Monday, June 3, 2013

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, JAJI JOSEPH S. WARIOBA, KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UZINDUZI WA RASIMU YA KATIBA LEO TAREHE 03 JUNI, 2013 KWENYE VIWANJA VYA UKUMBI WA KARIMJEE,

DAR ES SALAAM.
 Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilali – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano,
 Mhe. Mizengo K. P. Pinda (Mb.) - Waziri Mkuu,
 Mhe. Seif Sharif Hamad – Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
 Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (Mb.) - Makamo wa Pili wa Rais - Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
 Mhe. Mathias Chikawe – Waziri wa Katiba na Sheria,
 Mhe. Abubakar Khamis Bakary - Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
 Mhe. Jaji Frederick M Werema - Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
 Mhe. Othman Masoud Othuman - Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
 Viongozi wa Vyama vya Siasa,
 Waheshimiwa Wajumbe wa Tume na Wajumbe wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
 Ndugu Wananchi,
 Wageni Waalikuwa
 Waandishi wa Habari Mabibi na Mabwana.
1.0. UTANGULIZI
Ndugu Wananchi,
2
Awali ya yote namshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya leo ya kuzindua Rasimu ya Katiba. pia, niwashukuru ninyi nyote mliohudhuria halfa hii ikiwa ni mwendelezo wa mchakato muhimu wa Mabadiliko ya Katiba ya nchi yetu.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilipitishwa Bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa mabadiliko Februari, 2012. Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu wa Kifungu 6(1) cha sheria hiyo (Cap.83). Wajumbe 34 wa Tume waliteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mwezi Aprili, 2012. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume imepewa miezi kumi na minane kukamilisha kazi yake kuanzia siku ilipoanza kazi rasmi ambayo ilikuwa Mei 2, 2012.
Tume iliandaa ratiba ya utekelezaji wa majukumu yake. Kufuatana na ratiba hiyo Tume ilijipanga kukusanya maoni ya wananchi katika kipindi cha miezi mitano kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2012. Kazi hiyo ilifanywa kama tulivyopanga. Tume ilijigawa katika makundi na ilitembelea mkoa yote thelathini.
Tume ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi wapatao 1,365,337 ambao kati ya hao wananchi 333,537 walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au kwa maandishi. Tume pia ilipata maoni ya wananchi wengi, wa ndani na nje ya nchi kwa njia mbali mbali kama vile; Mikutano ya hadhara, Fomu maalum za Tume, barua kupitia Masanduku ya Barua ya Tume, Mitandao ya Kijamii ya barua pepe; facebook ya Tume, Tovuti ya Tume; Makala mbalimbali kutoka kwenye magazeti na ujumbe mfupi wa simu.
Tume ilitumia mwezi Januari, 2013 kukusanya maoni ya makundi mbali mbali katika jamii, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi za Serikali, taasisi za dini, wakulima, wafugaji, wafanyakazi, asasi za kiraia na kadhalika. Makundi zaidi ya 160 yalikutana na Tume na kutoa maoni. Tume pia ilipata maoni ya viongozi wa juu wa Serikali walioko madarakani na waliostaafu. Kwa jumla viongozi 43walitoa maoni.
3
Tume ilipanga kutumia miezi mitatu ya Februari, Machi na Aprili kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba. Lakini tuligundua kwamba maoni tuliyopata yalikuwa mengi sana, na pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa, tulitambua umuhimu wa kuongeza muda hadi mwisho wa mwezi Mei, Maoni ya wananchi yaligusa mambo yote yanayohusu Katiba na mengi ya maoni hayo yalikinzana. Aidha, baadhi ya maoni yaligusia masuala ya Kisera, Kisheria na Kiutendaji. Tulifanya uchambuzi makini na wa ndani wa maoni hayo na kazi hiyo tumeikamilisha na rasimu imeandaliwa na Tume na leo tupo hapa kwa ajili ya kuizindua, ambapo Wananchi watapata nafasi ya kuisoma. Kwa leo, kwa niaba ya Tume, napenda kutaja maeneo machache tu ambayo tunayapendekeza.
2.0. IBARA ZINAZOPENDEKEZWA KWENYE RASIMU YA KATIBA
Ndugu Wananchi,
Katiba yetu ya sasa ina ibara 152. Tume ilifanya jitihada kubwa sana kuandaa rasimu ambayo siyo ndefu. Lakini katika hali halisi haikuwezekana. Rasimu ya Katiba tunayopendekeza ina ibara 240.
3.0. MISINGI MIKUU YA TAIFA
Utangulizi wa Katiba ya sasa ndio unaobeba misingi mikuu ya Taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Tume inaamini kwamba misingi hii ni mizito na inastahili kubaki kwenye Katiba mpya. Hata hivyo, Tume imeona ni busara kuongeza misingi mingine mitatu ya Usawa, Umoja na Mshikamano. Hivyo, Tume imependekeza Katiba iwe na Misingi Mikuu saba ya Taifa;yaani; Uhuru, Haki, Udugu, Usawa, Umoja, Amani na Mshikamano.
4.0. TUNU ZA TAIFA
Katiba yetu ya sasa haina sehemu inayoelezea tunu za Taifa (National Values). Wananchi wengi walitoa maoni kwamba Katiba itaje Tunu za Taifa. Tume imependekeza Tunu zifuatazo zitajwe ndani ya Katiba. Tunu hizo ni;- Utu,
4
Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.
5.0. MALENGO YA TAIFA
Tume ilipozunguka nchi nzima wananchi walizungumzia sana kuhusu malengo ya taifa. Walitaka Katiba ionyeshe dira ya taifa. Wananchi wanayo ndoto yao ya Tanzania ya kesho na kesho kutwa. Kwa kuzingatia maoni ya wananchi, kuna sura nzima inayohusu Malengo mahsusi na ya msingi ya mwelekeo wa shughuli za Kiserikali na Sera za Kitaifa. Rasimu ya Katiba inaeleza kuwa Malengo ya Kitaifa yaliyoainishwa ndani ya Rasimu yatakuwa ni Mwongozo kwa Serikali, Bunge, Mahakama, Vyama vya Siasa, Taasisi na Mamlaka nyingine, na kwa kila mwananchi katika matumizi au kutafsiri Masharti ya Katiba au Sheria nyingine za Nchi.
Kwa msingi huo, Tume imependekeza malengo makuu ya taifa yapanuliwe kwa mpangilio wa kuonesha malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kimazingira na sera ya mambo ya nje. Malengo hayo yameingizwa kwenye Rasimu ya Katiba.
6.0. VYOMBO VYA KIKATIBA
Wananchi walizungumzia suala la kubainishwa kwa vyombo vya Kikatiba na kuingizwa kwenye Katiba ili viwe na nguvu ya Kikatiba katika utekelezaji wa majukumu yao. Tume imependekeza baadhi ya vyombo vifuatavyo viwe vya Kikatiba; Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali, Baraza la Mawaziri, Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri; Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
5
7.0. MAADILI YA VIONGOZI NA MIIKO YA UONGOZI
Wananchi wengi pia walizungumzia kwa upana sana kuhusu maadili na miiko ya Viongozi, kwa kuzingatia maoni ya wananchi Tume inapendekeza maadili ya viongozi wa umma, pamoja na miiko ya uongozi yawekwe kwenye Katiba. Tume pia imependekeza kuwa Sekretariati ya Maadili ibadilishwe kuwa Tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wanaovunja miiko ya uongozi.
8.0. HAKI ZA BINADAMU
Kuhusu haki za binadamu wananchi walitaka haki hizi ziimarishwe na kusiwe na vikwazo visivyo vya lazima. Tume imependekeza mabadiliko katika baadhi ya haki za binadamu kwa madhumuni ya kuziimarisha. Moja ya mabadiliko hayo ni kuhusu uhuru wa mwananchi kushiriki shughuli za umma. Tume inapendekeza kwamba vikwazo vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.
Tume pia, inapendekeza haki mpya ziingizwe kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi, , haki ya mtoto, haki za Watu wenye Ulemavu, Haki za Wanawake, Haki za Wazee, Haki za Makundi Madogo katika Jamii, Haki ya Elimu na Kujifunza, Haki ya kupata habari, Haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari na kadhalika.
9.0. URAIA
Wananchi wengi walipendekeza kuwa suala la Uraia libainishwe wazi kwenye Katiba. Tume imependekeza kwa kutaja Raia wa Jamhuri ya Muungano na haki zake.
10.0. MIKOPO NA DENI LA TAIFA
Ndugu Wananchi,
Wananchi walizungumzia suala la uwepo wa Ukomo wa nchi kukopa na uwepo wa utaratibu wa kulipa Deni la Taifa ili kuilinda Nchi isiwe na deni kubwa. Kwa kuzingatia
6
maoni ya Wananchi, Tume imependekeza kuwa, Serikali itawajibika kutoa taarifa Bungeni kuhusu Mikopo kwa kuainisha kiasi cha deni lililopo, riba yake na matumizi ya fedha za Mikopo na utaratibu wa kulipa Madeni ya Taifa.
11.0. MFUMO WA UTAWALA
Kuhusu utawala, Tume inapendekeza Tanzania iendelee na mfumo wa Jamhuri kwa maana ya nchi inayoongozwa na Rais Mtendaji ambaye ni Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
12.0. UCHAGUZI WA RAIS
12.1. Umri wa kugombea Urais
Tume ilipokea maoni yanayokinzana kuhusu umri wa mwananchi kugombea Urais. Baadhi walipendekeza mtu akishakuwa na sifa ya kupiga kura awe pia na sifa ya kugombea Urais. Umri wa mtu kuruhusiwa kupiga kura ni miaka 18. Wengine walipendekeza umri uliopo kwenye Katiba wa mtu kugombea Urais, yaani kuanzia miaka 40 na kuendelea, uendelee kubaki kama ulivyo.
Wengine walisema Umri wa mtu kuruhusiwa kugombea Urais uwe miaka 35 au miaka 50 na kuendelea.
Tume imeyachambua maoni yote hayo, ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za Nchi zingine na uhalisia wa watu wanaogombea na kuchaguliwa kuwa Marais katika Nchi mbalimbali Duniani ambazo zingine zimeruhusu wagombea wa nafasi ya Urais kuwa na umri chini ya miaka 40.
Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo walikuwa na umri wa miaka 40 au zaidi.
Kwa kuzingatia maoni ya wananchi, utafiti na hali halisi, Tume inapendekeza Rais aendelea kuchaguliwa na wananchi na pamoja na sifa nyingine, mtu anayeomba urais asiwe chini ya miaka 40.
7
Uchaguzi wa Rais itakuwa kama ilivyo sasa, yaani mgombea Urais atakuwa na mgombea mwenza kwa utaratibu kama ilivyo sasa. Isipokuwa, Tume imependekeza Mgombea Urais anaweza kupendekezwa na Chama cha Siasa au kuwa Mgombea Huru.
Mgombea wa nafasi ya Rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa.
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa Mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza kufungua kesi. Wanaoweza kufungua kesi ni wagombea Urais. Aidha, ni Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na Mamlaka na uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe ndani ya mwezi mmoja, yaani siku therathini.
Rais aliyeshinda ataapishwa siku thelathini tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na Mahakama.
13.0. MADARAKA YA RAIS
Ndugu Wananchi,
Tume inapendekeza kwamba, Rais abaki na madaraka ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu. Hata hivyo inapendekezwa Rais ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi. Kwa mfano:
Uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri, Rais atateua na Bunge litathibitisha.
Kuhusu Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu Rais atawateua kutokana na majina ya watu waliopendekezwa na Tume ya Uutumishi wa Mahakama na baada ya hapo Bunge litathibitisha.
Kuhusu Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama inapendekezwa kianzishwe chombo kipya kitakachoitwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, ambalo kati ya
8
majukumu yake itakuwa ni kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kuhusu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma.
14.0. KINGA YA RAIS
Tume baada ya kupitia maoni ya Wananchi, inapendekeza Rais abaki na kinga kama ilivyo sasa na anaweza kushitakiwa na Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.
15.0. IDADI YA MAWAZIRI
Inapendekezwa Rais aunde Serikali ndogo iliyo na Mawaziri wasiozidi kumi na tano na mawaziri hao wasiwe wabunge. Mawaziri hawatahudhuria vikao vya Bunge isipokuwa kama watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge.
16.0. BUNGE
Ndugu Wananchi,
Kuhusu Bunge kutakuwa na wabunge wa aina mbili. Kutakuwa na Wabunge wa kuchaguliwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha Watu wenye Ulemavu.
Kila Jimbo la Uchaguzi litakuwa na Wabunge Wawili mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.
Tume inapendekeza kwamba, Mbunge akifukuzwa na Chama cha Siasa abaki kuwa Mbunge lakini akihama Chama atapoteza Ubunge wake.
Inapendekezwa ukomo wa Ubunge uwe vipindi vitatu vya miaka mitano mitano. Hata hivyo, wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kabla ya mwisho wa kipindi chake.
Inapendekezwa pia kusiwepo na uchaguzi mdogo isipokuwa kama nafasi inayokuwa wazi inatokana na Mbunge huru ndipo utafanyika uchaguzi mdogo kujaza
9
nafasi hiyo, lakini kama nafasi ikiwa wazi kutokana na Mbunge wa Chama cha Siasa basi nafasi hiyo, ijazwe na mtu kutoka Chama hicho.
Inapendekezwa Spika na Naibu Spika wasitokane na Wabunge na wasiwe Viongozi wa vyama vya Siasa.
17.0. TUME YA UCHAGUZI
Tume imefanya uchambuzi wa maoni ya wananchi kuhusu Tume ya Uchaguzi. Tume inapendekeza jina la tume liwe Tume Huru ya Uchaguzi. Tume pia inapendekeza sifa za wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi ziwekwe kwenye Katiba. Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watapatikana kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya Katiba kwa kuomba. Majina ya waombaji yatachambuliwa na Kamati ya Uteuzi ambayo Mwenyekiti wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni Majaji Wakuu wa nchi Washirika, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Maspika wa Mabunge wa nchi Washirika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu.
Kamati ya uteuzi itapendekeza majina ya watu wanaofaa kwa Rais ambaye atateua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wengine. Bunge litathibitisha uteuzi wao. Wabunge na viongozi wa aina hiyo hawatakuwa na sifa za kuwa wajumbe wa tume ya uchaguzi.
Inapendekezwa Tume huru ya Uchaguzi isimamie masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na Usajili wa Vyama vya Siasa.
18.0. MAHAKAMA
Kuhusu Mahakama inapendekezwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) Majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
19.0. MUUNDO WA MUUNGANO
10
Ndugu Wananchi,
Suala la muundo wa Muungano ndilo lililokuwa gumu kuliko masuala yote. Tume ilitumia muda mwingi kuchambua maoni ya wananchi. Pamoja na kwamba hadidu za rejea zilielekeza Tume kuzingatia uwepo wa Muungano, baadhi ya wananchi walitoa maoni kwamba Muungano uvunjwe na Tume iliyapokea maoni hayo. Licha ya kwamba waliotaka kuvunjwa muungano walikuwa wachache sana, Tume ilichambua sababu walizotoa na kuridhika kwamba hazikuwa na uzito.
Wananchi walio wengi walitaka Muungano uendelee. Kati yao wapo waliopendekeza Muungano wa Serikali moja, Serikali mbili, Serikali tatu, Serikali nne na muungano wa mkataba. Sababu za wale waliopendekeza Serikali nne hazikuwa na uzito, kwa hiyo Tume ikaamua kutopendekeza muundo huo.
Wananchi waliopendekeza Serikali moja walikuwa wachache lakini sababu zao zilkuwa na uzito. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia hali halisi iliona ni changamoto kubwa kuwa na Muungano wa Serikali Moja
Wananchi waliopendekeza Muungano wa Mkataba walikuwa wengi (hasa wananchi wa Zanzibar) na sababu zao zilikuwa na uzito. Lakini uchambuzi wa Tume ilionekana wazi kwamba ili kupata mkataba lazima kwanza kuwe na nchi mbili huru kabisa lakini hakukuwa na mazingira ya uhakika ya kupata mkataba wa muungano. Tume iliona kuna changamoto ya muungano kuvunjika ingawa waliotoa maoni walisisitiza muungano ubaki. Hivyo, Tume iliamua kutopendekeza muundo huo.
Wananchi waliopendekeza Tanzania iendelee na Muundo wa sasa wa Serikali mbili walikuwa wengi na sababu zao zilikuwa nzito. Hata hivyo, wananchi katika kundi hili walipendekeza mabadiliko mengi na makubwa. Tathmini ya Tume ilionyesha kwamba isingewezekana kufanya mabadiliko yote yaliyopendekezwa.
Wananchi waliopendekeza muundo wa Serikali tatu walikuwa wengi kuliko makundi yote. Sababu zao zilikuwa nzito lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi na nzito. Pamoja na maoni ya wananchi Tume ilirejea sababu za kupendekeza muundo huu zilizotolewa na Tume zilizopita na Tafiti zilizofanywa na Tume kuhusu aina mbalimbali
11
za Muungano. Baada ya yote hayo Tume ilifikia uamuzi wa kupendekeza mfumo wa Serikali tatu. Yaani Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
20.0. ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO
Ndugu Wananchi,
Tume imependekeza katika Rasimu ya Katiba kuwa orodha ya Mambo ya Muungano yawe 7 badala ya 22 yaliyopo sasa.
Mambo ya muungano yanayopendekwa ni:
1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
2. Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
3. Uraia na Uhamiaji
4. Sarafu na Benki Kuu
5. Mambo ya Nje
6. Usajili wa Vyama vya Siasa
7. Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
21.0. BENKI KUU
Kwa kuwa Tume imependekeza Muungano wa Shirikisho kutokana na uzito wa maoni ya wananchi. Hivyokutakuwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa na wajibu wa kusimamia masuala ya Sarafu na Fedha za Kigeni na Benki za Washirika wa Muungano.
12
22.0. BENKI ZA SERIKALI ZA WASHIRIKA
Kutokana na pendekezo la kuwepo kwa Serikali ya Shirikisho la Nchi tatu, inapendekezwa kuwepo kwa Benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za Serikali za kila Mshirika wa Muungano na kuzisimamia benki za biashara katika mamlaka zao.
23.0. BAADHI YA MAMBO AMBAYO HAYAMO KWENYE RASIMU YA KATIBA
23.1. Serikali ya Majimbo
Ndugu Wananchi,
Tume ilipokea maoni kuhusu mambo mengine muhimu ambayo hayamo katika rasimu hii. Moja ya mambo hayo ni Serikali za Majimbo. Tume ilichambua maoni na sababu za wananchi kupendekeza Serikali za Majimbo lakini Tume ilibaini changamoto nyingi na ikaamua kutopendekeza muundo huu.
Kwanza, baada ya kuamua kupendekeza Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu, ilionekana ni dhahiri kuongeza ngazi nyingine ya Serikali ingeleta gharama kubwa. Serikali nyingine kumi zingekuwa na Wakuu wa Majimbo, Mabaraza ya Mawaziri na Mabunge na gharama yake ingekuwa kubwa.
Pili, katika kutembelea nchi Tume ilishuhudia dalili za wazi za mivutano ya Udini, ukanda,malalamiko ya upendeleo wa baadhi ya maeneo na ukabila. Dalili zilikuwa wazi kwamba utawala wa majimbo ungeirudisha nchi kwenye utawala utakaoigawa nchi kwa misingi ya ukabila, udini na ukanda na kuzigawa rasilimali za taifa kikanda na hivyo kuleta tofauti kubwa ya kimaendeleo katika nchi.
23.2. Mahakama ya Kadhi
Ndugu wananchi,
Jambo la pili ni mahakama ya kadhi. Tume ilipokea maoni mengi kuhusu suala hili. Baadhi ya wananchi walitaka mahakama ya kadhi iingizwe kwenye Katiba na
13
wengine walipinga. Baada ya kuamua kuwa Muundo wa Muungano uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona kuwa Mahakama ya Kadhi siyo suala la Muungano na imeliacha ili lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
Hata hivyo ilionekana kuwa suala siyo kuwapo au kutokuwapo kwa mahakama ya kadhi. Mahakama hizo zinaweza kuwapo bila ya kuwa katika Katiba. Zanzibar kuna mahakama ya kadhi bila kuingizwa kwenye Katiba ya Zanzibar. Kwa kutumia uzoefu huo hata Tanzania Bara inaweza kupata ufumbuzi wa suala hili.
23.3. Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
Jambo la Tatu ni Kuwepo au kutokuwepo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Baadhi ya Wananchi walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasiwepo, wengine walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kuwepo lakini wachaguliwe na wananchi na waengine wakasema wawepo na waendelee kuteuliwa na Rais kama ilivyo sasa. Tume ilitafakari kuhusu suala hili na kuamua kwamba siyo suala la Muungano na kwa kuwa Muundo wa Muungano imependekezwa uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona suala la uwepo au kutokuwepo na namna ya upatikanaji wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
23.4. Serikali za Mitaa
Kuhusu Serikali za Mitaa, Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi kuhusu kuziimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzipatia uhuru kamili wa kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa na Serikali Kuu. Tume ilitafakari suala hili na kuamua kwamba siyo jambo la Muungano na hivyo, litashughulikiwa kwenye Katiba za Washirika wa Muungano.
23.5. Uraia wa Nchi mbili
Ndugu Wananchi,
14
Jambo la tatu ni Uraia wa Nchi mbili. Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu kuwekwa kwenye Katiba suala la Uraia wa nchi mbili. Baada ya kufanya uchambuzi kwa kutengenisha mambo yapi ni ya Kikatiba na yapi yanaweza kutekelezwa bila kuingizwa kwenye Katiba bali kwenye Sheria inayohusu jambo husika, Tume imependekeza kuwa suala la Uraia wa nchi mbili linaweza kuwekwa kwenye Sheria badala ya kuwekwa kwenye Katiba. hii ni kwa sababu kutokana na utafiti uliofanywa na Tume, suala hilo linaweza kubadilika wakati wowote na hivyo likiwa kwenye Katiba linaweza kuifanya Katiba kubadilishwa mara kwa mara.
24.0. MWISHO
Naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Tume kuwashukuru Watanzania wote kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, kuanzia hatua ya kutoa maoni na kuwachagua wawakilishi wenu watakaopata fursa ya kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba. Ushirikiano huu ulikuwa muhimu sana kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hasa ukizingatia kuwa lengo ni kupata Katiba Mpya ambayo itaakisi ndoto na matakwa ya Wananchi wa Tanzania.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar:
1. Kwa kuipatia vifaa afisi na mahitaji ya lazima
2. Kwa kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu,
3. Kwa kutokuingilia Uhuru wa Tume wakati wa Utekelezaji wa Majukumu yake na
4. Kutoa Wataalam wenye Weledi, Mahiri, Makini na Waadilifu ambao wameunda Sekretarieti ya Tume.
Ndugu Wananchi,
15
Shukrani za pekee ziwaendee:
1. Wakuu wa Mikoa,
2. Wakuu wa Wilaya,
3. Wakurugenzi / Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
4. Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya,
5. Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa na Masheha.
Kwa kuisaidia Tume kutekeleza Majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, tunazishukuru Asasi za Kiraia, Taasisi, Jumuiya za Kidini, Vyama vya Siasa na Makundi mbalimbali kwa namna walivyoshiriki katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika kutoa maoni.
Mwisho ingawa siyo kwa umuhimu, Tunawashukuru Wanahabari wote kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuisaidia Tume kufikisha taarifa mbalimbali za Tume kwa Wananchi na katika kuhamasisha Wananchi kushiriki katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Nachukua nafasi hii kuwaomba Wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye Malengo yanyofanana kushiriki vyema, kwa umakini, utulivu na kwa amani katika hatua hii ya kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba.
Tume imekuwa ikithamini na itandelea kuthamini mawazo na maoni kutoka kwa Watanzania wote.
Rasimu ya Katiba itapatikana kwenye tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya www.katiba.go.tz
SASA NAKUOMBA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS UIZINDUE RASMI RASIMU YA KATIBA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
TOA MAONI TUPATE KATIBA MPYA

No comments: