Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, alipofika ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, alipofika ofisini kwake Migombani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Fatma Abdulhabib Ferej, akizungumza na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, alipofika ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amevitaka vyombo vya ulinzi nchini kusimamia vyema majukumu yake ili kuhakikisha kuwa bahari na mipaka ya nchi inakuwa salama.
Amesema Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa, inakabiliwa na changamoto moto nyingi za kiulinzi na usalama kuhakikisha kuwa magaidi hawaingii nchini, sambamba na kukabiliana na vitendo vya uharamia na usafirishaji wa dawa za kulevya. Maalim Seif ameeleza hayo ofisini kwake Migombani alipokuwa na mazungumzo na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman.
Amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa ni tishio la vitendo vya kigaidi katika Pembe ya Afrika, jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa ili vitendo hivyo visije kuiathiri Zanzibar. “Suala la ulinzi halina mbadala, kitu cha msingi ni kwa vyombo vya ulinzi na dola kushirikiana kuhakikisha kuwa nchi iko salama kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla”, alisisitiza Maalim Seif.
Kuhusu vitendo vya uharamia vinavyofanywa katika bahari ya hindi, Maalim Seif amesema vinaathiri shughuli za kibiashara na uchumi na vinastahiki kupigwa vita kwa nguvu zote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, amesema suala la ulinzi ndio jukumu la msingi kwa vyombo vya ulinzi, na kuahidi kushirikiana na vyombo vya dola na wananchi katika kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi zaidi. Jererali Othman ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Zanzibar, amesifu mashirikiano anayoyapata kutoka kwa viongozi wa nchi na watendaji wengine katika kufanikisha jukumu hilo la kiulinzi.
Jererali Othman pia amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji na kubadilishana mawazo juu ya majumu ya ofisi hiyo.
Waziri Fereji amesema katika kukabiliana na majukumu ya ofisi hiyo, wanahitaji mashirikiano ya karibu na vyombo vya ulinzi katika kukabiliana na na vitendo viovu vikiwemo udhalilishaji wa watu wenye ulemavu, uchafuzi wa mazingira na matumizi ya dawa za kulevya.
Amevishauri vyombo vya ulinzi kujiimarisha zaidi ili kuweza kukabiliana na makundi ya kihalifu yakiwemo yale yanayojihusisha na uchimbaji wa mchanga kinyume na utaratibu.
“Ukweli ni aibu kusema kuwa jeshi la polisi linashindwa kuwakamata wachimbaji wa mchanga kwa sababu wana pamanga na marungu au mawe, wakija wakiamua kuingia barabarani je mutawafanyaje?”, alihoji Waziri Fereji.
Kuhusu UKIMWI, Waziri Fereji amesema licha ya kuwa kiwango cha maambukizi bado ni chini ya asilimia moja, lakini athari kubwa inajitokeza kwa makundi hatarishi likiwemo lile linalojihusisha na biashara haramu ya ukahaba.
No comments:
Post a Comment