UZINDUZI
WA CHAMA CHA WAZAZI WA WATOTO WENYE ULEMAVU WA MTINDIO WA UBONGO, AKILI NA
VIUNGO TANZANIA. (CHAWAUMAVITA)
UTAKAOFANYIKA SIKU YA JUMAMOSI AGOSTI 24’ 2013 KATIKA UKUMBI WA SABASABA AMBAPO
MGENI RASMI ANATARAJIWA KUWA RAIS WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA
JAKAYA MRISHO KIKWETE.
1.0 UTANGULIZI
Kwa kuwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za Binadamu
kwa watoto wenye ulemavu wa Mtindio wa ubongo, akili na viungo vimekuwa
vikishamiri nchini;
Na kwa kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakifarakana,
kukimbiana, na hata kumtelekeza mtoto na pia wakati mwingine kumdhuru mtoto
mwenye ulemavu baada ya mtoto huyo kuzaliwa au kupatwa na ulemavu baadaye;
Na kwa kuwa kumekuwa na dhana potofu iliyotawala
katika jamii juu ya upatikanaji wa watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo, akili
na viungo na maisha yao kwa ujumla;
Na kwa kuwa hakuna huduma za awali kabla na baada ya
tatizo zilizo endelevu zitolewazo kwa watoto wenye mtindio wa ubongo, akili na
Viungo kwa watoto/watu wanoishi na ulemavu huo;
Na kwa kuwa mipango na mikakati iliyopo nchini haikidhi changamoto
zinazoendelea kujitokeza kwa
watoto/watu wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo, akili na viungo nchini;
Na kwa kuwa
mtoto mwenye ulemavu ni sawa na mtoto mwingine yeyote anastahili kupata
huduma na vifaa tiba maalum vya matibabu, na nafasi sawa ya elimu na mazoezi
ili kumsaidia kufikia malengo yake ya kimaisha;
Na kwa kuwa sisi wazazi na wananchi kwa ujumla tuna
jukumu la awali la kuhakikisha kuwa
watoto/watu wenye ulemavu wa mtindio wa
Ubongo na Viungo wanakuwa salama na duniani panakuwa ni mahala bora pa kuishi
kwao;
HIVYO
BASI Sisi Wazazi wa Watoto wenye Ulemavu wa Mtindio wa
Ubongo na Viungo tunaopata huduma katika Hospitali na vituo vya CCBRT tuliamua, kuunda chama kiitwacho CHAMA CHA WAZAZI WA WATOTO WENYE ULEMAVU WA
MTINDIO WA UBONGO, AKILI NA VIUNGO TANZANIA. (CHAWAUMAVITA)
Dira ya CHAWAUMAVITA ni kuwa CHAMA cha mfano
kinachochangia upatikanaji wa huduma
bora na endelevu kwa watoto wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo
Tanzania ili kuhakikisha watoto wenye Ulemavu huo wanasaidiwa kukabiliana na
changamoto zilizopo na kuandaa mazingira bora ya makuzi na maisha yao kwa
ujumla.
Chama kimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya ndani tangu
April 2013 kwa usajili wenye namba S.A 18732.
MALENGO
YA CHAWAUMAVITA NI:-
Kuwaleta pamoja watu/familia zinazolea watoto wenye ulemavu wa mtindio wa Ubongo, akili
na viungo ili kubadilishana uzoefu, kupata elimu ya namna ya kuwatunza watoto
wenye ulemavu huo.
Kutoa elimu ya ulemavu wa Mtindio wa Ubongo na
Viungo kwa jamii ili Kupunguza athari na
maumivu yatokanayo na Mtindio wa Ubongo, akili na viungo.
Kukusanya, kuchapisha na kusambaza taarifa
zinazohusu matatizo yatokanayo na ulemavu wa Mtindio wa Ubongo,akili na viungo.
Kuwasaidia wanachama/wazazi katika kuwatunza na kutetea na kupata haki zao kwa mujibu wa
sheria.
Kujenga na kuendeleza vituo vya mazoezi tiba, kuratibu
na kusambaza vifaa tiba kwenya vituo na;
Kujenga na kuimarisha vituo kwa ajili ya masuala ya
kijamii na michezo kwa watoto wenye
ulemavu
UZINDUZI
Baada ya Usajili, CHAWAUMAVITA iliandaa Mpango
Mkakati wa Miaka mitano 2013-2018 ambao una
lengo la kuwasaidia watoto wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo akili na
Viungo pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili kwanza jamii ishiriki katika kuzuia
upatikanaji wa watoto hawa na pia iwalee na kuwasaidia kupata mahitaji yao
muhimu ya kila siku pamoja na kufikia malengo yao ya kimaisha
Ni kwa muktadha huu Ndio maana tumeamua kufanya
Uzinduzi wa Chama cha CHAWAUMAVITA na kumualika Rais Jakaya Mrisho Kikwete
ili:-
Ø Kuishirikisha jamii na wadau wengine kushiriki
katika harakati kupigania ustawi wa watoto wenye ulemavu kwa maslahi ya watoto
wote wa Tanzania wenye Ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na Viungo.
Ø Kuzindua Mpango Mkakati wa chama wa miaka mitano
2013-2018.
Ø Kuonyesha Makala Filamu (Documentary) inayoonyesha
hali halisi ya maisha ya jamii inayowalea watoto wenye ulemavu wa Mtindio wa
Ubongo Akili na Viungo pamoja na walezi wao.
Ø Kuzindua tovuti ya Chama na kualika juhudi za wadau
katika kuchangia harakati za kufikia malengo ya Chama na jamii kwa ujumla.
Uzinduzi utafanyika siku ya jumamosi ya tarehe
24.08.2013, saa 4:00 Asubuhi hadi saa 8:00 Mchana. Na Mgeni rasmi anatarajiwa
kuwa Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr Jakaya Mrisho Kikwete.
Chawaumavita inachukua fursa hii kuwaalika wadau
wote muhimu wakiwemo waandishi wa habari, Serikali, Mabalozi, Asasi na taasisi
mbalimbali kushiriki katika tukio hili muhimu kwa maslahi ya watoto wenye
ulemavu wa Mtindio wa Ubongo, Akili na viungo Tanzania.
Imtolewa na
Jonathan
Kawamala
MWENYEKITI
CHAWAUMAVITA
MAFANIKIO
Kwa takribani kipindi cha mwaka mmoja tangu
kuanzishwa na kusajiliwa kwa chama, tumeweza kufanya yafuatayo;
·
Kujenga mawasiliano mazuri na taasisi za serikali ,binafsi na za kiraia.
·
Mwaka jana kupitia wizara ya afya,tuliweza kupata mfadhili katika kampuni
ya Montero kwa kushirikiana na mama ANNA MKAPA ambapo watoto walemavu 50
waliweza kupatiwa baiskeli za watoto wenye ulemavu kutoka katika vituo mbali
mbali jiji Dar es salaam.
·
Kupata usajili wa kamili,kuandikisha wanachama wapya na kuongeza hamasa
kwa wazazi wenye watoto walemavu.
Changamoto:
·
ELIMU kuhusu upatikanaji wa watoto wenye ulemavu haijafikishwa kwa jamii
vya kutosha,
·
Elimu juu ya utunzaji, mazoezi tiba, huduma za kijamii kwa wazazi imekuwa
hairidhishi
·
Asilimia kubwa ya wazazi wenye watoto walemavu ni akina mama wa nyumban
ambao hawana fursa ya kupata bima za afya hivyo utunzaji wa watoto ni gharama kubwa.
Tunaamini-
“Umoja daima ndio suluhisho kwa changamoto”
Kwa
pamoja tukishikamana tutashinda. AHSANTE!
No comments:
Post a Comment