Na Hassan Abbas
WAKATI
dunia ikiingia muongo wa pili katika karne ya 21, yaani mwaka 2012, wanataaluma
wawili waliandika maoni mawili kuonesha hisia zao mbili tofauti. Hawa hawakuwa
wakitofautiana, bali wote walikuwa wakieleza na kuainisha hoja na haja ya
kuonesha changamozo za msingi za kufanyiwakazi na dunia hii tuliyomo.
Mchumi
mashuhuri duniani Joseph Stiglitz, aliaandika katika makala yake “The Year of Personal Pessimism”
akionesha wasiwasi wake kuwa uchumi wa dunia ungedorora zaidi, lakini kwa
upande wake aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair, yeye aliamini katika
makala yake “Taking Faith Seriously”
kuwa lazima tuendeleze mwafaka baina ya watu wa dini na tamaduni mbalimbali ili
dunia iwe salama zaidi.
Wote
hawa walikuwa wakizungumzia mambo wanayodhani katika mwaka huo yangeikwaza au
kuisukuma dunia katika maendeleo zaidi. Walitofautiana juu ya nini kifanyike
lakini walikuwa wanaungana juu ya umuhimu wa dunia kuwa salama zaidi kiuchumi,
kisiasa na kijamii.
Nimetanguliza
nukuu hizo kuonesha sote tunavyoweza kuwa na maoni tofauti na katika namna
tofauti lakini tukiwa sote tunakubaliana kuhusu jambo moja muhimu na
adhimu-maendeleo na maisha ya watu.
Huu
ndio mtazamo wangu wa kati baada ya kuzisoma makala mbili zilizojaa ufundi za
hivi karibuni kuhusu maoni ya watu wawili adhimu-Balozi Ombeni Sefue, Katibu
Mkuu Kiongozi wa Ikulu yetu ya Dar es Salaam na kwa upande wa pili mmoja wa
wanahabari makini nchini, komredi Peter Nyanje.
Ingawa
makala hizi ziliandikwa miezi kadhaa iliyopita kwa sababu bado uzito na umuhimu
wake wa hoja zilizomo unaendelea kuwepo na kuibua mijadala mingine zaidi,
nimeona si kosa nami leo nikaingia katika mjadala huu.
Katika
maoni yake aliyoyapa anuani ya “Presidential Delivery Unit a waste of money,”
aliyoyachapisha katika gazeti la The
Citizen, komredi Nyange alionesha wasiwasi wake, moja kuhusu kufanikiwa kwa
Kitengo kitakachoanzishwa cha Kufuatilia Utekelezaji wa Miradi Mikubwa (PDB)
chini ya dhana ya BIG RESULTS NOW.
Katika
andiko lake mhariri na rafiki yangu huyu wa zamani katika taaluma alionesha
wasiwasi kadhaa ikiwemo kuhoji kama kuanzishwa kwa Kitengo cha Ufuatiliaji
(PDB) chini ya Ofisi ya Rais si kuhamisha majukumu ambayo tayari yapo Tume ya
Mipango na katika Mawizara mbalimbali?
Mahali
fulani komredi Nyange alihoji kutokana na mengi ya kihistoria: “Considering the
country’s failure to accomplish many development projects due to financial
constraints, the establishment of the Presidential Delivery Unit does not make
sense at all.”
Akichangia
hoja katika makala yake aliyoipa anuani ya “Learn from history: Don’t be
condemned by it,” mwanajumuiya mwenzangu na mwanamijadala katika Majadiliano
Yenye Manufaa kwa Wote (Smart Partnership Movement), Balozi Sefue alieleza tofauti
kubwa kati ya Tume ya Mipango na PDB.
Alieleza
kuwa wakati Tume ya Mipango inapanga na kusimamia mipango na maeneo mapana ya
kitaifa ya maendeleo ya nchi, PDP itakuwa ikisaidia kusimamia utekelezaji wa
kasi na haraka wa maeneo machache ya mkakati na yanayohitaji matokeo ya haraka
zaidi.
Balozi
Sefue aliandika: “What President Jakaya Kikwete, his government and Parliament
have decided is that we have to find a lasting solution to this problem of
implementation.
“Putting
more money through a system that falls short on delivery would be the real
“waste”. Establishing the PDB will not lead to duplication of monitoring and
evaluation efforts. PDB will instead fill gaps in the existing delivery system
by, for the first time, bringing together essential “disciplines”.
Nimefurahi
leo nami kuingia katika mjadala huu kwa sababu kama nilivyoainisha katika
anuani ya makala yangu hii, mimi ni muumini wa utekelezaji si uteterekaji
katika suala la maendeleo. Kama wanamjadala hao wote wanavyokubaliana, wakati
fulani mahali fulani nchi yetu imekumbwa sana na changamoto ya utekelezaji.
Wakati
fulani suala si fedha, suala si watu na wala suala si mipango mizuri bali
kukosekana kwa mfumo makini na wa kitaalamu wa usimamizi wa utekelezaji
kumekwaza sana kufikiwa kwa haraka na wakati mwingine kutofikiwa kabisa kwa
baadhi ya mambo yaliyopangwa.
Dhana
au falsafa ya BIG RESULTS NOW (BRN) kama ninavyoielewa imelenga kuja na tiba
mujarabu ya gonjwa hili. Gonjwa la kupanga si kutekeleza. Gonjwa la kutekeleza
kusikokuwa na uwiano na mipango. Na gonjwa la kutekeleza mengi yenye uwiano na
mipango lakini si kwa lengo la haraka (SASA) na bila kujali aina ya matokeo:
MATOKEO MAKUBWA au MAJANGA MAKUBWA!
Ukiangalia
muktadha wa kuanzishwa kwa dhana hii na hicho kitengo ni dhahiri kuwa haya ni
mageuzi makubwa tunayopaswa kuyapa nafasi katika nchi yetu. Nasema hivi kwa
sababu binafsi nina amini kuwa walioleta dhana hii hawakutumia hisia, kujitakia
bali tafiti.
BRN ni utafiti si kujitakia
Napingana
na wanaodhanai kuwa uamuzi wa nchi yetu kutekeleza dhana hii ya utekelezaji
labda ni jambo la mtu mmoja tu kajitakia iwe hivi. Binafsi naamini kuja kwa
falsafa hii ni matokeo ya uongozi uliosikiliza na kutafakati maoni na kelele
nyingi za wananchi na tafiti za watafiti.
Dhana
kwamba tumekuwa na tatizo katika nchi zetu zinazoendelea hasa katika eneo la
kutambua vipaumbele na kutekeleza kwa makini, si suala la hisia tena. Bahati
nzuri wana mjadala wenzangu niliowataja hapo juu nao wote kwa pamoja
wanakubaliana na hili.
Bahati
nzuri Bara la Afrika hivi sasa lina hazina ya Ripoti za utafiti zinazoainisha
masuala anuai yanayokwaza Bara hili kuendelea. Katika Ripoti za Mpango wa
Afrika Kujitathmini katika Utawala Bora (APRM) za nchi zaidi ya 15 sasa za
Afrika zilizofikia hatua ya kutahminiwa ikiwemo Tanzania, kumesheheni matokeo
haya ya kiutafiti.
Ripoti
ya nchi yetu kwa mfano ya APRM ile ya awali (2009) na ya sasa iliyokamilika ya
mwaka 2013 zote zinaainisha tatizo hili la falsafa yetu ya maendeleo huko nyuma
kuathiriwa sana na changamoto katika utekelezaji na usimamizi wa utekelezaji wa
mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma.
Katika
andiko la kutafakari miaka 10 tangu kuanzishwa kwa APRM ambayo Tanzania pia ni
moja ya nchi wanachama tena hai, wataalamu wa masuala ya utawala bora
walioongozwa na mnazi mkubwa wa sera za Mwalimu Nyerere, komredi wangu Prof.
Ahmed Muhiddin wa Kenya wanasema katika kijitabu chao “African Peer Review
Mechanism; Best Practices and Lessons Learnt” (2013) kuwa Afrika imeponzwa sana
na eneo hili la utekelezaji na ni gonjwa la kutafutiwa dawa.
Kwa
hakika kwa maoni ya watafiti hawa (empirical evidence) na hata hali halisi
(observed reality) tunayoiona katika
siku na zama hizi hatupaswi kubaki tukifungwa minyororo na historia. Historia
inapaswa kutoonesha makosa yetu ya jana, kutusaidia tuyarekebishe leo ili tuwe
na kesho bora zaidi.
Kwa
kuwa watafiti wote hawa wanakubaliana kuwa kuna mahali tulikosea katika
nadharia yetu ya maendeleo, si kosa kuweka mikakati ya kurekebisha hali hii.
Mwalimu Nyerere alisema katika “TUJISAHIHISHE” kuwa kujikosoa ni kujisahihisha.
Hivyo
basi kwa nchi yetu kuichukua falsafa hii iliyopimwa na kuthibitishwa kuwa na
manufaa (tested delivery model) kutoka kwa ndugu zetu Malaysia, kuiweka katika
mazingira ya Kitanzania, kwangu mimi ni HATUA KUBWA.
Nimepata
kukutana na Dr. Omar Abdulrahman mmoja wa watu walioisaidia sana Malaysia
tunayoisikia sasa na pia mmoja ya vichwa nyuma ya Mpango kama huu wa Big
Results huko Malaysia.
Kwa
wasiomfahamu, Dr. Omar ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa Waziri Mkuu maarufu sana
wa Malaysia, Dr. Mahathir Mohammed katika eneo la teknolojia kwa
maendeleo.Akitoa siri ya mafanikio ya Malaysia anasema ni kuchagua, kupanga na
kutekeleza.
Ukikutana
na watu walioyaona haya kivitendo kama Dr. Mahathir mwenyewe na CEO wa sasa wa
Kitengo cha Kusimamia Utekelezaji (PEMANDU) kule Malaysia, Prof Idris Jalla
wote watakwambua siri hiyo hiyo kwamba kama unataka maendeleo ya haraka lazima
uchague maeneo mahsusi, uyawekee mkakati na kisha utekeleze ipasavyo.
Ninachokiona
hapa kuhusu wasiwasi unaoanza kujitokeza ni umuhimu mkubwa wa jamii
kufahamishwa muktadha, maudhui na hata hatua na mafanikio ya mabadiliko haya
yote ninayoamini yana manufaa kwa jamii yote.
Nasema
hivi kwa sababu naamini kuwa Serikali au taasisi inaweza kupanga na kufanya
makubwa lakini si tu yasionekane bali msingi na mantiki yake ukakumbana na
ushindani mkubwa kwa sababu tu watu hawana ufahamu.
Ni
changamoto kwa wanamipango walioko nyuma ya BRN na hata PDB kuweka mkakati
maalum wa mawasiliano kwa umma, mkakati utakaotekelezwa kwa weledi ili wananchi
wafahamu tena katika kila hatua kwa nini BIG RESULT ni MATOKEO MAKUBWA na si
MAJANGA MAKUBWA (kama jamaa yangu mmoja alivyokwenda mbali na kuuita hivyo).
Mkakati
huo utakuwa unajibu maswali magumu ya wananchi kila siku lakini pia utakuwa
ndio hasa majibu kwa wasiwasi uliowajaa watu wengi waliofungwa minyororo na
mfumo wa zamani waliouona haukuwa na ufanisi sana.
Hivyo
naungana na Balozi Sefue kuwa tusifungwe minyororo na historia, nisisitize pia
kuwa ni vyema tukaungana kama Taifa katika kutekeleza mipango yetu kuliko
kuendelea kuacha utekelezaji ukitetereka kama ilivyokuwa katika mifumo ya
awali.
*Mwandishi
ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na sheria. Kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo
Cha Mawasiliano katika Mpango wa Afrika Kutathmini Utawala Bora (APRM
Tanzania).Maoni 0713 584467.Baruapepe: habbas@aprmtanzania.org
No comments:
Post a Comment