati Ndogo ya Ulinzi na Usalama ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Julius Nyerere ilikutana tarehe 09 Julai, 2013 na kuagiza uchunguzi uanze mara moja. Kwa utaratibu, jalada lilifunguliwa, watuhumiwa kuhojiwa na hatimaye jalada hilo kupelekwa  kwa  Mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam tarehe 29 Julai, 2013 kwa ajili ya maamuzi ya Kisheria. Taratibu za kukamilisha uchunguzi wa tukio hili zinaendelea.

71.         Kama nilivyosema, changamoto kubwa tuliyonayo ni uharakishaji  wa  Mashauri  ya  Dawa za Kulevya ambayo nina imani tukijipanga vizuri inawezekana. Iko hoja kwamba, labda  tutafika  mahala tufikirie kuwepo na Mahakama Maalum ya  Dawa za Kulevya ambayo itakuwa na kazi moja tu  ya  kusimamia  Mashauri  yanayohusu  Dawa  za  Kulevya. Vilevile, Vita vya Dawa za Kulevya ni shirikishi kwa kushirikiana na Nchi mbalimbali Duniani. Jitihada hizi hufanywa kwa kufanya Mikutano ya pamoja ambapo mikakati mikubwa ya kufanya misako ya pamoja, mafunzo ya pamoja na matumizi ya Vifaa mbalimbali hupangwa. Vilevile, kuhamasisha kutunga Sheria Kali zinazofanana ili kutotoa mwanya kwa watuhumiwa kupenya na kufikisha Dawa za Kulevya kwa watumiaji. Ni kweli kwamba, Vita vya Dawa za Kulevya haiwezi kukomeshwa na Nchi moja, kwa hiyo Mapambano dhidi ya Wafanyabiashara Haramu wa Dawa za Kulevya yatafanikiwa tu, kwa Nchi zote Duniani kuungana katika kudhibiti biashara hii. Wauzaji, Wasafirishaji na Watumiaji wa Dawa hizi tunao katika jamii zetu na baadhi yao tunawafahamu. Nitoe wito kwa Wananchi wote kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kuwafichua na kutoa taarifa za wale wote wanaojihusisha na Biashara ya Dawa za Kulevya. Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaobainika kuhusika na Dawa za Kulevya.
    
X.                   HITIMISHO

72.         Mheshimiwa Spika, napenda nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na kwa michango yenu mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake pamoja na Wataalamu wote wa Serikali na Taasisi zake kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu.

73.         Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema wakati mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi. Kwa maana hiyo, naomba sasa kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 29 Oktoba, 2013 Saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Ukumbi huu hapa Dodoma.


74.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: