Friday, August 2, 2013

watanzania waishio ughaibuni watakiwa kuwalea watoto wao kwa kufuata mila na desturi za kitanzania

Na Anna Nkinda- aliyekuwa Gaborone,  Botswana

Watanzania waishio nchi za nje wametakiwa kuwalea watoto wao katika misingi bora ya malezi yanayofuata mila, desturi  na utamaduni wa mtanzania ili waendane  na maadili ya kitanzania ya kuishi kwa unyenyekevu, upendo, ushirikiano na kuheshimu watu.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais  Mama Salma Kikwete wakati wa futari ya pamoja iliyoandaliwa na chama cha watanzania waishio nchini Botswana (ATB) katika hoteli ya Grand Palm mjini Gaborone nchini humo.

Mama Kikwete alisema kuwa ni vizuri watoto wawe na tabia njema inayokubalika na jamii ya kitanzania kuliko kulelewa katika mazingira yatakayowafanya wajue mila na tamaduni za nchi zingine kwani nyumbani ni nyumbani na ili  waendane na  hilo ni lazima walelewe kama  wazazi wao walivyolelewa.

“Ninawapongeza kwa  kuwa na umoja imara na wenye nguvu na ushirikiano ambao unawafanya kuwa kitu kimoja na pale ambapo jambo lolote linatokea liwe zuri au baya mnaweza kukabiliana nalo kwani  umoja ni nguvu na mahali penye upendo chuki hujitenga”, alisema Mama Kikwete.

Alisema ni jambo la kufurahisha kuona kuwa ndani ya  umoja huo kuna umoja wa kinamama ambao lengo lao ni  kuwaweka watoto pamoja na kuwafundisha mila na utamaduni wa mtanzania na kuwaomba wanawake ambao hawajajiunga na umoja huo waweze kujiunga  ili wajenge mshikamano ambao ni silaha kubwa ya watanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini humo Radhia Msuya Mtengeti alisema kuwa umoja huo ni wa kuigwa mfano kwani wanafungu la kuwasaidia watanzania wenye shida pia kila mwaka wanafanya ukaguzi wa hesabu zao za fedha jambo ambalo ni nadra kufanyika katika vyama vingine.

Balozi Mtengeti alisema, “Nimekuwa nikishirikiana na umoja huu katika kazi zangu zote ni watu wanaoshirikiana na Serikali na hata pale ambapo sipo kazi zimekuwa zikifanyika  bila tatizo hakika najivunia kuwa na watanzania wenye moyo wa kujitolea na kujituma kama hawa”.

Alisema kuwa wao kama watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa njia moja au nyingine wanaunga mkono kuchangia mikakati mbalimbali ya maendeleo ya  kuwasaidia watanzania kwani nchi yenye maendeleo ya mama na mtoto ni lazima itambulike kimataifa.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa kinamama Rehema Kalabam alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya ya  kuisaidia jamii ili kuhakikisha kuwa kina mama na watoto wa Tanzania wanapata  maendeo na kumuomba aendelee kufanya hivyo kwani  yeye kama mke wa Rais akiamua kufanya  jambo kila mtu atamsikiliza na kumuunga mkono.

“Tuliamua kuanzisha umoja huu tangu mwaka 2004 lengo letu  kuu likiwa ni  kuhakikisha kuwa kina mama wanashiriki kikamilifu katika kusaidia malezi ya jamii na hasa watoto wa kitanzania, kuwafundisha mila na tamaduni nzuri za nyumbani na za hapa ambazo ni nzuri”, alisema Mama Kalabam.

Alisema wanawasaidia  vijana katika hatua za ukuaji, kuwakutanisha wanawake ili waweze kuangalia namna wanavyoweza kuwasaidia  watu wenye mahitaji nchini Botwana na Tanzania.

Pia wanawasaidia wanawake wasikae bila ya kufanya kazi  wawe na mambo mbalimbali ya kufanya. Katika kutekeleza hilo wanamfuko wao  ambao unawasaidia  kina mama katika jitihada mbalimbali za kujikwamua kiuchumi kama vile kufanya biashara hivyo basi wanawakopesha fedha wahitaji ambazo wanazirudisha kidogokidogo.

Mama kikwete alikuwa nchini humo kwa ajili ya kuhudhulia  mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Lengo kuu la mkutano huo ilikuwa ni kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia na stadi za maisha jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi  ugonjwa wa Ukimwi.

1 comment:

Anonymous said...

Hongera mama. Mbona hakuna picha?