Monday, March 18, 2013

TAARIFA KWA UMMA toka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma


Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1).

Ni vyema tufahamu kuwa chimbuko la Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma limetokana na maboresho yanayoendelea katika Utumishi wa Umma nchini.  Ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na marekebisho ya Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 toleo Na. 2 la mwaka 2008 ambapo katika Vifungu Na. 4.6  na 6.6. vya Sera hiyo ambavyo vimetamka kuwepo kwa chombo maalum cha kushughulikia mchakato wa masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma.

Kwa mujibu wa Sheria, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ndio chombo pekee chenye wajibu wa kutekeleza  majukumu yafuatayo:-
i)        Kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za wataalam.
ii)      Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazojitokeza katika Utumishi wa Umma.
iii)    Kuhusisha wataalam maalum ili kushirikiana nao kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji.
iv)    Kuwashauri waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa ajira.
v)      Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo na wataalam weledi kwa madhumuni ya kurahisisha rejea za ujazaji wa nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma.

Aidha, kwa mujibu wa Sera hiyo, kuwepo kwa chombo hiki kutaziwezesha Mamlaka za Ajira nchini (zikiwemo zile za Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa) kubaki na majukumu yake ya msingi (Core functions) ambayo yameainishwa katika uundaji wa Mamlaka hizo ili kuongeza ufanisi. 

Kutokana na maelezo hayo hapo juu ni vyema wananchi wote wakafahamu kuwa ni kosa kwa mtu au taasisi yeyote ile kuchukua Matangazo ya Sekretarieti ya Ajira na kuyafanyia marekebisho au kuandaa matangazo mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kupotosha umma ilihali wakijua wazi kuwa taarifa hizo wanazozichapisha au wanazoziandika katika mitandao ya kijamii hazijatolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Tumefikia hatua ya kusema haya kutokana na baadhi ya taarifa zinazohusu mchakato wa ajira hususani uwepo wa nafasi za kazi zilizopo katika baadhi ya mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira ametoa matangazo hayo.
Moja ya tangazo hilo  la kughushi na lenye nia ya kupotosha umma ni lile lililoko katika anwani hii www.eastafricajobscareer.com lenye kichwa cha habari kinachosomeka Tangazo la Kazi Utumishi Tanzania June 2013” ambalo linaonyesha Mwisho wa kupokea barua za maombi ni tarehe 8 Juni, 2013”.
Katibu anapenda kuwasisitizia wadau wote wa Sekretarieti ya Ajira wanaotafuta kazi pindi wanapoona matangazo katika Vyombo mbalimbali vya Habari wajiridhishe kwa kuthibitisha taarifa hizo kama ni za kweli kwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz kwa taarifa sahihi zihusianazo na ajira katika Utumishi wa Umma.
Sekretarieti ya ajira haiwajibiki na wala haitawajibika kwa Matangazo ama taarifa zozote zinazohusiana na mchakato wa ajira  katika Utumishi wa Umma ambazo haijazitoa rasmi.
Imetolewa 18 Machi, 2013 na 
                                     Katibu,
Ofisi ya Rais,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Maktaba Kuu ya Taifa/Barabara ya Bibi Titi Mohammedi
S. L. P 63100, Dar Es Salaam.
Simu; +255 22 2153517
Nukushi; +255 22 2153518
Barua pepe: katibu@ajira.go.tz
                                    Tovuti; www.ajira.go.tz
  
Aidha, kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini kwa Barua pepe; gcu@ajira.go.tz  au
Simu; 255-687624975

No comments: