Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi Mdogo wa China aneyeishi Zanzibar,Bibi Chen Qiman,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akifuatana na Balozi Mdogo wa China aneyeishi Zanzibar,Bibi Chen Qiman,(kushoto) mara baada ya mazungumzo yao alipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana.Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesifu juhudi za China za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi Mdogo wa China Mhe. Bibi Chen Qiman, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Bibi Chen kuwa China imekuwa na mashirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika maeneo kadhaa ya maendeleo.
Alisema kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria ambao ulianzishwa na waasisi wa pande mbili hizo na kuzidi kuendelezwa hadi hivi leo.
Dk. Shein alieleza kuwa ujio wa Rais Xi Jinping nchini Tanzania nao umezidi kuimarika na Zanzibar ilisaini makubaliano kadhaa na hatimae kufanya mazungumzo na kiongozi huyo.
Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kwa kutoa pongezi na shukurani kwa madaktari kutoka China ambao wanafanyakazi katika hospitali za Unguja na Pemba kwani wameweza kutoa huduma nzuri na bora kwa wananchi.
Kwa upande wa ujenzi wa hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba, Dk. Shein alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuimarisha huduma za afya kwa wananchi ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa.
Dk. Shein alieleza kuwa China imeweza kusaida miradi kadhaa ikiwa ni kuipatia Zanzibar mikopo nafuu katika kuendeleza miradi ukiwemo mradi wa maji safi na salama, ujenzi wa viwanda mbali mbali mnamo miaka ya sabini.
Aidha, alieleza kuwa China imeweza kuunga mkono na kusaidia sekta ya habari, nafasi za masomo, afya, miundombinu, ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume unaoendelea, mawasiliano pamoja na miradi mengineyo na kutumia fursa hiyo kupongeza kwa kukamilika mradi wa mitambo ya redio huko Dole ambapo nchi hiyo imesaidia.
‘China na Zanzibar zinahistoria kubwa za mashirikiano hivyo kuna kila sababu ya kuyaimarisha na kuyatunza …..Pia, natumia fursa hii kutoa pongezi na shukurani zangu kwako wewe Mhe. Chen kwa juhudi zako binafsi katika uendelezaji wa miradi kadhaa hapa Zanzibar”,alisema Dk. Shein.
Nae Balozi Chen alimuaahidi Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa jumla kutokana na uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati ya pande hizo.
Alisema kuwa China inazithamini sana juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuhakikisha maendeleo yanaimarika kwa kila upande na ndio maana imekuwa ikitoa ushirikiano mwema katika kuimarisha sekta za maendeleo na za kiuchumi.
Balozi Chen alimueleza Dk. Shein kuwa Rais Xi Jinping amefurahishwa sana na ziara yake nchini Tanzania hivi karibuni na kutoa shukurani kwa viongozi na wananchi kutokana na mapokezi na makaribisho makubwa aliyoyapata akiwa nchini Tanzania.
Alieleza kuwa hatua hiyo imedhihirisha wazi kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na China sambamba na juhudi za pamoja katika kuimarisha sekta za kimaendeleo.
Aidha, Balozi Chen alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imo katika kutekeleza miradi mbali mbali ambayo baadhi yake inatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa Wizara husika ukiwemo ujenzi wa skuli ya Msingi ya Mwanakwereke pamoja na mradi wa taa za barabarani zinazotumia mwaganza wa jua huku akiahidi kuanzwa kwa miradi mengine mbali mbali ambayo ni mipya baada ya kusainiwa makubaliano.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment