Tuesday, September 10, 2013

Ardhi haiwezi kuwa chanzo cha upotevu wa amani - Waziri Mkuu Pinda

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itahakikisha kuwa ardhi ambayo Watanzania wamepewa na Mungu haibadiliki na kuwa chanzo cha upotevu wa amani nchini.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Septemba 10, 2013) wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa siku tatu unaojadili haki na amani katika masuala ya ardhi Tanzania ulianza jana jijini Dar es Salaam.
 
“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa ardhi yetu haileti laana bali inabakia kuwa baraka ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia. Ninawasihi wale wote wenye mamlaka na utoaji wa ardhi wahakikishe kuwa wanatimiza wajibu wao wanaposimamia masuala ya ardhi ili haki isipotee na hatimaye kuepusha migogoro ya ardhi,” alisema.
 
“Ninawasihi Watanzania iwe ni wanasiasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, wasomi na umma wote kwa ujumla. Ninaomba tuitunze amani tuliyonayo na tutambue kwamba Tanzania ndiyo nchi pekee tuliyojaliwa kuwa nayo. Madhara ya ukosefu wa amani ni makubwa. Tuangalie nchi za wenzetu zenye migogoro  na tuone jinsi machafuko hayo yatatuathiri sisi wenyewe, watoto wetu na wajukuu wetu,” alisisitiza.
 
Alisema anatambua hofu ambayo imewakumba watu wengi kuhusiana na uwekezaji iwe ni kwenye kilimo ama madini.  “Ninatambua kwamba kuna hofu kubwa imejengeka miongoni mwa wananchi wengi hasa wanaposikia suala la uwekezaji hasa kwenye kilimo,” alisema.
 
Alisema tangu wakati Mwalimu Nyerere akiwa madarakani, alishasema kuwa ardhi ni rasilmali ya watu wote. “Aliweka mifumo ambayo hairuhusu mtu kumiliki ardhi ambayo haina ukomo, kuna ukomo wa miaka kati ya 33 na 99. Na pia kuliwekwa masharti kuwa ni lazima ukipata ardhi uiendeleze, usipoiendeleza, unanyang’anywa,” aliongeza.
 
Alisema kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999, imekataza mgeni (Mtanzania ambaye si mzawa) kumiliki ardhi hapa nchini. “Ardhi inatolewa kwa wawekezaji, chini ya sheria ya uwekezaji kwa muda maalum. Mwekezaji akimaliza muda wake, anatuachia ardhi yetu, na ndiyo maana Serikali ya Kijiji hairuhusiwi kutoa ardhi zaidi ya ekari 50,” alisema.
 
Alisema chini ya sheria ya ardhi na sheria ya uwekezaji, hapa nchini kuna wawekezaji wakubwa 122 ambao ni wa ndani na wa nje na kwa ujumla wao wanamiliki kilometa za mraba 1,296 kati ya kilometa za mraba 945,087 ambazo ni ukubwa wa nchi nzima.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 200 wakiwemo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi wa dini, washiriki kutoka nchi za Ujerumani, Sweden, Burma, Finland, Norway na Afrika Kusini.

No comments: