Friday, May 24, 2013

HAKUNA JAMII ITAKAYOACHWA NYUMA KIMAENDELEO-TANZANIA


Balozi Ramadhan Mwinyi Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa Mkutano wa Kudumu wa 12 wa Masuala ya Wazawa, katika mchango wake kuhusu mada ya utafiti uliofanywa kuhusu Ujasiri, Maarifa ya Jadi na Kujenga uwezo Jamii ya Wafugaji katika Afrika, Mwakilishi huyo ameeleza kwamba Jamhuri ya Muungano inajukumu la kuwaletea maendeleo wananchi wake wote na kwamba katika hakuna jamii itakayoachwa nyuma. Akasisitiza haja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa na wadau wengine kushirikiana na Serikali kufanikisha azma hiyo lakini pia kuunga mkono hatua na maamuzi inayoyachukua kwa manufaa ya wananchi wake na taifa kwa ujumla. Nyuma ya Balozi ni Bi. Ellen Maduhu Afisa wa Ubalozi .

Na Mwandishi Maalum

 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kwamba inajukumu kubwa  la kuhakikisha kuwa mipango yake ya maendeleo endelevu inamfikia kila mwananchi na kwamba hakuna jamii itakayo achwa nyuma.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania imeitaka  Jumuiya ya Kimataifa na wadau wengine kushirikiana na Serikali katika kufanikisha azma  yake hiyo, lakini pia kutambua  kuwa maamuzi mbalimbali inayoyachukua  yanafanyika kwa nia njema.

Hayo yameelezwa na   Balozi  Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa   Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  alipokuwa akichangia  majadiliano ya mada   ya utafiti kuhusu Ujasiri, Maarifa ya Jadi na Kujenga Uwezo wa Jamii ya  Wafugaji katika Afrika.

Mada  hiyo ni sehemu ya mada kadhaa zikiwa zao afya, elimu, haki za binadamu, ujasiliamali, vijana mila na tamadu ambazo zimekuwa zikijadiliwa kwa nyakati tofauti katika Mkutano wa Kudumu wa 12  Kuhusu Masuala ya Wazawa. ( Forum on Indigenous Issues) Mkutano huu ambao ulianza mapema wiki hii unafanyika chini ya  usimamizi wa  Baraza la Uchumi na Maendeleo ya Jamii la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC).

Washiriki wa  mkutano  huu wapatao 2000 wanatoka katika Asasi zisizo za kiserikali  wakiwamo wawakilishi kutoka   baadhi ya  taasisi za kifedha kama  Banki ya Dunia,  Banki ya Maendeleo ya Afrika  na  Banki  ya Maendeleo ya Asia.

“Tunaendelea na  jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wetu ili kuhakikisha kwamba hakuna jamii inayoachwa nyuma kama ambavyo imeainishwa katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) na  kutafsriwa katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa na  mipango migineyo” akasisitiza Balozi Mwinyi.

Hata hivyo akasema licha ya jitihada hizo za serikali , bado kuna baadhi ya jamii chache ambazo zenyewe zimeamua    kudumisha  mila, tamaduni na   maisha yao ya jadi .

Akasema  jamii hizo ni zile ambazo hazifahamiki sana katika Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo kwa jamii ya  wamasaai.

Akizungumzia  masuala ya upatikanaji na ugawaji wa ardhi kwa wananchi  zikiwamo  jamii ambazo mfumo wa maisha yao unategemea zaidi ardhi na mali asili nyingine. Balozi   Mwinyi amewaeleza washiriki  wa  mkutano huo wakiwamo washiriki kutoka Tanzania, kwamba serikali imejiwekea sheria na taratibu zinazosimamia ugawaji wa ardhi.

Akafafanua  kwa kueleza kwamba kwa sheria na taratibu za Tanzania,   Hati ya umiliki wa Ardhi katika  ngazi ya kijiji hutolewa  kwa wanajamii ambao wanaishi au wamekusanyika katika  muundo wa kijiji ambao unatambuliwa rasmi.

“ Kwa mujibu wa sheria zetu, ni kijiji ndicho kinatambuliwa kisheria  kama chombo huru kinachosimamia masuala ya ardhi ambapo cheti  cha ardhi hutolewa kwaajili ya matumizi ya jamii nzima”. Akasema
Na kuongea “ Hata hivyo    kuna  baadhi ya maeneo  hasa yale ya wawindaji ambapo kama idadi ya  jamii ile haikukidhi  matakwa ya kisheria ya kuwa na hadhi ya kijiji kutokana na uchache wao, bado kwa mfano,  mwaka 2011, serikali ilitoa  hati ya  kumiliki ardhi kwa ya Wahdzabe ingawa walikosa sifa  zinazotakiwa kisheria.

Akizungumza kuhusu  Loliondo ambako  Serikali imetangaza kutenga eneo la kiasi cha kilomita za mraba 2,500  za ardhi kwaajili ya  makazi ya jamii ya wamasaai  na ambao wengi wao hawakuwa na ardhi na hivyo kuwa katika mazingira magumu. Balozi amesisitiza kwamba uamuzi huo ulikuwa ni wa manufaa kwa jamii hiyo na taifa kwa ujumla.

Akasema kuwa  eneo  lililotengwa   ni kubwa  kuliko nchi ya Luxeburg au  mara nne ya eneo la nchi ya Singapore ambayo ina kilomita za mraba 624.

Akasema eneo  lililobaki la kilomita za mraba 1,500 Serikali imelitenga kwaajili ya hifadhi ya wanyama pori na mazalia yake ikiwa ni  pamoja na uhifadhi wa uoto wa asili, utunzaji wa vyanzo vya maji  kwa maendeleo endelevu ya  uwepo wa wanyama na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu akafafanua Zaidi kwa kueleza kwamba, uamuzi huu wa Serikali wa kutenga ardhi kwaajili ya matumizi ya binadamu na mengine  kwa hifadhi ya  maliasili ni uamuzi halali na wala haukuanza sasa  bali umekuwa  ukitekelezwa katika  maeneo mengi ya nchi tangu uhuru.

No comments: