Wednesday, May 1, 2013

SHEREHE ZA MIAKA 49 YA MUUNGANO ZAFANA MUSCAT, OMAN

Ubalozi wa Tanzania mjini Muscat, Oman chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Balozi Ali Ahmed Saleh, uliandaa sherehe iliyofana sana ya kuadhimisha miaka 49 ya Muungano. Sherehe hii ilifanyika katika ukumbi wa Jibrin kwenye hotel ya kitalii ya Intercontinental Muscat. 
 Mgeni rasmi katika sherehe hii alikuwa Mheshimiwa Ahmed bin Mohamed bin Salim Al Futaisi, Waziri wa wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Oman aliyeongoza ujumbe mzito wa Serikali ya Oman ambao ulijumuisha Mheshimiwa Mohamed bin Yousuf Al Zarafi, Naibu Katibu Mkuu , Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman, Mheshimiwa Khalil bin Abdullah Al Khonji, Mwenyekiti wa chama cha wafanya biashara na wenye viwanda wa Oman pamoja na wabunge Wabunge la Oman pamoja na wakuu wa Idara na maafisa waandamizi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman. 
 Sherehe hii pia ilihudhuriwa na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Oman , wananchi wa Oman , wafanyabiashara , watanzania waishio Oman , pamoja na waomani wenye asili ya Tanzania Katika hotuba yake Mheshimiwa Balozi Ali Ahmed Saleh alisifu juhudi za serikali za Tanzania na Oman katika kukuza uhusiano baina ya nchi mbili ambo ni wa kihistoria na unazidi kuimarika kadri siku zinavyoenda. Alieleza kuwa ziara ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyoifanya nchini Oman mwezi oktoba 2012 imeongeza kasi mpya katika Uhusiano wa Tanzania na Oman.
Katika ziara hii mikataba kadhaa ilisainiwa ikiwa ni hatua ya kuboresha mazingira ya kisheria katika Uhusiano wa Tanzania na Oman, mikataba hii ni Mkataba wa kulinda na kuendeleza vitega uchumi , mkataba wa ushirikiano katika masuala ya kumbukumbu na nyaraka, Mkataba wa ushirikiano wa katika Elimu ya Juu kati ya Oman na Zanzibar, mkataba wa kuunda baraza la pamoja la biashara kati ya Tanzania na Oman.. 
 Mheshimiwa Balozi alieleza pia kuwa ziara ya waziri wa Elimu ya Juu wa Oman Mhe. Rawiyah Al Busaidi nchini Tanzania na uzinduzi wa mfuko wa uzamini wa masomo ya Elimu ya shahada za juu, kufanyika kwa kikao cha kwanza cha tume ya pamoja ya ushirikiano baina ya Oman na Tanzania na kusainiwa kwa mkataba wa maridhiano kuhusu mashauriano ya kisiasa baina ya Tanzania na Oman kuwa ni mambo yanayozidi kuimarisha na kuboresha uhusiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Oman. 
 Sherehe hizi zilizofana sana zilipambwa na Kikundi cha Taifa cha sanaa kutoka Zanzibar ambacho kilitumbuiza kwa ngoma za kutoka sehemu mbalimbali Tanzania bila kusahau ngoma maarufu ya Msewe ambayo ilikuwa kivutio kikubwa kwa wageni waalikwa . Mheshimiwa Balozi na mgeni Rasmi walikata keki ikiwa ni ishara kuitakia mema Tanzania na Oman.
 Balozi wa Tanzania nchini Oman Mhe Ali Ahmed Saleh akipozi na kikundi cha utamaduni kilichotumbuiza katika siku hii adhimu

Balozi Ali Ahmed saleh akikata keki na mgeni rasmi katika sherehe hii Mheshimiwa Ahmed bin Mohamed bin Salim Al Futaisi, Waziri  wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Oman 
 Ngoma ya utamaduni toka Zanzibar
 Balozi Ali Ahmed Saleh akisoma hotuba yake
 Hotuba
 Balozi akiwa na maofisa wa Ubalozi Muscat
 Balozi Ali Ahmed Saleh akihutubia
 Ngoma ya msewe toka Zanzibar ilitia fora
 Wageni wakisikiliza hotuba

No comments: