HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIFUNGUA WARSHA YA WAZI (OPEN DAY) KUHUSU MFUMO MPYA WA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KITAIFA YA KIPAUMBELE, VIWANJA VYA MAKUMBUSHO YA TAIFA, DAR ES SALAAM, MEI 24, 2013
Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri;
Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi;
Makatibu Wakuu;
Dkt. Philip Mpango, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango;
Washirika na Wadau wa Maendeleo;
Viongozi wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma;
Viongozi wa Kidini na Sekta Binafsi;
Wataalamu Elekezi kutoka PEMANDU na Mckinsey;
Washiriki wa Maabara;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana:
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika Warsha ya Wazi kuhusu mfumo mpya unaoanzishwa na Serikali wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kitaifa ya kipaumbele. Warsha hii inatoa nafasi ya pekee kwa wananchi kushiriki na kutoa mawazo yao jinsi ya kuboresha mfumo huo unaopendekezwa. Ni Warsha ya kuelimishana, kubadilishana mawazo na kufahamishana mipango na mambo ambayo Serikali inatarajia kuyafanya katika siku za karibuni.
Namshukuru Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Philip Mpango, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, viongozi na watumishi wote wa Tume ya Mipango kwa kuandaa Warsha hii mahsusi. Kwa namna ya pekee nawashukuru pia wataalamu wa PEMANDU na McKinsey kwa kushirikiana vizuri na wataalam wetu katika kila hatua ya safari hii ambayo Serikali yetu imeianza.
Ndugu Wananchi;
Kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo sio jambo geni hapa nchini. Ni jambo ambalo tumelifanya tangu tupate Uhuru na tunaendelea nalo. Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ilianza na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo mwaka 1961 – 1964. Mpango huo uliainisha maadui watatu wa maendeleo ambao ni umaskini, ujinga na maradhi. Mikakati mbalimbali na mipango madhubuti ya maendeleo ilibuniwa ili kupambana na maadui hao. Baada ya hapo ukaja Mpango wa Maendeleo wa Miaka 15 wa mwaka 1964 – 1980, uliokuwa umegawanywa katika vipindi vitatu vya utekelezaji vya miaka mitano mitano.
Baadhi yenu mtakumbuka kuwa utekelezaji wa vipindi viwili vya mwanzo ulikuwa wa kuridhisha. Hata hivyo, utekelezaji wa kipindi cha mwisho cha Mpango ule, yaani kati ya mwaka 1975 – 1980, ulikuwa duni mno. Utekelezaji wake ulivurugwa sana na changamoto za wakati ule kama vile kupanda sana bei ya mafuta, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (1977) na Vita ya Kagera. Mambo haya yalisababisha fedha zetu nyingi kutumika kuagiza mafuta, kujenga taasisi zetu wenyewe na kutetea mipaka ya nchi yetu. Rasilimali kidogo tuliyonayo ikaenda huko badala ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto zilizojitokeza, Serikali iliamua kuanzisha mpango mwingine wa maendeleo wa muda mrefu wa mwaka 1981 – 2000. Kwa bahati mbaya mpango huo nao haukutekelezwa kufuatia kuendelea kudorora kwa uchumi. Kati ya mwaka 1981 na miaka ya 90 mwanzoni, Serikali ilianza kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Tukawa na National Economic Survival Programme (NESP) mwaka 1981 – 82 na Structural Adjustment Programme (SAP) mwaka 1982 – 1985. Mipango hiyo haikutekelezwa vizuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa rasilimali za kutosha. Kati ya mwaka 1986 – 89, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ikaanza kutekeleza programu ya kwanza ya kufufua uchumi (ERP – I). Ya pili ikafuatia kati ya mwaka 1989 – 1992.
Mwaka 1994 Serikali ikaanza kuandaa mpango wa maendeleo wa muda mrefu utaowezesha kuzikabili changamoto mpya kufuatia mageuzi ya kiuchumi na kijamii yaliyokuwa yanaendelea nchini na duniani kwa ujumla. Kazi hiyo ilikamilika mwaka 1999 na kuzinduliwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025. Malengo ya Dira hiyo ni kuleta maendeleo ya haraka nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Maana yake ni kwamba wananchi wawe na chakula cha kutosha, huduma ya elimu na afya iliyo bora iwafikie watu wengi zaidi, vifo vya watoto na akina mama vipungue, wastani wa kuishi uongezeke, maji safi na salama yapatikane kwa wote, uhalifu upungue na umaskini uliokithiri usiwepo kabisa na pato la wastani la Watanzania liwe zaidi ya dola za Kimarekani 3,000. Vile vile pawe na maendeleo ya viwanda, matumizi ya teknolojia na sayansi yaongezeke, miundombinu ipanuke na uchumi ukue kwa asilimia 8 au zaidi.
Ndugu Wananchi;
Juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zote ikiwemo na hii ninayoiongoza mimi zimeleta mafanikio ya kutia moyo. Kwa mfano, uchumi wa nchi umekua kwa wastani wa asilimia 7 kwa miaka kumi iliyopita, mfumuko wa bei upo chini ya asilimia 10, mapato ya ndani yameongezeka, mauzo ya nje yameongezeka na hifadhi ya fedha za kigeni imeongezeka pia. Hata hivyo, idadi ya Watanzania walio maskini bado ni kubwa hususan umaskini wa kipato. Vile vile bado hatujafanikiwa kufikia malengo katika maeneo mengi tuliyojiwekea. Hata tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 tuliyofanya mwaka 2000 imethibitisha hivyo. Hatuendi kwa kasi inayotakiwa na utekelezaji wake siyo wa kuridhisha. Matokeo yake tupo nyuma ya hatua tuliyotakiwa kuwa. Kwa mfano, kwa upande wa safari ya kuelekea pato la wastani la watu kuwa dola 3,000 mwaka 2025, tulitakuwa tuwe tumefikia dola 995 mwaka 2010. Lakini ilikuwa tumefikia dola 545 tu. Kwa ukuaji wa uchumi, tulitakiwa tuwe asilimia 8, lakini tulikuwaasilimia 7.
Zipo changamoto nyingi za ndani na nje, zilizofanya tusifikie malengo hayo: Kubwa ni misukosuko ya uchumi wa dunia, uhaba wa rasilimali fedha na ufuatiliaji mdogo katika utekelezaji wa miradi iliyoainishwa kuleta maendeleo. Aidha, mipango na mikakati ya maendeleo ilikuwa na vipaumbele vingi kwa wakati mmoja wakati rasilimali za utekelezaji wake ni kidogo. Hali hii haikutuwezesha kujielekeza ipasavyo kwenye maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na kwa haraka.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutafakari yote haya, tukafikiria namna ya kuweza kufikia malengo yetu ya Dira ndani ya muda uliobakia. Hivyo, tukaamua kuja na Mpango ya Maendeleo wa Muda Mrefu wa Miaka 15 ambao utatekelezwa katika awamu tatu za miaka mitano mitano. Katika Mpango wa Kwanza Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12-2015/16), maeneo yaliyopewa kipaumbele ni Miundombinu, Kilimo, Viwanda, Huduma za jamii na Uendelezaji Rasilimali Watu na Utalii, Biashara na Huduma za Fedha. Changamoto kubwa ikabaki kuimarisha mfumo wetu wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili kuleta matokeo ya haraka. Kuendelea kufanya vilevile tulivyokuwa tukifanya kusingeweza kuleta mabadiliko tuliyokuwa tunayataka katika utekelezaji wa mipango yetu. Ilibidi tubadilike, ikiwezekana tukimbie pale ambapo wengine wanatembea.
