Friday, June 14, 2013

Mahojiano kati ya Freddy Macha na Mwandishi nguli Said Ahmed Mohammed



Profesa Said A Mohammed
 SEHEMU YA KWANZA

Profesa Said A Mohammed umeandika vitabu vingi. Ama kweli wewe ni hazina ya fasihi ya Kiswahili ambaye hujapata heshima inayokustahili. Najua hupendi kusifiwa – lakini lazima tukuthamini ungali hai maana wewe fahari yetu Waswahili. Hata ukiweka neno “Tanzanian Novelists”, “Zanzibar Writers”, au “Tanzanian Writers” katika Wikipedia hutajwi. Unadhani kwanini wengi  hasa Tanzania bara na visiwani hawakufahamu ipasavyo?

Mwandishi : Said A Mohammed
 Kama nilivyokueleza katika mkumbo wa masuali uliyoniuliza mwanzo hapo kitambo, Watanzania na zaidi Wazanzibari hawana utamaduni wa kusoma vitabu vya fasihi. Kwa hivyo hawajapata ari wala mwamko wa kujali na kuthamini fasihi yenyewe na waandishi wake. Kweli kuna wachache ambao wanatangazwa katika vyombo vya mawasiliano, lakini mimi simo katika orodha ya waandishi hao. Hili ni suala la vyombo vya habari ambavyo mara nyingi huwatukuza wale ambao wanataka wao watukuzwe. Vilevile kuna wasanii wanaopenda kujipeleka mbele ili wasikike na hata kuwa na fikra kwamba waandishi wengine wadidimie. Kwa bahati mbaya au labda kwa bahati nzuri, mimi si mtu wa kimbele mbele. Naamini sana maneno ya wahenga kwamba Kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza.
Katika dunia ya sasa kujipeleka mbele ili usikike bila umakinifu, ndilo jambo linaloharibu mambo mengi ikiwemo sanaa ya lugha. Vipawa vinadharauliwa na sanaa tunazokutana nazo ni sanaa zinazokuzwa tu bila ya kupitiwa kwa kina na kujadiliwa. Chambilecho, gwiji wetu wa fasihi, Profesa Ebrahim Hussein, hakuna fasihi tena kwa maana ya fasihi. Hakuna wasomaji wazingatifu. Hakuna uhakiki kwa maana ya uhakiki. Kuna fikra ya kwamba chochote kile ni sawa. Shairi, riwaya, hadithi fupi au tamthilia ikiwa ina sura ya tanzu inayohusika, basi ni fasihi tu kwa maoni ya wengi.  Fasihi haipo. Wasomaji hawapo. Umakinifu wa fasihi haupo. Uhakiki umepotea. Hata wale ambao tunawatarajia kufanya hivyo hawashughuliki na kusoma, kuandika, kuhakiki na kuzitangaza kazi za fasihi ya Kiswahili. Sisi waandishi hatuwezi kujitetea. Wanaojitetea na kuwaponda wenzao ndio katika hao wanaowekwa mstari wa mbele na wanaojitapa kuwa wanajua hata kuandika kazi za waandishi wenzi wao.   

 Kuna dhana inayodai ili mwandishi ajulikane labda aanzie uandishi wa habari, ajenge jina kihivyo kama walivyofanya baadhi ya waandishi maarufu duniani mfano: Gabriel Marquez (Colombia) , Ernest Hemingway (Marekani) au afungwe jela kama Wole Soyinka (wakati wa vita vya Biafra 1967-1970) na Ngugi Wa Thiong’o (Kenya, 1978). Hapa tunatumia neno “kujulikana” si kwa maana mbaya ya kutaka umashuhuri bali kutathmini wepesi wa wasomaji kuzijua, kuzithamini na kuzipenda kazi za mtunzi. Mathalan, Watanzania wengi wa kizazi kilichozaliwa baada ya mwaka 1970 wanamfaham marehem Elvis Musiba sana kutokana na tungo zake za mtindo wa kiupelelezi kuliko  marehem Said Muhammed  Said Abdulla aliyemtangulia kwa mtindo huo huo.

Mwandishi Said A Mohammed:
Suala halina ukweli kamili. Kuna mamilioni ya waandishi ambao hawajui hata maana ya uandishi habari na wengi katika hao ni waandishi wazuri wanaosifika na wako wazuri ambao hawajasifika kwa sababu hawajapewa nafasi ya kutangazwa katika vyombo vya habari. Nao hawapendi kujitokeza kifua mbele kwa kulazimisha kazi zao kuwa nzuri.

 Tukiendelea na mada hii hii. Waandishi wa vizazi mbalimbali wamefahamika kwa njia tofauti. Linganisha waandishi wa kizazi cha ukoloni na miaka michache baada ya ukoloni, mfano Mathias Mnyampala, Shaaban Robert, Muhammed Said Abdullah, Saadan Kandoro, Faraji Katalambula, nk-  waliothaminiwa kwa kazi zao. Vitabu vyao viliuzwa madukani na hapo hapo kutumika mashuleni. Linganisha awamu hiyo na ile ya miaka ya 1970 kuendelea: Mohammed S. Mohammed, Adam Shafi, Euphrase Kezilahabi, Ebrahim Hussein nk, waliojiingiza ama katika mashindano kwanza (Mohammed Suleiman na “Kiu” -1970), Adam Shafi (tuzo la Uandishi Bora1998) au kupitia sanaa za maonyesho (Ebrahim Hussein). Kuanzia hapo mambo yalibadilika kabisa - waandishi wa vizazi vya miaka 1980 kuendelea walijenga majina  kwa kujitangaza wenyewe kwa kutumia vyombo vya habari, makampuni waliyounda. Akina Kajubi Mukajanga, Hammie Rajab, marehem Ben Mtobwa, na mwandishi anayesomwa sana na vijana sasa hivi – E Shigongo – ambaye amewahi kuchapisha vitabu  India-na shirika lake la habari na blog- Global Publishers. Hawa waliamua kuingia mitaani.
 
Mwandishi Said Ahmed Mohammed:
 Kweli wakati au enzi ya wakati fulani na mambo yake yanaathiri sio tu fasihi, bali thamani ya fasihi, maudhui yake, fani yake, waandishi wake na kadhalika. Kwa maoni yangu wakati huu tulionao ni wakati wa upujufu mkubwa hasa katika dunia ya tatu. Wasomi hawana tena msimamo seuze watu wa kawaida. Pesa inatawala, tena inatakikana ipatikane bila ya kutoa jasho. Kila kitu kinauzwa na watu hawajui kuchagua au kutathmini vitu vyenye hadhi au pengine wanajua lakini hawana pesa za kununua vitu vyenye hadhi. Kwa hivyo tunaambukizana upotofu wa mambo na hatimaye hatutambui tunafanya nini. Kujijengea kampuni na kuuza vitabu vyake mtu ni jambo linawezekana na kwa kweli tunaliona, lakini mimi nadhani hakuna vipimo vizuri vya mtu anayefanya hivyo. Yeye mwenyewe aandike, tena avipitie mwenyewe, avihariri mwenyewe, atambue uzuri na ubaya wa kazi zake yeye mwenyewe na baadaye afyatue vitabu kama matofali, basi wanaonunua vitabu vyake lazima wawe na mushikeli. Kujitangaza na hata kutangazwa kwa maana ya kukuzwa tu na watu fulani hakuna maana ya kwamba hakuna wengineo wanaoandika, tena wanaoandika ambao wana vipawa vikubwa zaidi. Kuepuka utunzi wa kuuza badala ya kujiuza ndiko kunakopelekea fasihi ya Kiswahili idharauliwe na ipuuzwe duniani.

Je tunaweza kusema wewe kama mwandishi uliyeamkia miaka ya mwisho ya  Sabini, ulitegemea tu vitabu vyako kuingia madukani na kusomwa bila kuingia madukani kama Shigongo na Ben Mtobwa – Mungu amrehemu - waliouza vitabu kama miwa, miswaki, nyama choma na nyanya?

Mwandishi Said A Mohammed:
  Ndiyo, mimi niliandika na mpaka sasa naandika kwa kutegemea vitabu vyangu kuuzwa madukani, sababu ni kwamba sitaki vitabu vyangu niviuze kama miwa, miswaki, nyama choma na nyanya. Lengo langu sio pesa, bali ukweli na umahiri wa kuandika ingawa hata na mimi nathamini na nazitaka pesa kama wenzangu. 

Halafu kuna suala tulilozungumzia mwaka jana la kupitisha vitabu mashuleni kwanza ndipo visomwe au kuuzwa. Hapa tunaangalia pia tatizo linalowakumba wachapishaji na soko zima la vitabu vya Kiswahili. Wewe mwenyewe umeandika vitabu vingi katika medani hii...

Mwandishi Said A Mohammed:
Ingawa mimi nimeandika vitabu vingi mpaka sasa, vichache tu ndivyo vilivyopata nafasi kuingia mashuleni. Na hivyo vilivyoteuliwa kuingia shule vilisomwa mwanzo kabla ya kusomwa kwa madhumuni ya elimu shuleni.

Upo  usemi ulioenea kwamba waandishi wa Kiswahili toka enzi za ustaadh Shaaban Robert mwenyewe hadi leo hawawezi kuuza kazi zao duniani kama wasipoandika lugha za Kizungu. Hapa tutoe mifano ya William Mkufya (Wicked Walk), Ismail Mbise (Blood On Our Land), M G Vassanji na  Abdul Razak Gurnah.  Profesa Gurnah na Vassanji (ambao wamehama Afrika Mashariki miaka mingi sana) wameshashinda tuzo kibao za kimataifa kutokana na kuandika Kiingereza. Je ndiyo suluhisho? Mbona Watanzania na wasomaji wa Kiswahili hawawafahamu hawa wawili (Vassanji na Gurnah) hasa nao wamechangia sana kujenga fasihi ya Kiafrika muda mrefu?
 
Mwandishi Said A Mohammed:
Mimi ni mmojawapo ambaye ninaamini kuandika kwa lugha apendayo na kwa mtindo auchaguao ni haki ya mwandishi. Sababu za kuchagua lugha inakamatana na mtu kuandikia watu gani au kwa sababu gani. Wengine wanaandika kwa fahari ya lugha yao, utamaduni wao na uelevu wa watu wao ambao wangeweza kuisoma kazi husika na kuitafakari. Wengine wanaandika kwa lugha ya kigeni kwa sababu wanadhani kuwa lugha ya kigeni ina mvuto mkubwa kwa kazi ya fasihi, tena lugha ka ya Kiingereza husifiwa na kutoa hadhi kubwa kwa waandishi. Mimi nimo katika kundi la mwanzo, yaani kuandika kwa maana ya kukitukuza Kiswahili, fasihi na utamaduni wake. Pia kuwapa fursa wananchi walio wengi na ambao hawakijui Kiingereza lakini wana nafasi ya kufurahi sanaa yao lugha yao na kubwia fikra za raia wenzao ambao ni waandishi. Zaidi ya hayo, si kweli kwamba wanaoandika kwa Kiingereza wanathaminiwa au wanapata pesa nyingi. Inatia moyo kwamba duniani fasihi haiandikwi kwa Kingereza tu, bali Kichina, Kirusi, Kijerumani, Kifaransa, Kiholanzi n.k



No comments: