Injinia Mbogo Futakamba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Usalama wa Chakula na UShirika akizungumza wakati wa Kikao cha Tatu cha Kazi kilichokuwa kikijadili kuhusu maeneo mapya takayoweza kuingizwa katika Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu ( SDGs). Naibu Katibu Mkuu aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao hicho kilichomalizika mwishoni mwa wiki hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York.Tanzania ni kati ya Nchi 30 zilizochaguliwa kushiriki majadiliano hayo. Maeneo ambayo yalijadiliwa katika Kikao hicho ni ; upatikanaji wa chakula na lishe bora, kilimo endelevu, mmomonyoko wa udongo, ukame na kuongezeka kwa jangwa, upatikanaji wa maji na ushughulikiaji wa maji taka.
Na Mwandishi Maalum
Tanzania imeikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba Kilimo bado kinaendelea na kitaendelea kuwa tegemeo la maisha ya waafrika wengi. Na kwa umuhimu huo, Kilimo kinatakiwa kupewa kipaumbele cha pekee wakati wa majadiliano kuhusu maeneo mapya yanayotarajiwa kuwa sehemu ya Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu ( SDGs).
Hayo yameelezwa na Injinia Mbogo Futakamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Usalama wa Chakula na Ushirika wakati alipoongoa Ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Tatu cha Kikundi kazi kilichokuwa kikijadili kuhusu SDGs kilichomalizika mwishoni mwa wiki hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
“Tunapoendelea na majadiliano haya kuhusu malengo mapya ya maendeleo endelevu, lazima tukumbuke kwamba Kilimo ni sehemu ya maisha ya waafrika wengi. Uchumi imara na endelevu, maendeleo endelevu na uondoaji wa umaskini utawezekana tu ikiwa kilimo kitaendelea kupewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa miuondo mbinu ya kisasa ya kuboresha kilimo” akasema Naibu Katibu Mkuu.
Ni kwa sababu hiyo, akasema Tanzania imeridhika kwa kuona kwamba maeneo ya kilimo, usalama wa chakula na lishe bora, mmomonyoko wa udongo, ukame na kuongezeka kwa jangwa, upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka yalikuwa yamepewa kipaumbele cha kujadiliwa katika Kikao hicho cha Tatu.
Naibu Katibu Mkuu, akasema maeneo hayo na mengine yanayohusiana na hayo, yanapashwa kutoa malengo ya wazi kwaajili kufunguza fursa kubwa za kilimo kwa Afrika.
“ Ili Afrika iwe na fursa kubwa ya kunufaika na kilimo tunahitaji ongekezo katika upatikanaji wa misaada ya mikopo, fursa na haki sawa kwenye masoko ya kimataifa na biashara, kuboresha uzalishaki kwa ekari, uwekezaji katika miundo mbinu ya kilimo ikiwa ni pamoja na mifumo ya umwagiliaji, utafiti, usindikaji viwandaji ili kupunguza upotevu baada ya mavumo”.
Akasisitiza kwamba, majadiliano kuhusu maeneo hayo yamefanyika wakati muafaka na hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 75 ya watanzania wanaishi maeneo ya vijijini na kutegemea kilimo kwa maisha yao.
Kwa mujibu wa Naibu Katibua Mkuu, Hata taarifa ya Banki Maendeleo ya Afrika kuhusu mkatakati wa sekta ya kilimo kwa mwaka 2010-2014 imeeleza wazi kwamba kilimo kinasaidia maisha ya asilimia 80 ya idadi ya watu katika Afrika na kinatoa ajira kwa karibu asilimia 60 ya watu katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi.
Akizungumzia kuhusu suala la ardhi, Injinia Futakamba, alieleza kwamba ni jambo lililowazi kwamba idadi ya watu Afrika inaongezeka, hali inayochangia kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi nzuri kwaajili ya kilimo, ufugaji, uvuvi na hata ufugaji wa nyuki.
kuhusu lishe, Naibu Katibu Mkuu, alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelipa suala la lishe kipaumbele katika ajenda zake za maendeleo, hususani katika maeneo ya kilimo na afya kwa ujumla.
Akabainisha kwamba mkazo kuhusu lishe bora umelekezwa kwa watoto wakimo watoto wachanga na wenye umri wa kwenda shule, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha. Na kwamba juhudi hizo zinatekelezwa kwa pamoja kati ya Wizara za Kilimo, Afya, Elimu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Itakumbukwa kwamba Tanzania ni kati ya nchi 30 ambazo zimechaguliwa kuongoza majadiliano hayo kuhusu maeneo mapya yanayopashwa kuwa sehemu ya malengo mapya ya maendeleo endelevu. Vikao Kazi hivi vinafanyika nchini ya Uenyeviti Wenza wa Wawakilishi wa Kudumu wa Kenya na Hungary, Mabalozi Macharia Kamau na Csaba Korosi.
Kikao cha nne cha kazi kinatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 17-19 mwezi wa Sita mwaka huu ,ambapo itatarajiwa maeneo ya upatikanaji wa ajira bora na salama kwa wote, ulinzi wa jamii, vijana, elimu na utamaduni, afya na idadi ya watu yatajadiliwa
Kikao cha kwanza kabisa kilifanyika mwezi wa March huku Kikao cha pili kilifanyika mwezi Aprili ambapo maeneo kuhusu utawala bora, usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake na haki za binadamu na suala la kuondoa umaskini na maendeleo endelevu yalijadiliwa.
No comments:
Post a Comment