Ndugu Wananchi;
Tukiwa katika hali hiyo ya kutafakari cha kufanya, mwezi Mei, 2011 ikawa bahati mimi kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa “Langkawi International Dialogue” uliofanyika mjini Kuala Lumpur, Malaysia. Katika mkutano huo, Serikali ya Malaysia iliwasilisha mada jinsi inavyoendesha na kusimamia utendaji wake ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma kwa jamii. Mimi na viongozi wenzangu tuliohudhuria mkutano huo tulivutiwa sana na mfumo wa utendaji wa Malaysia na tukadhamiria kujifunza zaidi kutoka kwao. Tukaomba watusaidie. Bahati nzuri Serikali ya Malaysia ikakubali ombi letu na kuandaa warsha maalum mwezi Novemba, 2011. Ujumbe wa Tanzania kwenye warsha hiyo ya aina yake uliongozwa na Dkt. Philip Mpango. Waliporudi, tukaamua kuwa na sisi tuanze kutumia utaratibu wa Malaysia wa “Matokeo Makubwa Sasa” ama kwa Kiingereza “Big Results Now”.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mfumo wa “Big Results Now” hapa nchini ulianza kwa kuainisha maeneo sita yenye uwezo wa kutupatia matokeo makubwa kwa haraka. Maeneo hayo ni nishati, elimu, maji, miundombinu, kilimo na utafutaji fedha. Kazi ya kuchagua maeneo sita ya kwanza nayo haikuwa rahisi. Tulibishana sana katika kuchagua vipaumbele vichache lakini vyenye kuleta matokeo makubwa. Hatimaye tukafanikiwa. Vipaumbele hivi vinabeba msingi wa kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa Tanzania kwa ujumla na kuchochea ustawi wa maisha bora kwa wananchi.
Hatua ya pili ikawa ni kufanya uchambuzi wa kina kupitia awamu ya kwanza ya maabara (lab) kama alivyoeleza Katibu Mkuu Kiongozi. Kazi hiyo ilitekelezwa kwa wiki sita mfululizo na wataalam wetu zaidi ya 300 kutoka nyanja na sekta mbalimbali na kukamilika tarehe 05 Aprili, 2013. Nawapongeza sana kwa kazi hiyo kubwa na moyo wao wa kujitolea. Tumeandaa ratiba ya utekelezaji kwa kila mradi na programu ikionyesha kazi zilizopangwa kufanywa, mtekelezaji-husika na muda na kukamilisha kazi.
Katika mfumo huu, Mawaziri na Watendaji katika Wizara na Idara watapimwa kwa vigezo vilivyo wazi na ninyi wananchi mtapata fursa ya kuvijua vigezo hivi pamoja na matokeo ya upimaji. Hapatakuwa na siri. Hii itarahisisha usimamizi wa utendaji kwa maana Waziri au Katibu Mkuu atajifunga yeye mwenyewe kimaandishi na ataweka saini yake kwenye vigezo ambavyo atapimwa navyo na wananchi mtashuhudia matokeo ya upimaji huo.
Ndugu Wananchi;
Ili kuweza kuratibu vyema shughuli za ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mfumo huu mpya, nimeunda chombo maalum kitakachokuwa chini ya Ofisi yangu ambacho kitajulikana kama President’s Delivery Bureau (PDB). Kazi zake za msingi zitakuwa ni pamoja na: kupanga na kuendesha shughuli za uchambuzi wa kina wa kimaabara (labs); kuandaa mikataba ya kupima utendaji kazi wa Mawaziri kwenye miradi na programu za maendeleo katika wizara zao; kwa kushirikiana na Tume ya Mipango kuishauri Serikali kuhusu maeneo machache ya kipaumbele yenye kuleta matokeo ya haraka (National Key Results Areas); kusaidia sekta binafsi kuwekeza kwenye maeneo hayo; na kufanya tathmini huru ya utendaji kwa viongozi wote hususan Mawaziri katika utekelezaji wa maeneo muhimu ya kitaifa.
Ndugu Wananchi;
Tumefanya kazi kubwa sana ya kuandaa na kuainisha maeneo ya kimkakati na kuyaandalia programu za kina kwa ajili ya utekelezaji. Lakini tumeona ni vyema kuwashirikisha wadau na wananchi katika jambo hili kubwa. Ndio maana tupo hapa kuhakikisha kuwa wananchi kwa ujumla wenu mnapata fursa ya kuchangia katika miradi na programu hizo kwa maendeleo ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Zangu;
Sitapenda kuongea sana hivyo basi nataka niwape nafasi wananchi na wadau wengine mliofika hapa kupita katika eneo la kila maabara na kupata maelezo ya kina kutoka kwa wataalam. Muwe huru kuuliza maswali, kujenga hoja, kutoa maoni na kukosoa na kuboresha katika kila maabara. Baada ya kupata maoni yenu ndipo tutaboresha na kwenda kuyafanyia kazi maoni na ushauri wenu.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kusema hayo, napenda kutamka kuwa Warsha ya Wazi imefunguliwa rasmi. Ninawatakia majadiliano mazuri na uchangiaji mzuri.
Asanteni kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment