Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa na Mkuu mpya ya UNAMID Luteni Jenerali Paul Ignace Mella na kulia ni Luteni Jenerali Wynjones Mathew Kisamba Naibu Kamanda na ambaye pia alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda Mkuu UNAMID. Luteni Jenerali Mella na Luteni Jenerali Kisamba walikuwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa ziara ya Kikazi na mafunzo. Lt. Jenerali Mella anasema yupo tayari kulitekeleza jukumu alilokabidhiwa na Umoja wa Mataifa na kwamba uteuzi wake katika wadhifa huo ni heshima kubwa wa Tanzania, Afrika, kwake yeye binfasi na zaidi kwa JWTZ ambayo mwaka itakuwa inatimizia miaka 50 tangu kuanzishwa kwake
Mkuu Mpya wa UNAMID Luteni Jenerali Mella akiwa katika picha ya pamoja na waambata wa kijeshi kutoka nchi za Afrika na kwingineko wakati alipotambulishwa kwao katika hafla fupi iliyoandawali na Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. kutoka kushoto ni Naibu Mwakilishi Balozi Ramadhan Mwinyi, Lt. Jenerali Wynjones Kisamba, Balozi Tuvako Manongi, Lt. Jenerali Paul Mella na Maj. Jenerali Ngodi Mkuu wa jeshi la kulinda amani huko Lebano (UNFIL).
Mkuu mpya wa UNAMID, Luteni Jenerali Paul Mella akibadilishana mawazo na Kanali Mike Redmond ambaye ni Mwambata Jeshi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa.
Luteni Jenerali Mella akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa mataifa, wamo pia Balozi Tuvako Manoni, na Luteni Jenerali Kisamba.
Waambata Jeshi kutoka kushoto Kanali Mike Redmond ( UK) Luteni Kanali Tiffany Harris ( mwanadada) Naibu Mwambata Jeshi( Marekani), anayefuatia ni Mwabata Jeshi wa Kenya na Mkuu wa UNAFIL.
Na Mwandishi Maalum
Ni heshima kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni heshima kubwa kwa Afrika, ni heshima kubwa kwangu mimi binafsi, lakini kubwa zaidi ni heshima kubwa kwa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo mwakani litakuwa linatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Hiyo ni kauli ya Luteni Jenerali Paul Ignace Mella, Mkuu mpya wa Jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Mataifa katika Jimbo la Darfur (UNAMID)
Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, kwa madhumuni ya kumtambulisha Mkuu huyo mpya wa UNAMID kwa Waambata wa Kijeshi hususani wa Kiafrika na wengineo walioko Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Aidha hafla hiyo ililenga pia kutambua mchango mkubwa na wa kutukuka wa Naibu Kamanda na ambaye pia amekuwa akikaimu nafasi ya Kamanda Mkuu wa UNAMID Luteni Jenerali Wynjones Mathew Kisamba naye kutoka JWTZ.
Akizungumzia uteuzi huo ambao ulitangazwa hivi karibu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. Luteni Jenerali Mella amesema pamoja na heshima kubwa kwa nchi yake, kwa Afrika na JWTZ, lakini pia anasema anatambua fika changamoto na jukumu kubwa lililombele yake, jukumu la kuwalinda wananchi wa Jimbo la Darfur na kurejesha amani ya kudumu kati ya pande zinazopingana.
“Ni jukumu kubwa lenye changamoto nyingi, lakini nimejiandaa kulikabili na kuzikabili changamoto zilizo mbele yangu nipo tayari kuutumikia Umoja wa Mataifa” anasema Luteni Jenerali Mella.
Na kuongeza “ Dhamana kubwa ya jeshi la kulinda amani katika Darfur ni kuhakikisha usalama unapatikana wakati wote hususani kwa wananchi wasiokuwa na hatia na vilevile kwa Mashirika ya Kimataifa yanayopeleka misaada ya kibinadamu kwa wananchi hao. Pamoja na kuendeleza majadiliano ya kutafuta amani na kuhakikisha kwamba makubaliano yanapatikana na yanadumishwa kati ya pande zinazopigana”.
Mkuu huyo wa UNAMID alikuwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa ziara ya mafunzo na maandalizi ya kuanza jukumu lake, ambapo pia alihudhuria kikao cha pamoja cha Makamanda wa Misheni zote za Ulinzi wa amani chini ya Umoja wa mataifa. Kikao hiki hufanyika New York kila mwaka.
Akizungumzia kuhusu mafunzo waliyopewa, Luteni Jenerali Paula Mella, anasema mafunzo waliyopewa pamoja na mambo mengine, yalihusu mafunzo ya ukaguzi na uthibitishaji wa weledi, utayari na utimamu wa wanajeshi wanaopelekwa kulinda amani kupitia Umoja wa Mataifa.
Amefafanua zaidi kwa kusema kwamba wanajeshi wanaopelekwa katika misheni za kulinda amani wanapitia hatua mbalimbali za mafunzo ya kuthibitisha weledi wao, utayari na utimamu. Mafunzo , ukaguzi na uthibishaji wa kwanza unafanyika kwanza katika nchi yao wanakotoka na pili yanafanyika wakisha fika katika kituo cha kazi.
Aidha akasema, katika mafunzo hayo pamoja na mkutano walioufanya, matumizi ya teknolijia za kisasa katika misheni za ulinzi yalisisitizwa sana.
Teknolojia ambazo Umoja wa Mataifa umeamua kuanza kuzitumia katika baadhi ya maeneo kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa raia na kuboresha operesheni za ulinzi ni pamoja na ndege ambazo haziendeshwi na rubani (unmanned aerial systems ).
Akifafanua zaidi kuhudu teknolijia hiyo ya kutumia ndege ambazo hazirushwi na rubani , Mkuu huyo wa UNAMID anasema matumizi ya teknolojia hiyo ni muhimu sana hasa katika ukusanyaji wa taarifa za kitelejensia, na kutambua mwenendo wa makundi ya wanamgambo wenye silaha.
“ Hii ni teknolojia muhimu sana kwanza, kwa sababu inauwezo wa kukusanya habari na pili kupiga picha ya nini kinachoendelea katika eneo fulani,na kwa kutumia zana hii itasaidi sana katika kuyadhibiti makundi yenye silaha na hivyo kuwa na uwezo wa kuwalinda wananchi dhidi ya hatari ambayo inaweza kuwakabili.
Vilevile ameeleza kwamba katika mafunzo hayo, wakuu wao wa majeshi ya kulinda amani walifundishwa umuhimu ya kuwa karibu na vyombo vya habari.
“ Tumejifunza mengi kwa kweli, likiwano hili la uhusiano wetu na vyombo vya habari, hili ni jambo ambalo pia limepewa msisitizo wa aina yake, kwamba tunapashwa, katika utekelezaji wa majukumu yetu kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari” anasema Luteni Jenerali Mella.
Awali akimtabulisha Mkuu huyo mpya wa UNAMID kwa waambata jeshi hao, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, aliomba ushirikiano kutoka kwa waambata jeshi hao na serikali zao.
Akasema ingawa nafasi hiyo amepewa mtanzania lakini wanajeshi wanaounda UNAMID wanatoka katika nchi mbalimbali zikiwamo za Afrika kwa hiyo heshma hiyo ilikuwa ni ya waafrika wote na kwamba mafanikio ya UNAMID ni mafanikio ya Afrika, ni mafanikio ya Umoja wa Mataifa na ni mafanikio ya wapenda amani na kubwa zaidi kwa amani, usalama na ustawi wa ni wananchi wa Sudan hususani jimbo la Darfur.
Lt. Jen. Paul Ignace Mella, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Lt. Jenarali Patrick Nyamvumba kutoka Rwanda ambaye amestaafu Marchi 31, 2013.
Jeshi la kulinda amani la UNAMID linahudumiwa na watu wa kada za aina mbalimbali wapatato 19,148 . Kati yao vipo vikosi vya kijeshi vyenye wanajeshi 14,055, wangalizi wa kijeshi 342 ( Military Observers), Polisi 4,721, wafanyakazi wa kimataifa 1,077 , wafanyakazi wenyeji ni 2,924 na 448 ni wafanyakazi wa kujitolea kutoka Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment