·
Japan itasaidia
Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika Afrika
·
Kushiriki maboresho
Reli ya Kati
·
Kusaidia kupanua na
kuboresha Bandari ya Dar Es Salaam
·
Viwanda vya Japan kujengwa
nchini kikiwemo cha kutengeneza pikipiki za Honda
·
Ni matokeo ya Ziara
ya Rais Kikwete Japan
JAPAN imeamua kuanzisha
ushirikiano mkubwa zaidi na Tanzania ambako nchi hiyo itaifanya Tanzania kuwa
nchi lengwa ya Japan na kuiwezesha kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika
Afrika kwa nia ya kuiwezesha kuwa na uchumi ulioimarika na wenye kuzalisha
ajira nyingi kwa wananchi.
Uamuzi huo wa Japan ni matunda
ya mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe yaliyofanyika
Tokyo, Japan wakati Rais Kikwete alipotembelea nchi hiyo Juni, mwaka huu, 2013.
Uamuzi na msimamo mpya wa Japan
umetangazwa rasmi leo, Jumamosi, Agosti 10, 2013 na Waziri wa Uchumi, Biashara
na Viwanda wa nchi hiyo, Mheshimiwa Toshimistu Motegi alipokutana na kufanya
mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu, Dar Es Salaam.
Kwa upande wa Tanzania,
mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anashughulika na Uwekezaji na Uwezeshaji
Mheshimiwa Mary Nagu, Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Abdallah
Kigoda na Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe.
Waziri Motegi amemwambia Rais
Kikwete kuwa ametumwa na Waziri Mkuu Abe kufuatilia mazungumzo kati yao na kutangaza
rasmi kuwa Japan imeiteua Tanzania kuwa nchi lengwa na kitovu cha uwekezaji wa
Japan katika Afrika Mashariki na katika Afrika kwa jumla.
Waziri Motegi pia amemwambia
Rais Kikwete kuwa pia amekuja Tanzania kutoa taarifa kuwa Japan iko tayari
kushiriki katika kuboresha na kuifanya ya kisasa zaidi Reli ya Kati kwa kujenga
njia ya kimataifa badala ya njia nyembamba ya sasa. Amesema kuwa Japan itatuma
wataalam wake kuangalia jinsi gani ya kuanza kazi hiyo ya uboreshaji wa Reli
hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Motegi
ametangaza kuwa Japan itashiriki katika upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar
Es Salaam kwa kuifanya ya kisasa zaidi.
Waziri Motegi amesema kuwa
katika azma ya Japan ya kuifanya Tanzania nchi ya mfano katika Afrika katika
uwekezaji na uchumi ulioimarisha, amekuja na kundi la wafanya biashara wa Japan
ambao wanaendelea kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Tanzania kuona jinsi
gani wanavyoweza kusaidiana katika kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Waziri pia amesema kuwa
moja ya malengo ya uamuzi huo wa Japan ni kuhakikisha kuwa bidhaa ambazo kwa
sasa zinanunuliwa moja kwa moja kutoka Japan zitazalishwa hapa nchini katika
viwanda ambavyo vitajengwa na makampuni ya Japan.
Kwa kuanzia amesema kuwa
makampuni mawili ya Honda na Panasonic yamekubali kujenga viwanda nchini kimoja
kwa ajili ya kutengeneza pikipiki za Honda hapa hapa nchini na kingine kwa
ajili ya kutengeneza vifaa vya umeme.
“Huu ni mwanzo tu Mheshimiwa
Rais kwa sababu kama nilivyosema kuwa tunataka Tanzania kuwa nchi mfano ya
uwekezaji wa Japan katika eneo hili la
dunia na namna hiyo kwa pamoja tutakuwa tumeshirikiana katika kuongeza ajira
kwa wananchi wa Tanzania,” Mheshimiwa Motegi amemwambia Rais Kikwete.
Waziri huyo pia amesema kuwa
baadhi ya makampuni ya Japan yana mipango ya kuwekeza katika kilimo, na hasa
kilimo cha pamba, na kuanzisha viwanda vya nguo hapa hapa nchini.
Wakati wa mazungumzo yao mjini
Tokyo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Mkuu Abe kuwekeza zaidi katika Afrika
akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa makubwa duniani ambayo yamefanikiwa
kupata soko kubwa katika Afrika na hasa soko la magari.
Uamuzi huo wa Japan na ziara ya
Mheshimiwa Motegi inakuja wiki na miezi michache baada ya Tanzania kuwa
imepokea viongozi wa mataifa mengi yakiwemo mataifa makubwa ya Marekani na China
na inathibitisha ni kiasi gani siasa na sera za Tanzania zinavyokubalika
duniani.
No comments:
Post a Comment