Na
Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu lilikuwa na majadiliano juu ya
kukosekana kwa usawa wa kiuchumi na kijamii
kati ya mtu na mtu, na baina ya
nchi na nchi na adhari zake kwa mstakabali
wa amani, usalama na maendeleo endelevu.
Majadiliano
hayo ya siku moja
yaliandaliwa na Rais wa Baraza Kuu Bw Vuk Jeremic na kufunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon, yaliwahusisha baadhi
ya mawaziri kutoka nchi kadhaa, wakuu wa Mashirika yaliyo chini ya Umoja wa
Mataifa, Jumuiya za Kikanda pamoja na
Asasi zisizo za kiserikali.
Akifungua majadiliano hayo, Katibu Mkuu amesema, licha ya kuwapo kwa mafanikio kadhaa
katika upatikanaji wa huduma za kijamii,
kama vile afya, elimu, maji safi na salama kupitia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya
Millenia ( MDGs). Bado pengo kati ya walionacho
na wasio nacho ni kubwa na linaendelea kukua.
Kwa mfano, anasema, katika miaka michache iliyopita jumuiya ya kimataifa imeshuhudia
ongezeko la idadi ya watoto wanaokwenda
shule hasa watoto wa kike, kupungua kwa
vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga, na vita dhidi ya magonjwa kama vile malaria, maambukizi ya ukimwi na kifua kikuu.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuboresha maisha ya watu milioni 200
wanaoishi katika makazi duni , huku watu
milioni mia sita wakiondolewa kutoka katika umaskini wa kupindukia.
Hata hivyo anasema
Ban Ki Moon. “ Lakini mafanikio haya na mengine mengi hayana uwiano uliosawa ndani ya mataifa mbalimbali na baina ya taifa moja na jingine. Mataifa mengi, tajiri na maskini yanashuhudia ongezeko
la ukosekanaji wa usawa wa kiuchumi na
kijamii”.
Akasisitiza kwa kusema sura ya pengo hilo la
usawa katika maeneo kwa vile afya
na elimu inajionyesha dhahiri kati ya kaya za matajiri na maskini.
Ban Ki Moon anasema idadi kubwa ya watu wanaoishi katika mazingira magumu wengi wao
wana kiwango kidogo cha elimu, au elimu yao ni duni inayowakosesha ujuzi na uwezo wa
kushindana katika soko la leo la ajira.
Kama hiyo haitoshi
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataia, ameeleza pia kwamba, pengo la ukosefu wa fursa za kiuchumi na kijamii pia linaongezeka sana
kati ya maeneo ya mijini na yale ya
vijijini. Akatoa mfano kwa kusema zaidi
ya watu 2.6 bilioni ambao hawana huduma za usafi wa mazingira na maji taka wengi wao wanaishi maeneo ya vijijini.
Akatahadharisha
kwa kusema, kukosekana kwa usawa wa kiuchumi na kijamii kuna weza kuwa
chimbuko la uhalifu, milipuko ya magonjwa, uharibifu wa
mazingira na kudhoofisha ukuaji wa uchumi na maendeleo.
Ban Ki Moon anasema
ndio maana suala la usawa limekuwa moja ya nguzo muhimu katika majadiliano yanayoendelea hivi sasa juu ya mwelekeo wa ajenda ya maendeleo baada ya 2015.
Akasema kunahitajika mikakati madhubuti na mageuzi
makubwa ili kuikabili changamoto hii ya kupunguza pengo la ukosefu wa usawa.
Anataja baadhi
ya mabadiliko na mikakati hiyo kuwa ni
pamoja na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kiuchumi na kifedha
na kuendelea na juhudi za kutokomeza umaskini uliokidhiri na njaa.
Akasisitiza pia umuhimu wa kuongeza uwekeza zaidi katika afya elimu, ulinzi wa jamii, ajira za
uhakika hususani kwa vijana na uwezeshwaji wa wanawake katika maeneo yote.
Kuhusu
ajira Katibu Mkuu anaeleza kuwa zinahitajika
ajira mpya milioni 470 kati ya mwaka 2014 na 2030.
Baadhi ya washiriki wa majadiliano hayo akiwamo Rais
wa Baraza Kuu, Bw. Vuk Jeremic walisisitiza
haja na umuhimu wa nchi kushirikiana katika kutafuta mbinu muafaka za
kupunguza pengo kati ya walionacho na wasionacho. Washiriki hao pia walielezea juhudi mbalimbali zinazochukuliwa
na serikali zao katika kukabiliana na changamoto hiyo.
No comments:
Post a Comment